WAZIRI Mkuu wa Nchi, Kassim Majaliwa Majaliwa amezikumbusha taasisi na mashirika yote ya Serikali yaliyopo kote nchini Tanzania ambayo  yanahudumia watu zaidi ya 100, kutekeleza bila shuruti agizo lake la kuitangaza Desemba 31, 2024 kuwa siku ya mwisho kwa matumizi ya mkaa na kuni kwenye shughuli za mapishi.

Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati akihutubia wananchi kwenye Tamasha la Azimio la Kizimkazi 2024, linalofanyika kwa mara ya pili Ruangwa mkoani Lindi ikiwa ni mara baada ya kuzinduliwa kwake mapema mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan, Kizimkazi Visiwani Zanzibar.

Aidha, Majaliwa amezitaja taasisi zinazohusika na agizo hilo kuwa ni pamoja na taasisi zote zenye kuhudumia watu zaidi ya mia moja ikiwemo majeshi mbalimbali, shule za bweni za binafsi na za serikali, magereza pamoja na wazabuni wanaopika vyakula vya zaidi ya watu 100 ambapo lengo ni kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ili kuondokana na athari za kiafya na uharibifu wa misitu unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.