Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Msako mkali uliopewa jina la ‘Operesheni Serengeti’ uliofanywa na Polisi wa kimataifa dhidi ya wizi na utapeli mitandaoni umefanikiwa kuwanasa watu 1,006; JAMHURI linaripoti.
JAMHURI limeelezwa kwamba Operesheni Serengeti imefanyika katika mataifa 19 barani Afrika na kuokoa mamilioni ya dola za Marekani, huku ukiwanusuru maelfu ya raia wema kupoteza mali zao.
“Ni umahiri wa hali ya juu ulioonyeshwa na maofisa wa Shirika la Polisi la Kimataifa (INTEPOL) kwa kushirikiana na Taasisi ya Ushirikiano wa Polisi Afrika (AFRIPOL) na kusambaratisha magenge ya matapeli wa mitandaoni,” anasema mmoja wa maofisa walioshiriki Operesheni Serengeti.
Jijini Dar es Salaam, maofisa wa Interpol na Afripol walifanya upekuzi katika nyumba kadhaa za kupanga (apartments), nyingi kama si zote zikikaliwa na raia wa kigeni hasa kutoka Nigeria.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa ‘apartments’ zilizopo maeneo ya Masaki, Mikocheni, Mbezi Beach, Victoria, Regent na Sinza ndiyo viota vya matapeli wa mtandaoni vilivyokumbwa na upekuzi wa ‘Operesheni Serengeti’.
“Hawa jamaa mchana hawaonekani mitaani. Wanajifungia ndani wakifanya utapeli kwa kutumia simu au kompyuta.
Giza likishaingia, ndipo wanatoka kuzunguka katika kumbi za starehe,” anasema mtoa habari wetu aliyeshiriki operesheni.
Anasema wakiwa kwenye starehe, raia hao wa Nigeria hujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi na wasichana wa Kitanzania na kuwatumia ‘kutakatisha’ fedha walizoiba mitandaoni kwa kuwarubuni kuziingiza kwenye akaunti zao, kisha kuzitoa kwa ajili ya kufanyia starehe.
Upekuzi uliofanyika ulikamata rundo la vifaa vya kielektroniki vinavyotumika kufanya vitendo vya utapeli.
Kwa mujibu wa taarifa ya Interpol ya Novemba 26, 2024, ‘Operesheni Serengeti’ ilifanyika kuanzia Septemba 2 hadi Oktoba 31, mwaka huu.
“Waathirika 35,000 wametambulika na karibu Sh bilioni 436 zimegundulika kuwa zimetapeliwa katika mataifa mbalimbali (barani Afrika),” inasomeka sehemu ya taarifa ya Interpol.
Interpol inasema taarifa za kiintelijensia walizokuwa nazo ndizo zilizofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wa utapeli na wizi wa mitandaoni.
“Kutoka kwenye utapeli wa aina tofauti, sasa ni utapeli wa mitandaoni. Huu unazidi kuongezeka na unapaswa kutiliwa maanani. Operesheni Serengeti imeonyesha jinsi gani tunaweza kufanikiwa endapo tutafanya kazi kwa ushirikiano.
“Kukamatwa kwa matapeli hawa walau kunawapunguzia maumivu waathirika wa utapeli. Na huu ni mwanzo tu, tutaendelea kuwasaka popote pale walipo duniani,” anasema Katibu Mkuu wa Interpol, Valdecy Urquiza.
Anapongeza ushirikiano kati ya maofisa wa polisi wa kimataifa na sekta binafsi zikiwamo kampuni zinazotoa huduma za intaneti katika nchi husika baada ya kukubali kusaidia uchambuzi wa kiintelijensia.
Kampuni hizo ni Cybercrime Atlas, Fortinet, Group-IB, Kaspersky, Team Cymru, Trend Micro na Uppsala Security.
Akizungumza na JAMHURI, Mkuu wa Kitengo cha Interpol nchini, Gemini Mushi, amesema ‘Operesheni Serengeti’ imefanyika lakini hakutaka kueleza kwa undani, kwa kuwa: “Mimi si Msemaji wa Jeshi la Polisi.”
‘Operesheni Serengeti’ hadi nje ya mipaka
Mbali na Tanzania, ‘Operesheni Serengeti’ imefanyika katika mataifa ya Algeria, Angola, Benin, Cameroon, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Gabon, Ghana, Kenya, Mauritius, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia, Zambia na Zimbabwe.
Zaidi ya miundombinu na mitandao 134,089 ya uhalifu mtandaoni imevunjwa kupitia ‘Operesheni Serengeti’, iliyowalenga matapeli wanaofanya wizi unaotokana na ulaghai wa barua pepe za kibiashara, utapeli wa kidijitali na udanganyifu mtandaoni; vitendo vilivyoainishwa katika ripoti kuu ya tishio la uhalifu wa mtandao Afrika kwa mwaka huu.
Nchini Kenya, Operesheni Serengeti iling’amua kuwapo utapeli wa dola za Marekani milioni 8.6 uliofanyika baada ya matapeli kudukua mifumo ya benki na kuhamisha fedha kwenda Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Nigeria na China.
Watu zaidi ya 12 wamekamatwa kutokana na kuhusika katika matukio hayo.
Watu wengine wanane; raia watano wa China na watatu wa Nigeria wamekamatwa nchini Senegal baada ya kuendesha utapeli wa dola milioni sita za Marekani mtandaoni uliowaathiri watu 1,811.
Upekuzi uliofanywa na Interpol katika nyumba walimokuwa wakiishi ulikamata laini 900 za simu za mkononi, dola 11,000, simu, kompyuta mpakato na nakala za vitambulisho vya waathirika wa utapeli.
Huko Nigeria mtu mmoja amekamatwa kwa makosa ya kufanya utapeli wa mtandaoni wa takriban dola 300,000, akiwarubuni watu kwa kuwaambia kuwa atawapatia fedha za kimtandao (cryptocurrencies).
Cameroon nako si salama kwani mamlaka nchini humo zinadai kulinasa genge la wahalifu lililokuwa likifanya utapeli wa mtandaoni katika nchi saba tofauti.
Genge hilo lilikuwa likiwahadaa waathirika wa vitendo hivyo kulipa kiingilio kisha wanaahidiwa kupata fursa za ajira au mafunzo.
Baadaye waathirika walikuwa wakitekwa na kupewa masharti kwamba ili waachiliwe huru inawabidi wawaingize wenzao katika mfumo wa utapeli. Hadi genge lilipokamatwa lilikuwa limeshatapeli dola 150,000.
Nako nchini Angola, mamlaka zimefanikiwa kulikamata genge lililokuwa linaendesha mchezo wa kasino mtandaoni na kuwatapeli wacheza kamari kutoka Brazil na Nigeria kwa kuwalaghai kuwaongezea sehemu ya kiwango cha ushindi wanachokipata endapo watawashawishi wengine kucheza.
Baada ya ‘Operesheni Serengeti’, watu 150 wamekamatwa, simu zaidi ya 100 na kompyuta 200 nazo zimekamatwa.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Uganda kwa sasa inafanya uchunguzi wa wizi wa takriban dola milioni 17 zilizoibwa hivi karibuni kutoka benki na wadukuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Afripol, Balozi Jalel Chelba, amesema:
“Kupitia Operesheni Serengeti, Afripol imeongeza msaada wa kisheria katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
“Tumesaidia matapeli kukamatwa na sasa hivi tutazingatia matishio mengine ya kimtandao yatakayotokea ikiwamo mashambulio ya akili mnemba.”