DAR ES SALAAM
NA MWANDISHI WETU
Mapinduzi makubwa ya kimfumo na uwekezaji wa kutosha kwenye teknolojia mpya kumesaidia kupanua upatikanaji wa huduma za intaneti nchini katika kipindi cha muongo mmoja.
Takwimu za kisekta zinaonyesha kuwa miaka kumi iliyopita watumiaji wa intaneti walikuwa 520,000 tu ikilinganishwa na mamilioni wanaofaidi mtandao huu sasa hivi.
Chama cha Kampuni Zinazotoa Huduma ya Intaneti Tanzania (TISPA) kinasema kuongezeka kwa matumizi ya intaneti nchini kumechochea ubora wa maisha kupitia kukua kwa sekta muhimu za biashara, uzalishaji, huduma za jamii, burudani, michezo na hata siasa na utawala bora.
Meneja Mkuu wa TISPA, Mzee Boma, anasema pamoja na kusambaa sana kwa intaneti, bado maeneo mengi ya vijijini hayajafikiwa kikamilifu. Mkurugenzi Mkuu wa Halotel Tanzania, Nguyen Anh Son, anataja sababu kubwa ya huduma hizo kutofika vijijini kuwa ni kutokana na changamoto ya uwekezaji ingawa kampuni yao imesambaza miundombinu husika nje ya miji mikubwa.
Kati ya mwaka 2013 na 2018, watumiaji wa intaneti kwa nchi nzima waliongezeka kwa wastani wa milioni 2.8 kwa mwaka na kufikia milioni 23.1 kutoka milioni 9.3. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasema matumizi ya intaneti yaliongezeka zaidi ya maradufu katika kipindi hicho kutokana na mchango wa simu na vifaa vya mkononi visivyounganishwa na nyaya.
Na simu mtelezo, maarufu kama simu janja, ndizo zilizochangia sana kupatikana kwa maendeleo haya ambayo yanawafanya Watanzania zaidi ya 40 kati ya 100 kuwa na uhakika wa intaneti hivi sasa. Mwaka jana, idadi hii ilikuwa watu 43 ikilinganishwa na watu 21 mwaka 2013 na chini ya watu 10 kati ya mwaka 2000 na 2009.
“Simu mtelezo ni aina ya simu ya mkononi isiyokuwa na vitufe bonye na badala yake hutumia kingamuzi kilichofichwa ndani ya kioo. Neno simu janja linatumika lakini si rasmi na bado tunapokea mapendekezo ya jina la simu hizi,” mtaalamu wa lugha kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Richard Mtambo, ameliambia JAMHURI wiki
iliyopita.
Kabla teknolojia kuwezesha simu kuwa na intaneti, watu wengi waliikosa huduma hii kutokana na mfumo wa upatikanaji wake uliokuwepo. Hiyo ni kabla ya 2006/07 wakati intaneti ilipatikana sana maofisini na kupitia intaneti kefu tu.
Mamlaka husika zinakiri kuwepo ongezeko la matumizi ya simu janja katika Nyanja mbalimbali kadiri siku zinavyoendelea. Kwa sasa simu hizi zinakadiriwa kuwa asilimia 30 ya simu zote za mkononi na ndani ya miaka mitano ndizo zinatarajiwa kuwa nyingi sokoni.
Wadau wa sekta ya mawasiliano wanasema ifikapo mwaka 2024 idadi ya simu janja nchini itafika milioni 30 na kuchochea kwa kiasi kikubwa matumizi ya intaneti. Pia watumiaji wake wanatarajiwa kuongezeka zaidi baada ya kampuni za simu kuja na simu za kiganjani za kawaida zenye sifa za simu mtelezo.
Hii ni sehemu ya mkakati wa kuongeza matumizi ya data ambalo ndilo eneo linalolipa sana kwenye biashara ya huduma za simu za mkononi. Mkuu wa Idara ya Mauzo na Usambazaji wa Vodacom Tanzania, George Lugata, anasema umaarufu wa simu janja unatokana na wigo wake mpana wa matumizi yake.
