Magenge ya matapeli kwenye biashara ya madini, yameibuka na kuendesha shughuli zake bila hofu.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwapo kwa matukio ya utapeli na kuifanya sifa ya Tanzania izidi kuchafuka mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Mwaka 2013, JAMHURI lilichapisha majina na kampuni za matapeli wa madini; hatua iliyoifanya Serikali ikunjue makucha kupambana na magenge hayo.
Wiki kadhaa zilizopita, raia wawili wa Singapore wametapeliwa dola 45,000 (shilingi zaidi ya milioni 90), baada ya kuuziwa dhahabu feki.
Wageni hao, Yang Jun Ho Joshua na Thiam Seng Oh, wanasema wametapeliwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wamiliki wa kampuni ya Tamasha Mining (T) Ltd ya jijini Dar es Salaam. Haieleweki vema mahali ziliko ofisi za kampuni hiyo kama ni Tangi Bovu au Mikocheni.
Wanasema kwenye utapeli huo wahusika wengine ni polisi na maofisa wa forodha. Polisi aliyehusika kwenye utapeli huu na kukamatwa anatoka Kituo cha Msimbazi, lakini kutoakana na mtandao ulivyo, wenzake wa Oysterbay wamemfichia siri. Uzoefu unaonesha kuwa mara kadhaa utapeli kwenye biashara ya madini hujumuisha mtandao mkubwa kuanzia kwa matapeli wenyewe, polisi, Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hata maofisa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama.
Kituo cha Polisi Oysterbay, kinatajwa kuongoza katika matukio ya utapeli, huku kesi nyingi, ama zikiishia hapo, au zikivurugwa na askari na maofisa katika kituo hicho.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, ameahidi kutoa taarifa kutokana na tukio hilo na mengine ya aina hiyo yanayoendelea nchini.
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki, ameulizwa na JAMHURI juu ya kuwapo kwa matukio kadhaa ya polisi kushiriki utapeli huo, lakini ‘amerusha mpira’ kwa Msemaji wa Jeshi hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Advera Bulimba, ambaye hata hivyo hakuweza kupatikana.
Matukio mengi na makubwa ya utapeli wa madini yamekuwa yakitokea Wilaya ya Kinondoni, na hivyo kukifanya Kituo cha Polisi Oysterbay kuwa kwenye orodha ya sehemu zinazotajwa kuufanya uhalifu huo ushamiri.
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), amekuwa akitaka wanunuzi na wasafirishaji madini nje ya nchi kufuata sheria za nchi, ikiwa ni pamoja na wageni kupata ushauri na maelekezo juu ya biashara ya madini kutoka kwenye vyombo vinavyotambulika kisheria.
Kampeni kubwa iliyofanywa na TMMA kuanzia mwaka 2013 ilisaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa matukio ya utapeli kwenye biashara ya madini. Balozi za mataifa mbalimbali hapa nchini zimekuwa zikiwaelekeza raia wake wanaotaka kufanya biashara ya madini hapa nchini kuwasiliana na TMAA ili kukwepa kutapeliwa.
Hata hivyo JAMHURI lilivyowatafuta wahusika wa kampuni inayodaiwa kuwatapeli Rais wa Singapore, gazeti hili lilizungumza na mmoja wa watuhumiwa, ambaye hakutaja jina lake lakini alikuwa anatumia namba +255 743176431, hapa chini ni sehemu ya mahojiano baina ya JAMHURI na mmoja wa watuhumiwa;
JAMHURI: Kuna taarifa kwamba kampuni yenu ‘imewapiga’ Wasingapore, mnatuhumiwa kuwatapeli kwa kushirikiana na Polisi, je, ni kweli?
TAMASHA MINING: Sio kweli…hao watu walikuwa ni wezi, umesema wanatoka Singapore? Nao walikuwa ni ‘wapigaji’ na sisi tukawashtukia. Wanataka nini sasa? Kwa hiyo wanataka ninyi mwandike gazetini ili warudishiwe pesa zao?
JAMHURI: wanataka mamlaka zijue kinachoendelea,
TAMASHA MINING: Hizi ripoti wamewatumia wakiwa Singapore ama bado wako hapa nchini? Hao watu hao…hiyo biashara hakuna, walete ushahidi kwamba ‘walipigwa’ hawawezi kutuhumu tu.
