Mwaka 2011 nililala kwenye hoteli ya mjini Moshi, chumba kilirembwa na dari iliyonakshiwa kwa jasi inayojulikana zaidi kama gypsum.
Ilikuwa ni jasi iliyokaa muda mrefu na ilikuwa inapukutika kwa urahisi. Siku iliyofuata niliiugua, nikapatwa na homa kidogo na mafua, ingawa hali hiyo mbaya haikuendelea kwa siku nyingi.
Niliamini kwa uhakika kabisa wakati huo kuwa ni kuvuta kwa hewa iliyoathiriwa na vumbi vumbi ya jasi iliyokuwa inapukutika ndiyo iliyosababisha kuugua kwangu.Hali mbaya haukudumu sana kwa hiyo sikulazimika kutafuta matibabu.
Nimekumbuka tukio hili kwa sababu hivi karibuni nimemsikia mtu mmoja akisema kuwa anapolala kwenye chumba kilichorembwa na jasi, huamka akiwa anaugua homa.
Ukichunguza utengenezaji wa kuta za jasi, zinazotumika zaidi kwenye ujenzi wa nyumba nchini Marekani, unapata mwanga kidogo wa sababu inayoweza kuchangia kuleta athari kwa binadamu.
Jasi ni mchanganyiko wa madini ya jasighafi iliyopashwa moto kufikia nyuzijoto 150 na baadaye kupoozwa na kuloweshwa kwa kiasi fulani. Baada ya hapo inachanganywa na karatasi na kemikali mbalimbali.
Mchanganyiko huu, ukiwa bado mbichi, unabanwa kati ya karatasi mbili ngumu. Baada ya muda karatasi zenye mchanganyiko huu zinaingizwa kwenye tanuri, na kuchomwa na kuwa ngumu na imara kiasi cha kutosha kuweza kutumika kwenye ujenzi.
Bidhaa inayotoka ni ngumu na kavu, lakini iliyobana kemikali kadhaa. Naamini kuwa tatizo linazuka bidhaa inapopasuka au kupata unyevunyevu na kusababisha baadhi ya hizo kemikali kuingia kwenye mzunguko wa hewa tunayopumua.
Nchini Marekani tatizo kama hili limejitokeza. Marekani yenyewe ni mtengenezaji mkubwa wa bidhaa za jasi kwa matumizi ya ujenzi, ikiwa inazalisha mita za mraba bilioni 3.9 kwa mwaka.
Ni mahitaji ambayo kwa kiasi kikubwa yameweza kutimizwa na viwanda vya chini Marekani.
Hata hivyo kati ya mwaka 2004 na 2007 ongezeko la ujenzi pamoja na maafa ya mafuriko yaliongeza mahitaji ya bidhaa kupita uwezo wa viwanda, na Marekani ikalazimika kuagiza kuta za jasi kutoka China.
Marekani ikamaliza tatizo la upungufu wa jasi lakini ikazua tatizo lingine. Baada ya muda ilibainika kuwa zile jasi za China zinavujisha kemikali aina ya salfa.
Sababu za kuvuja kwa kemikali hazikujulikana mara moja lakini inaaminika kuwa kulisababishwa na mchakato duni wa uzalishaji unaotumika kwenye viwanda vya China.
Wamarekani waliodai kuathirika na bidhaa hizo kutoka China walilalamika juu ya harufu mbaya ndani ya nyumba, kuharibika kwa vyuma vilivyokaribiana na jasi, pamoja na athari za kiafya.
Kutokana na tatizo hili kati ya nyumba 60,000 na 100,000 nchini Marekani ziliathirika na baada ya kufunguliwa shauri mahakamani, kampuni zilizozalisha bidhaa hizi zililazimika kulipa fidia zilizokadiriwa kufikia mabilioni ya dola za Marekani ikiwa ni pamoja na kurekebisha upya kasoro zilizosababishwa na bidhaa zao.
Utafiti mwingine uliyofanyika nchini Marekani unabaini tatizo la ziada. Uchunguzi wa bidhaa za jasi za Marekani na China ulibaini kuwa bidhaa hizo zinavujisha zebaki kwa viwango tofauti.
Kati ya bidhaa zilizochunguzwa, bidhaa za China zilikuwa zina viwango vya juu zaidi vya kuvuja.
Zebaki ni kemikali yenye athari hatarishi kwa binadamu.
Athari hizi ni pamoja na hatari za kukua kwa watoto ambao hawajazaliwa na wachanga; sumu kwenye mifumo ya neva, ya kumeng’enya na kinga za mwili, mapafu, figo, ngozi, na macho.
Zipo dalili kuwa matumizi ya jasi ni hatari kwa afya ya binadamu, lakini athari hizi zinakuzwa zaidi kwa sababu ya nafasi ya China kwenye uchumi wa dunia.
Kwa sasa China inajulikana kama kiwanda cha ulimwengu. Ni nchi inayoongoza kwa kuwa inatengeneza bidhaa zinazohudumia sehemu kubwa ya masoko ya dunia.
Zipo sababu nyingi zinazofanya China kushika nafasi hiyo, ikiwa ni pamoja na mishahara midogo, mfumo imara wa ushirikiano kati ya wazalishaji, na kutotoza kodi bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.
Lakini sababu kuu ni ya mamlaka za China kushindwa kushurutisha kutimizwa kwa vigezo mbalimbali vya uzalishaji, kama vigezo vya usalama wa bidhaa.
Nchi zilizoendelea kama Marekani zina uwezo mkubwa wa kukinga raia wake wasiathirike na bidhaa ambazo si salama kwa binadamu, kama ambavyo ilivyojitokeza kwa jasi zilizoingizwa kutoka China. Siamini kama kwenye nchi zinazoendelea tunapata kinga hiyo.
China ina bidhaa ambazo zinazingatia uwezo na matakwa ya kila mnunuzi. Akija mfanyabiashara Mmarekani na vigezo vya usalama vya Marekani atauziwa bidhaa inayozingatia vigezo hivyo na bei ya juu kidogo ambayo mfanyabiashara Mtanzania hataimudu.
Matokeo ni kuwa Watanzania tutaletewa bidhaa ambazo pengine hazifikii vigezo vya jasi inayopelekwa Marekani.
Swali ambalo halina jibu ni kufahamu tatizo ni pana kiasi gani. Siyo Watanzania wote wanaotumia jasi katika ujenzi wa nyumba zao.
Lakini kwa wale wanaotumia nina wasiwasi kuwa wanalala na kuamkia ndani ya tatizo ambalo athari zake zitaibuka baada ya muda. Kulala siku moja kwenye chumba chenye athari hizi ni suala moja. Je kulala kwenye mazingira hayo kwa miaka kumi mfululizo?
Viashiria ya kwamba kuna tatizo vipo. Vimeonekana Marekani, nimevishuhudia Moshi, na nimevisika Musoma. Kama siyo tatizo kubwa nchini kwetu mamlaka husika zinapaswa kutoa tamko kuthibitisha hilo. Kama ni tatizo basi zinapaswa kuchukuliwa hatua za haraka kuweka taratibu zitakazolinda afya za muda mfupi na muda mrefuza watumiaji.