Nimekaa hivi karibuni kwenye kikao cha siasa kisicho rasmi na kupata fursa ya kutafakari baadhi ya masuala yaliyopo na yale yaliyopita ndani ya jamii.
Nikarusha swali kwa wajumbe: “Unakumbuka enzi zile ambazo raia akiwa na pesa ambayo hawezi kuelezea ameitoa wapi, siyo tu alijikuta akiisadia polisi katika uchunguzi, bali pia alikuwa anakaribisha nguvu yote ya Serikali kuwasimamia polisi kuhakikisha kukamilika kwa uchunguzi juu ya uhalali wa kuwa na hiyo pesa?
Wapo wanaokumbuka. Ilikuwa ni enzi ambayo mwizi alikuwa na hadhi ya wizi tu, na hakuwa na hadhi nyingine yoyote ilimradi ilionekana kuwa amepata pesa kwa njia ambazo hawezi kuzielezea.
Enzi hizo, enzi za Mwalimu Nyerere, Serikali iliweka mikakati ya kimaadili, kisera, na kisheria kusimamia utekelezaji wa nia ya kulinda hadhi ya uongozi na ya Serikali ndani ya jamii. Wakati mwingine ilitumia sheria kama ya kuweka watu kizuizini, The Preventive Detention Act 1962, na ile ya Usalama wa Taifa, National Security Act 1970 kufikia malengo hayo.
Hizi ni sheria ambazo zimekosolewa kwa namna mbalimbali. Tume ya Nyalali, iliyoteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1991 na kuwasilisha taarifa yake mwaka 1992, ilitaja hizi sheria mbili pamoja na sheria nyingine 38 kuwa ni sheria ambazo, kimsingi, zinaondolea raia uhuru na haki zao za msingi, ikiwa ni pamoja na kuwa zinakiuka utawala wa sheria, na haki za kikatiba.
Mwalimu Nyerere mwenyewe alikiri kuwa aliongoza Tanzania akiwa na madaraka na nguvu kubwa za kisheria ambazo zingeweza kumfanya kuwa dikteta.
Lakini pamoja na kukubali hitilafu zilizokuwapo kwenye hizo sheria, ambazo zilifanyiwa marekebisho kutokana na mapendekezo ya Tume ya Nyalali, hatuwezi kufunika macho na kujiziba masikio ili kusahau kuwa ni sheria zilizosaidia sana kuweka sawa masuala kadhaa ambayo leo hii tunalalamika kuwa hayaendi sawa.
Mwarobaini ni mchungu sana, lakini unatibu malaria. Tulitema mwarobaini tukaanza kula peremende kujaribu kutibu malaria. Uchungu ukaondoka tukafurahia ladha tamu, na leo hii tukubaliane kuwa jamii ina malaria sugu.
Ile Tanzania ya enzi za Mwalimu ya mtu aliyeogopa kukutwa na mali nyingi ambazo hawezi kuelezea amezipata kwa njia zipi ilituponyoka hatua kwa hatua, kuanzia awamu moja hadi awamu nyingine. Na katika kutekeleza mabadiliko ya sheria zinazolinda uhuru na haki za msingi za raia, ikajitokeza fursa kwa watuhumiwa wa kujitafutia mali kwa njia zisizo halali kupumua kidogo.
Watuhumiwa wa wizi na wezi wakaanza kupata hadhi ambayo hawakuwa nayo zamani. Ahueni kwenye sheria ikawa ni mlolongo wa ahueni nyingine kwenye michakato ya siasa, na ndani ya jamii. Baadhi ya watu ambao zamani wasingethubutu hata kuota tu kugombea nafasi za uongozi kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya uadilifu katika mchakato wa kuchujwa kama wagombea, wakaona njia iko wazi kugombea uongozi.
Ambaye hakuingia kwenye uongozi akawa huru tu, katika mazingira mapya ya kutoulizana sana juu ya mafanikio yasiyoelezeka, kuendelea kujilimbikizia mali ambazo hazijulikani zimetoka wapi. Hawa nao wakawa vyanzo vizuri vya pesa za kusaidia baadhi ya wale waliojitokeza katika awamu mbalimbali kuwania nafasi za uongozi.
Matokeo yake ni kuwapo kwa mlolongo wa viongozi ambao wamepokea misaada ya pesa ambazo hazijulikani zimetoka wapi na wakazitumia kuchaguliwa kwenye ngazi mbalimbali za uongozi. Yule kiongozi wa enzi zile ambaye angeweza kukemea ukiukwaji wa maadili au ukiukwaji wa sheria akawa yeye mwenyewe kajiziba mdomo kwa kupokea msaada wa pesa ambazo hazijulikani zimepatikana kwa njia zipi.
Kusema kuwa hali hii imewaathiri baadhi ya viongozi pekee haitakuwa sahihi. Na sisi wapiga kura tumekuwa tunasubiri uchaguzi kwa shauku kubwa kwa sababu huwa ni fursa yetu ya kunufaika na hiyo pesa ambayo haijulikani imetoka wapi. Hatujui hali itakayojitokeza kwenye uchaguzi mkuu ujao, lakini tunafahamu kuwa desturi ya kuwania nafasi za uongozi nchini inaambatana na matumizi makubwa ya pesa ambazo hazijulikani zilikotoka.
Hayupo anayeweza kutetea hoja ya kurudi kwenye zile sheria za enzi hizo. Lakini wapo wengi watakaounga mkono ukali ule wa zamani wa Serikali kuhoji uhalali wa upatikanaji wa mali. Woga kuwa Serikali, kama chombo cha kutekeleza sheria, itadai uthibitisho na uhalali wa mali ya raia ni suala ambalo litajenga jamii ambayo itazingatia sheria katika maisha ya kila siku, ikiwa ni pamoja na kwenye biashara na uzalishaji.
Sheria zilinde uhuru na haki za msingi za raia, lakini Serikali iwe na jitihada ya kutolewa mfano katika kusimamia sheria ambazo zinamlazimu kila mmoja wetu kuthibitisha uhalali wa mali anazomiliki.
Bila hivyo tutakuwa na Serikali ambayo inasahau kutekeleza majukumu yake.