JAMHURI: Wanasema ninyi mmeshirikiana na Polisi Oysterbay, mmewatepeli, kwani wao (Wasingapore) walitaka kuwatepeli namna gani?
TAMASHA MINING: Sasa kama mtu anakuambia kwamba amekuja kununua mawe kwako, wakati amekuja na visa ya utalii na sio ya biashara….Pesa hizo walituma wapi? Nikisikia gazeti limeandika nitashitaki hilo.
JAMHURI: Unatutisha ili tusiandike?
TAMASHA MINING: Hapana, isipokuwa tunataka msiandike maana jambo lenyewe halina ushahidi, mfano wewe hapo ulipo niseme kwamba umeniibia dola milioni 50. Walete vielelezo la sivyo tutawashtaki.
JAMHURI: Kwa nini wawataje ninyi kama watekelezaji wa mpango wa kuwaibia?
TAMASHA MINING: hao watu walitaka kufanya biashara na sisi, lakini tukagundua kwamba hao ni wezi, halafu wanafanya biashara ya dawa za kulevya, sisi tukawa wajanja. Maana na wenyewe ni wapigaji, halafu wameingia na document mbilimbili.
JAMHURI: Mlivyobaini kwamba walikuwa na rekodi ya uhalifu, mlitoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama?
TAMASHA MINING: tulifungua kesi, ila wakawahi kukimbia
JAMHURI: Walikimbia namna gani wakati walitakiwa kupanda ndege?
TAMASHA MINING: Wakati tunakwenda kutoa taarifa pale Polisi na Idara ya Uhamiaji, Uwanja wa ndege tukakuta wameshaondoka nchini, maana hao watu walikuwa na hati za kusafiria mbili mbili.
JAMHURI: Kwani ninyi ofisi yenu iko wapi?
TAMASHA MINING: Sisi ofisi yetu iko Mikocheni.
JAMHURI: Sasa kama ofisi yenu iko Mikocheni, kwa nini hamkutoa taarifa kituo cha Polisi kilichoko jirani, mpaka mkaamua kwenda Uwanja wa ndege?
TAMASHA MINING: Tuliamua kwenda huko, maana ndiko walitakiwa kupita, lengo letu lilikuwa ni kuwazuia wasiondoke nchini lakini tulichelewa, wakaondoka.
Aliyetapeliwa asimulia
Nilishawishiwa na raia wa Korea, Geigeun Yoon, ili nikanunue dhahabu nchini Tanzania. Alinitumia picha za dhahabu aliyoipata Tanzania.
Niliwasiliana na mmoja wa marafiki zangu wa Singapore na akasema wako tayari kununua dhahabu nikiwa nao kama ni halisi.
Raia wa Korea aliwasili Singapore akiwa na sampuli ya dhahabu, tukathibitisha kuwa ni dhahabu halisi baada ya kuifanyia vipimo.
Kwa kuwa sampuli ilibainika kuwa dhahabu halisi, tukafanya mawasiliano kwa njia ya Whatsapp na Bwana Thomas mwenye namba +255743176431 –ambaye ni mmoja wa matapeli. Akatufanyia taratibu za safari kuja nchini Tanzania Mei 19, 2016.
Bwana Thomas, siku tunawasili Tanzania alitusaidia kubadilishana dola 45,000 za Marekani kwa dhahabu. Tukakubaliana yeye na bosi wake aliyemtaja kwa jina la Dk. Yusufu Musa Ali kuiyeyusha dhahabu yote ili iwe katika mkuo (bar) chini ya uangalizi wa maofisa forodha wa Tanzania.
Kampuni (ya kitapeli) ikatuma dereva na gari lililotupeleka katika hoteli inayoitwa SeaScape, ambako walikuwa wameweka miadi ya vyumba vyetu vya kulala.
Asubuhi iliyofuata, dereva wa matapeli aliyejulikana kwa jina la Bwana Frank, aliyekuwa akitumia simu yenye namba +255743184257 alifika kutuchukua akiwa na Bwana Thomas, ili twende katika ofisi zilizoko eneo la Tangi Bovu (Dar es Salaam).
Tulipofika katika ofisi hizo ambazo ni nyumba iliyoko katika mtaa ambao haupitilizi, tulikuta kuna watu wachache; mmoja kutoka Congo na wengine wakawa wanazungumza na sisi, lakini hatukujua dhima yao ilikuwa nini; jumla yao ilikuwa watu 12 hivi ndani ya ofisi.
