Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), limetangaza matokeo ya darasa la saba ya mwaka huu ambapo watahiniwa milioni 1.07 wamefaulu kwa kupata madaraja A na B na C.
Akitangaza matokeo hayo leo Desemba 1, 2022 Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi amesema kuwa jumla ta watahiniwa wote walikuwa milioni 1.34 kati ya hao wasichana ni 558,825 ambao ni sawa na asilimia 78.91 na wavulana ni 514,577 sawa na asilimia 80.41.
Amesema kitakwimu kuna kupungua kwa ufaulu kwa asilimia 2.35 ingawa idadi ya watahiniwa waliofaulu imeongezeka kwa watahiniwa 165, 600 sawa na asilimia 18.24 ikilinganishwa na mwaka jana.
Hata hivyo ameongeza kuwa NECTA limevifungia vituo 24 vya mitihani baada ya kubainika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.
Amezitaja shule hizo ni Kadama shule ya msingi iliyopo Chato- Geita, Rweikiza (Bukoba), Kilimanjaro shule ya msingi (Arusha) Sahare (Tanga), Ukerewe (Mwanza), Peaceland (Mwanza), Karume (Kagera), Al-hikma (Dar es Salaam),Kazoba (Kagera), Mugini (Mwanza).
Nyingine ni Busara (Mwanza), Jamia (Kagera), Winners (Mwanza), Musabe (Mwanza), Elisabene (Songwe), High Challenge (Arusha), Tumaini (Mwanza), Olele (Mwanza), Mustlead (Pwani), Musabe ( Mwanza) na St.Anne Marie ( Dar es Salaam ), Rweikiza (Kagera). Moregas (Mara), Leaders (Mara), Kivulini (Mwanza) na St Severine (Kagera)
“Vituo hivi vimefungiwa kwa mujibu wa kifungu 4(8) cha kanuni za mitihani mwaka 2016 hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani ya kitaifa,” amesema.
Amesema kuwa mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi uliofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu.