Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma
Imeelezwa kuwa ifikapo mwaka 2030 watu zaidi ya milioni 10 watakufa kwa kila mwaka kutokana na matumizi holela ya dawa za mifugo ambayo yamekuwa yakisabaishwa vimelea vya magonjwa kujenga usugu.
Aidha matumizi ya dawa kiholela ya dawa hasa za aina ya antibaiotiki huweza pia kuwaathiri binadamu kutokana na kula mabaki ya dawa hizo kwenye vyakula vinavyotokana na wanyama.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023,
Amesema hali hiyo ni tatizo kubwa linaloikabiri dunia kwa sasa na wafugaji wanapaswa kuzingatia ushauri unaotolewa ili kulidhibiti.
“Inakadiriwa kwamba kufikia 2030, watu zaidi ya milioni 10, watakufa kila mwaka kutokana na dawa kushidwa kuwatibu kwani vimelea vya magonjwa vitakuwa vimejenga usugu unaotokana na matumizi holela ya dawa kwa binadamu na mifugo”ameeleza.
Amesema jumla ya sampuli 163,722 kutoka kwa wanyama mbalimbali zilipokelewa na kufanyiwa uchunguzi na utambuzi wa magonjwa.
Dk.Bitanyi,amesema kuwa njia za uchunguzi zilizotumika ni pamoja na kuchunguza vimelea vya magonjwa kwa kutumia hadubini kuchunguza viaashiria vya uwepo wa kinga dhidi ya kimelea kwenye damu kwa kutumia ELISA na kipimo cha juu kabisa cha uchunguzi wa aina ya kimelea kwa kutumia vinasaba yaani PCR.
“Katika kipindi cha miaka mitano kati ya 2017/2018 hadi Septemba 30, 2022 jumla ya sampuli 163,722 kutoka kwa wanyama mbalimbali zilipokelewa na kufanyiwa uchunguzi na utambuzi wa magonjwa.
“Magonjwa muhimu yaliyotambuliwa kwa wingi ni mdondo/kideri, ndigana baridi, ndigana kali, ndui kwa kuku, homa ya nguruwe, kimeta, ugonjwa wa kutupa mimba, homa ya mapafu ya ng’ombe, homaya mapafu ya mbuzi, kichaa cha mbwa, sotoka ya mbuzi na kondoo”amesema Dk.Bitanyi
Kuhusu uzalishaji na usambazaji wa chanjo za mifugo, amesema Wakala inatekeleza jukumu hilo kupitia Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyoko Kibaha mkoani Pwani.
Amesema hivi sasa TVI, Kibaha inazalisha chanjo saba na uzalishaji kwa mwaka 2021/2022 ulifika dozi milioni 65.
“Kwa kuwa chanjo haziwezi kuzalishwa na kusubiri wateja, kiwanda huzalisha kulingana na mahitaji ya soko. Uwezo kamili wa uzalishaji wa chanjo ni zaidi ya dozi milioni 100, kwa mwaka ambao hata hivyo bado haujafikiwa kutokana na uhitaji wa soko kuwa chini”amesama