Tulizungumza na Dk. Yusufu Musa Ali taratibu za usafirishaji dhahabu kutoka Tanzania kwenda Hong Kong.
Akatuonesha hati za usajili wa kampuni na cheti cha kodi, na akatuambia kuwa nyaraka zote zilikuwa halali; na kwamba maofisa forodha watakuwa hapo ofisini kuhakiki utaratibu mzima wa ununuzi wa dhahabu hiyo. Maofisa hao wa forodha wakaleta ofisini mzigo wa dhahabu ghafi wenye uzito wa kilogramu 30 wakiwa wamesindikizwa na polisi.
Ofisa forodha aliyehusika kwenye mpango huu aliuliza kama nina nyaraka halali za kuniwezesha kununua dhahabu na pia akauliza jina la kampuni yangu. Namna mambo yalivyokuwa, na namna walivyokuwa makini, nikaamini kuwa kweli walikuwa maofisa wa Serikali.
Bwana Yoon na rafiki yangu mwingine kutoka Singapore, Bwana Jovince, wakawa wanaangalia hatua zote zilivyokuwa zikiendelea.
Ofisa wa forodha akatuambia kuwa tunapaswa kulipa kodi ya Serikali ya asilimia 4, na kwamba napaswa kufanya hivyo haraka kwa vile itachukua siku mbili hadi tatu kwa ajili ya mchakato wa nyaraka zote za usafirishaji mzigo, na hizo nyaraka akakabidhiwa Dk. Yusufu.
Tukakubaliana miongoni mwetu kuwa yaelekea mchakato unaoendelea ni halisi, maofisa wa polisi na wale wa forodha walionekana ni halisi kutokana hata na sare walizovaa. Tukaona hakuna hatari ya kukabidhi fedha kwa kuamini vyombo vya Serikali vilikuwa vikisimamia shughuli hii.
Baada ya hapo, tukasubiri hadi dhahabu ilipoyeyushwa na kuwa katika umbo la mkuo na kuwekwa kwenye kasiki; kwa kuambiwa kuwa kilogramu 28 za mkuo huo wa dhahabu iliyofungiwa kwenye kasiki ingepelekwa ofisi za forodha katika Uwanja wa Ndege, na kilogramu 2 Dk. Yusufu akatukabidhi tuwe nazo. Kuona hivyo tukamkabidhi dola 45,000 za Marekani kama amana kwa hizo kilogramu 28.
Akasema angerejea kwetu akiwa na nyaraka zilizokwishathibitishwa ndani ya siku chache, na tungekuwa tayari kusafiri kwenda Hong Kong. Maofisa forodha wakaondoka wakiwa na polisi na mtu aliyebeba kasiki lenye mkuo wa dhahabu yenye uzito wa kilogramu 28.
Bwana Yoon, mimi, Jovince, Bwana Thomas na Dk. Yusufu, tukaenda katika ofisi za Yusufu. Tulipoketi tukaomba atupatie stakabadhi- iandikwe jina la kampuni yetu pamoja na kiasi cha amana ya dola 45,000 za Marekani; pamoja na kumtaka tuweke maandishi ya kilogramu mbili za dhahabu tulizokuwa nazo.
Bwana Thomas akaandaa nyaraka zote kwa kutumia kipakatarishi (laptop) chake. Bwana Thomas, akamtaka dereva Frank, atupeleke hotelini ili tutunze dhahabu yetu kwenye kasiki wakati tukiendelea kusubiri ankara na nyaraka za usafirishaji mizigo, nyaraka za kodi na vibali vya kusafirisha dhahabu.
Baada ya siku mbili za kusubiri, Bwana Thomas alitupigia simu akisema ofisa wa forodha alikuwa ofisini kwa Dk. Yusufu, na kwamba angekuja kutuchukua sote kwa ajili ya kwenda kwenye kikao. Baada ya kukutana, ofisa forodha akatueleza kuwa mkuu wake wa kazi alikuwa amekataa kuweka saini kwenye nyaraka za mzigo kutokana na msisitizo wa Serikali mpya wa kutaka kodi zote za usafirishaji mizigo zilipwe kwa mkupuo, na siyo kidogo kidogo.
