DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Kampuni zinazouza bima kwa magari yanayosafirishwa nje ya nchi (IT) zinaendelea kufanya biashara hiyo licha ya kubainika kuwa ni utapeli.
Wakati Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ikisema stika za bima za muda kwa magari hayo zinapaswa kuuzwa Sh 28,000 kwa kila gari (ikijumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani –VAT), stika hizo zinauzwa chini ya kiwango hicho. Baadhi ya mawakala wanauza Sh 15,000.

Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita biashara hiyo imeendelea japo si kwa uwazi kama ilivyokuwa awali.
Pamoja na kuuza kwa kiwango hicho, kampuni hizo zimekuwa zikiwahadaa wateja kupitia sera zake kwa kuwaahidi kuwalipa mamilioni ya shilingi endapo watafikwa na ajali.
Mathalani, kampuni moja (jina tunalo) ambayo inauza stika hizo kwa Sh 20,000; inawaahidi wanaozinunua mambo makuu matatu: Mosi, ajali inayosababisha kifo au majeruhi, malipo yake kwa mteja ni Sh milioni 20. Pili, ajali na vifo kwa kila tukio linalohusisha idadi yoyote ya watu kiwango cha juu na cha mwisho cha malipo ni Sh milioni 60; na tatu, mali zinazoharibika kwenye ajali fidia yake ni Sh milioni 30.
“Haiingii akilini mtu aliyekata bima ya Sh 15,000 gari likipata ajali mtu akafa itolewe fidia ya Sh milioni 30. Nani akupe hizo fedha?” kimehoji chanzo chetu.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI kwa miezi kadhaa umedhihirisha pasipo shaka kuwa kwenye ajali zote za IT zinazotokea na kuondoa uhai au kusababisha ulemavu wa kudumu, hakuna kampuni ya bima iliyotoa fidia. Kwenye matoleo yajayo JAMHURI litachapisha majina ya baadhi ya watu waliokufa na waliopata ulemavu wa kudumu kwenye ajali zilizosababishwa na magari ya IT na ambao hawakuambulia fidia yoyote.
Ofisa Mawasiliano wa TIRA, Oyuke Filemon, ameulizwa kuhusu mkanganyiko huo, lakini ametetea kwa kusema magari yote ya IT yanapaswa kuwa na bima hizo zinazodumu kwa saa kadhaa.
“Malipo ya bima ni Sh 25,000 na VAT ni Sh 3,000. Jumla ni Sh 28,000. Kila gari lazima liwe na hiyo bima ili likipata ajali fidia itolewe kwa wahusika,” amesema Oyuke.
Amesema utaratibu huo ni kwa magari yote ya IT yanayosafirishwa kwenye barabara nchini hadi mipakani.

Amesema magari ya IT yanao usajili wake wa namba nne za mwisho za chesesi, na ndiyo maana zinahakikiwa kwenye mtandao wa uhakiki wa TIRA (TIRA MIS).
Oyuke ameulizwa juu ya uhalali wa malipo hayo kisheria ilhali unaojulikana zaidi ni ule wa premium na comprehensive. “Nitakupatia majibu zaidi nikiwa ofisini, leo (Jumamosi iliyopita) niko nje ya ofisi,” amesema.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini mtandao wa stika feki za bima unaowahusisha baadhi ya watendaji waandamizi katika Bandari ya Dar es Salaam, Wakala wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na kampuni za bima.
Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA) Kanda ya Kaskazini, Joe Simwanza, amezungumza na JAMHURI ofisini kwake mpakani Nakonde, Zambia na kusema utapeli huo unatishia kuua biashara ya usafirishaji wa magari yanayokwenda nchini humo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Mamia ya magari ya IT yanayopata ajali njiani yanatelekezwa. Madereva wanaopona hunyofoa stika za bima na kutoweka. Mabaki ya magari hayo yako katika vituo vya polisi na kwenye yadi zilizoko Mbala, Zambia.
Wastani wa magari 300 ya IT yanasafirishwa kwenda nje kupitia Bandari ya Dar es Salaam kila siku.
Bima zinazouzwa hazina viwango maalumu vya malipo, badala yake kilichopo ni makubaliano kati ya muuzaji na mnunuzi.
JAMHURI tumenunua baadhi ya bima hizo kwa Sh 15,000, 20,000 na Sh 25,000 kwa kila stika. Pia tumenunua bima ya COMESA (Umoja wa Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika) kwa Sh 40,000. Tanzania ilijitoa katika umoja huo mwaka 1999.

Msimamizi wa uuzaji wa stika za COMESA ni Shirika la Bima la Taifa (NIC). Mwenye dhamana hiyo aliyejulikana kwa jina la Holo, amekataa kuzungumza kwa masharti kuwa hadi apate kibali kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Samwel Kamanga. Mkurugenzi huyo yuko nje ya nchi kikazi.
Stika zinauzwa kama ‘njugu’ katika maeneo yote yanayozunguka Bandari ya Dar es Salaam na katika vibanda vilivyopo Mnara wa Saa, Water Front, Gate No. 2, Dawasa, Mnazi Mmoja na Kariakoo.
Fedha zinazotokana na utapeli kwenye stika za bima ni mapato ya mtandao mahususi wenye nguvu na ushawishi.
Baadhi ya wahusika tuna majina na vyeo vyao, lakini kwa sababu za kitaaluma tunaendelea kuwahifadhi hadi tutakapozungumza nao.
Miongoni mwao ni baadhi ya watendaji waandamizi katika Bandari ya Dar es Salaam, SUMATRA na mfanyakazi mmoja mwanamke katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Mwanamke huyo ana watoto wake wawili wanaofanya kazi ya uwakala wa kununua na kuuza magari ughaibuni.
Uchunguzi huu umefanywa kwa ushirikiano kati ya Gazeti la JAMHURI na Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).