“Simu janja inafanya kazi kwa kutumia mfumo ambao ni sawa na ule wa kompyuta. Ina uwezo wa intaneti ambayo unaweza kutumia kupiga simu za video na sauti, kutuma picha na video mbalimbali na kupakua zana mbalimbali,” Lugata ameliambia JAMHURI hivi karibuni.
Kwa mujibu Lugata, ongezeko la matumizi ya simu janja pia linachangiwa na ubunifu unaofanyika kwenye sekta, uliosaidia kuleta bidhaa mbalimbali sokoni zenye unafuu na kutoa fursa kwa watu wengi kujiunga na ulimwengu wa kidijitali.
“Mfano mzuri ni simu ya Smart Kitochi ambayo tumeiingiza sokoni hivi karibuni. Ni simu ya bei nafuu yenye sifa zote za simu janja ikiwa na lengo la kuwapa fursa watumiaji wengi. Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa kizuizi kikubwa katika matumizi ya simu janja ni upatikanaji wa nyenzo,” anafafanua.
Lugata anasema pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ili kuhakikisha kuwa mitandao ya 3G na 4G inapatikana kote nchini, bado kuna matumizi duni ya intaneti kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa watu wengi kumudu manunuzi ya simu janja.
Kwa Tigo Tanzania, kupungua kwa bei kuna mchango mkubwa kwenye matumizi ya simu janja na intaneti kwa ujumla. Meneja Mawasiliano wa kampuni hiyo, Woinde Shisael, anasema zaidi ya asilimia 90 ya watumiaji wa intaneti wanatumia simu janja kuupata mtandao huo, kwa hiyo suala la gharama halikwepeki.
“Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa smartphones zikishuka bei na kufikia dola 30 za Marekani, (kama Sh 69,000), watu wengi zaidi wataweza kuzimiliki, hivyo kutumia intaneti zaidi,” aliliambia gazeti hili hivi karibuni.
“Kuzinduliwa kwa Kitochi 4G Smart na Tigo ni mkakati wa makusudi wa kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia intaneti hapa nchini, hasa intaneti ya 4G yenye kasi kubwa,” Woinde anasema na kuongeza kuwa bila kuwepo teknolojia za 3G na 4G hali ingekuwa tofauti kabisa.
Simu mtelezo na matumizi ya intaneti Tanzania
Ripoti ya mawasiliano ya Juni mwaka 2019 ya TCRA inaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti nchini imefikia zaidi ya watu 23,142,960 na kati ya hao 22,281,727 wanatumia mtandao huo kupitia simu zao za mkononi.
Nayo Kampuni ya GlobalData Technology ya Uingereza inasema ifikapo mwaka 2024, idadi ya simu janja nchini itafika milioni 30, hali inayotarajiwa kuongeza matumizi ya intaneti maradufu kwa sababu zifuatazo:
Uwepo wa teknolojia husika (3G, 4G & 4G+).
Uwepo wa simu za mkononi zinazowezesha matumizi ya intaneti.
Uelewa wa kidijitali. Watu wanazidi kuelimika katika matumizi ya intaneti.
Uwepo wa majukwaa rafiki kama mitandao ya kijamii (facebook, twitter nk).
Kampuni za simu kutoa vifurushi vinavyowezesha wateja kutumia intaneti kwa
urahisi zaidi.
Maudhui sahihi.
“Lengo letu ni kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa kidijitali. Tunaamini kwamba
jamii iliyounganishwa kidijitali ina nguvu, watu wake wanaweza kupata taarifa muhimu,
huduma za afya mtandaoni, elimu, tahadhari za maafa na zaidi,”
GEORGE LUGATA,
MKUU WA IDARA YA MAUZO NA USAMBAZAJI – VODACOM TANZANIA.
Mwisho