Tukaambiwa kuwa Dk. Yusufu alikuwa na kilogramu 100 za dhahabu katika himaya ya maofisa forodha, na kuwa alitakiwa alipe kwanza kodi kwa mzigo wote wa kilogramu 100 ili kuwezesha mzigo huu mpya wa kilogramu 30 kusafirishwa nje ya Tanzania.
Ofisa forodha akatupatia siku sita kufanya malipo mengine ya kodi kwa kilogramu 100 za dhahabu. Tukazungumza na Dk. Yusufu, na kumwuliza kwanini hali hii itokee, na iweje tatizo hili liwe letu. Hapo tukawa tumeanza kuhisi kutapeliwa.
Raia wa Congo aliyeuza dhahabu ghafi kwa Dk. Yusufu, akaingia katika chumba tulimokuwa akiwa amekasilika na kutueleza anataka dhahabu yake ghafi au arejeshwe fedha zake.
Nilishitushwa kwa kuona suala hili likinilemea mimi. Dk. Yusufu akasema angeweza kumalizana naye na akaniomba namna ninavyoweza kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha malipo ya kodi kwa kilo 70. Naye akasema alikuwa tayari kuhangaika kupata fedha kwa ajili ya malipo ya kiasi hicho, lakini akatoa hadhari kuwa malipo hayo yangechukua muda kwa vile alipaswa apate fedha kutoka kwenye biashara zake nyingine.
Tulirejea hotelini tukijua tumeshatapeliwa. Nikazungumza na Bwana Jovince na Bwana Yoon, na pia nikaomba bosi wa Bwana Yoon kama tunaweza kuendelea na mpango huu. Wakasema wangejitahidi kupata kiasi kilichopungua cha kodi kwa kilogramu 70 ambacho ni dola 106,000 za Marekani na kwamba wangesafiri kuja kukutana na sisi. Nikawaambia “Hapana”, na nikawaeleza kuwa naamini tumetapeliwa.
Nikamweleza bosi wa Bwana Yoon kwamba namfahamu Mtanzania mwingine anayeitwa Edwin aliyekuwa akiniendesha, na ningemwomba ushauri wa namna ya kuendelea na suala hili.
Nilimpigia simu Edwin, akaja akakutana na sisi muda wa saa 5. Nikamwomba ahakikishe taarifa hizi haziwafikii watu wengine kwa kuhofu maisha yetu yalikuwa hatarini. Nilimweleza yaliyotusibu.
Akasema tutakuwa na matatizo kwa vile hatukuwa na viza ya kufanya biashara, na nilikuwa nimetunza kilogramu mbili za dhahabu bila kuwa na vibali kisheria.
Akasema tungewindwa au kusakiziwa kwa maofisa wa Serikali ambao wangetutia mbaroni. Akasema ana polisi ambaye ni rafiki yake anayeitwa James (James Kasusura), mwenye cheo cha Afisa Mrakibu wa Polisi (SSP). Akasema kwamba angenisaidia kunipa ushauri wa nini cha kufanya.
Akanishauri pia nimpelekee zile kilogramu 2 za dhahabu kwa maelezo kuwa ana rafiki yake ambaye ni dalali aliyeidhinishwa ambaye anaweza kutupeleka kwenye maduka ya dhahabu nchini Tanzania kupima.
Tukakubali Edwin siku inayofuata atuendeshe twende kupima dhahabu tuliyokuwa tumetunza kwenye kasiki.
Tukafungua kasiki na tukaenda kuipima katika maduka mbalimbali ya dhahabu. Mikuo minne ya dhahabu, kila mmoja ukiwa na gramu 500 ikabainika kuwa ni shaka tu.
Edwin akatueleza kuwa tunapaswa kukutana na rafiki yake (SSP James Kasusura) na kusikia ana maoni gani.
SSP James akajitambulisha kwetu na akanipatia kadi yake iliyoonesha kuwa kweli ni polisi. Tukamweleza yaliyotusibu. Akasema tunaweza kuondoka au kufungua kesi polisi na kuweza kuwakamata matapeli; akiamini kulikuwa na fursa ya kuwakamata, lakini hakuwa na hakika ya kuzipata dola 45,000. Tulikubali ushauri wa SSP James.
SSP James akatutaka tukutane naye ofisi za Polisi na kuonana na OCD wa Kituo cha Polisi Oysterbay ambako mpango wa kuwakamata matapeli ungeandaliwa.
Siku iliyofuata Edwin alitupeleka Kituo cha Polisi Oysrebay na SSP James alikuwapo. Akazunngumza na OCD juu ya kesi yetu; na OCD akasema tungeendelea na kesi, lakini Jumamosi angekuwa na mkutano, na kwamba Jumapili angefanya operesheni ya kuwakamata matapeli hao.
Baada ya mkutano na OCD, James alitupakia kwenye gari lake hadi katika eneo kuliko na ofisi za matapeli ili kuweza kumwonesha mahali nyumba/ofisi ilipo. Tulienda hadi kwenye ofisi na katika mtaa ulio nyuma ili kama kutakuwa na tapeli atakayekimbia wakati wa operesheni ya kuwakamata, kuwe na polisi maeneo hayo wa kuwatia mbaroni.
Siku ya operesheni ambayo ilikuwa Jumapili, tukawa na makubaliano na OCD na SSP James kwamba wajibu wangu ni kuhakikisha Bwana Thomas au dereva Frank ananipeleka katika ofisi, pindi tukiwa ndani na kujiridhisha kuwa matapeli wote wako ndani, nitapeleka ujumbe kwa SSP James na hivyo wataingia ndani ili kuwakamata.
Tukapanga na Bwana Thomas tuwe na mkutano Jumapili ambako Thomas hatimaye akawa tayari kwa kazi hiyo baada ya kuwa tumezungumza kwa simu kwa saa tatu asubuhi, lakini tulichelewa hadi saa 5.
Baada ya kufika eneo la tukio (kwa matapeli), nikaona matapeli wote wapo, isipokuwa yule ofisa forodha niliyekutana naye awali kabisa, lakini nikapokewa na ofisa forodha mwingine.
Tukaenda kuangalia zile kilogramu 70 za dhahabu, na kukuta tayari walikuwa wameanza kuziyeyusha, na kwa mara nyingine alikuwapo yule askari polisi aliyesimamia awali.
Nikawa namfuata Bwana Jovince ili ampelekee meseji James kwamba anaweza kuingia sasa, lakini akasimamishwa ghafla na Thomas ambaye aliniambia kuwa napaswa kukimbia naye nikiwa na begi kwa vile eti kulikuwa na mtu anakuja kufanya uporaji.
Nikamsukuma pembeni na kwenda nje ya ofisi kumuona Jovince, na wakati huo OCD na SSP James pamoja na polisi mwingine wakawa langoni wakiingia ndani.
Baada ya kuingia, nikapigwa bumbuwazi kwa spidi ya wale matapeli ambao wanane kati yao waliokuwapo asubuhi ile wakitoroka kwa kuruka uzio.
Akakamatwa Dk. Yusufu, huku yule polisi mwingine akiwaachia wale wengine wote watoroke. Akaanza kuhoji badala ya kuwakamata matapeli ambao wakati huo walikuwa wamepamia ukuta wa uzio na kutokomea.
Polisi wakakamata kipakatarishi (laptop) ambacho kilitumiwa na Thomas kuandaa stakabadhi na nyaraka zikiwamo taarifa zangu za ndege, wakakamata mihuri yote ya kampuni, cheti cha usajili na hati mbalimbali za kodi.
Polisi pia wakakamata magari matatu. Katika gari moja kulikuwa na makasha mawili yenye dhahabu feki, na katika gari jingine la Dk. Yusufu kulikuwa na nyaraka za benki.
SSP James akaniambia kuwa amefurahishwa na operesheni hiyo kwa vile imekuwa yenye mafanikio, na kuwa Dk. Yusufu atafungwa miaka mingi jela ikizingatiwa kuwa ana kesi nyingine tatu za aina hiyo. Akasema usiku wangeenda nyumbani kwake ili kukusanya vielelezo zaidi au kuokoa kiasi cha fedha tulichotapeliwa.
Kesho yake asubuhi mimi, Jovince na Yoon tulienda kuonana na OCD wa Oysterbay. OCD akatueleza kuwa kesi yetu amekabidhiwa CID. Akasema mkuu wa CID aitwaye Iddy, atasimamia kesi yetu. Akatupatia namba yake +2550759885117 na kusema kama kutakuwa na jambo lolote ningeweza kumpigia kwa msaada zaidi.
Tulirejea hotelini na kusubiri tukiambiwa kuwa wale matapeli waliokimbia watakamatwa kupitia simu zao za mkononi.
Baada ya siku kadhaa za kusubiri, OCD alinipigia simu na kunitaka niende Polisi Oysterbay kumtambua polisi aliyekuwa miongoni mwa matapeli wakati wa operesheni ya kuwakamata. Nikaambiwa natakiwa niende kwenye gwaride la utambuzi ili polisi huyo aweze kushitakiwa kijeshi.
Tukaenda Polisi Oysterbay, na baada ya kusubiri kwa saa kadhaa nikaambiwa na askari aliyekuwa zamu aliyejitambulishwa kwangu kwa jina la SSP Wabassa, ambaye aliniomba radhi akisema jalada la mashitaka lilikuwa halijakamilika. Nikaombwa nifike tena kituoni kesho asubuhi.
Siku iliyofuata tulienda tena kituoni kumshuhudia polisi aliyekamatwa.
Baada ya kazi hiyo, OCD akasema anataka kuniona mimi ofisini kwake. Hapo ilikuwa ni wiki moja tayari tangu Dk. Yusufu akamatwe, lakini si CID wala OCD, aliyenieleza kilichokuwa kikiendelea.
Sikufurahishwa hata kidogo, si tu nimetapeliwa, bali sikujua wapi walipo matapeli wengine waliokimbia. Sikupewa taarifa zozote za kibenki kutoka kwenye akaunti ya Dk. Yusufu, au mrejesho mwingine wowote.
Nikakutana na OCD na akaniambia nisikate tamaa kufanya biashara katika nchi hii. Akaniomba tukutane nje ya ofisi yake hapo kituoni na kuniahidi kunitambulisha kwa wafanyabiashara ya shaba. Akanitaka nimwamini kwa maelezo kuwa mambo yatakuwa mazuri.
Nikamweleza kuwa natambua Dk. Yusufu yuko nje kwa dhamana, na kwanini hakupata kunieleza hilo jambo hata mara moja. Nikajua ameachiwa siku mbili tu akiwa anakabiliwa na kesi nyingine tatu za aina yangu. Akanijibu kuwa hapakuwapo sababu ya kuendelea kumweka rumande.
Nikamweleza kuwa Thomas alikuwa akiendelea kuwasiliana na mimi, na tunaweza kufanya operesheni nyingine ya kuwakamata matapeli waliokimbia, mimi nikasema hapana.
Kila kitu kikawa kimeharibika.
Tukamweleza OCD kuwa tulikuwa tumepanga kurejea nyumbani Singapore kwa vile tulikuwa tumekaa Tanzania kwa karibu wiki tatu.
Baada ya kurejea hotelini kwangu usiku, akanipigia simu mara mbili akinishauri nishiriki biashara ya kuchimba shaba Mpwapwa ambako yeye amewahi kufanya kazi kama OCD, na hivyo ana mtandao wa uhakika.
Kwa ufupi, uzoefu wangu Tanzania ulikuwa ni huzuni na kukatishwa tamaa.
Kwanza, nimetapeliwa katika nchi hii. Suala hili linawezaje kuwa kesi ya jinai katika mahakama wakati wahusika wana uhusiano na Serikali kwa maana ya maofisa wa polisi na maofisa wa forodha.
Pili, sikuambiwa kama naweza kwenda mahakamani, na isitoshe, jalada limefungwa.
Tatu, ni kwa namna gani OCD aliruhusu dhamana baada ya siku mbili na asinieleze.
Ndimi,
Joshua Yang Jun Hao
Utapeli biashara ya madini unavyofanyika
Biashara udanganyifu wa madini hufanyika kwa wahusika kuanza kutangaza biashara yao kupitia mtandao wa internet na kupitia kwa watu ambao wanafahamiana nao wasiojua tabia zao kwa kufahamisha wateja kuwa wao au kampuni yao wanajihusisha na biashara ya madini ya vito dhahabu cooper au madini mengine kwa njia hiyo pia hushawishi wateja kuwa wauzia madini hayo kwa bei nafuu ukilinganisha na bei ya soko.
Matapeli hao pia wanazo nyaraka halali kutoka wizara husika na pia wanakuwa na nyaraka za kughushi wateja wanapopatikana na huoneshwa nyaraka halali na madini halisi yanayojulikana kwa lugha ya kitapeli kama RUNGU. Mara nyingi wakati wa kufanya biashara matapeli hao huwa na askari kutoka Jeshi la Polisi au Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa nia ya kuwaaminisha kuwa wanafanya biashara halali.