Reginald Mengi, mmoja wa wafanyabiashara wachache wanaotajwa kuwa na moyo wa kuwasaidia binadamu wenzao, hatunaye tena duniani.

Tangu taarifa za kifo chake zianze kusambaa wiki iliyopita, mamia kwa maelfu ya waombolezaji – ndani na nje ya nchi – wamejitokeza kutoa ushuhuda wa mema waliyotendewa na mzee Mengi.

Kifo chake kimeleta mzizimo mkubwa nchini kiasi cha kuwafanya watu wa kada mbalimbali wakiri kuwa tumepoteza mmoja wa wazalendo na watu wenye huruma.

Kuanzia watu wa kada ya chini kabisa hadi viongozi maarufu ndani na nje ya nchi yetu wameonyesha kuguswa na msiba huu. Huu ni ushahidi kuwa mzee Mengi alikuwa mtu wa watu.

Miezi michache kabla ya kufariki dunia alizindua kitabu cha historia ya maisha na mafanikio yake kwenye biashara. Anaeleza namna alivyotoka katika familia duni hadi ubilionea. Hili la kuacha maandishi yanayoeleza siri ya mafanikio yake ni jambo zuri na la kuigwa na Watanzania wengine, maana maandishi huwa hayafi. Kitabu hiki kitaendelea kuwa kitovu cha maarifa kwa vijana wanaotamani kufanikiwa katika maisha yao.

Tunatambua na kuenzi kazi kubwa iliyofanywa na mzee Mengi kwenye tasnia mbalimbali. Tunajua namna alivyohakikisha watu wa kada ya chini wanajiamini na kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini. Tunatambua alivyoshiriki kuongoza taasisi binafsi na za umma kwa mafanikio makubwa.

Mzee Mengi alikuwa mwana mazingira aliyeamini bila kuyatunza, juhudi za binadamu za maendeleo zingekuwa kazi bure. Kwa mfano, alitumia uwezo wake wote kuhifadhi mikoko katika eneo la bahari, alipanda maelfu ya miti kuzunguka Mlima Kilimanjaro, na kadhalika. Faida za uamuzi huo zinaonekana.

Mzee Mengi alikuwa tajiri asiyejivuna. Alikuwa mnyenyekevu bila kujali rika au hali ya mtu. Aliutumia utajiri wake kuwasaidia mamia kwa maelfu ya watu wenye mahitaji. Daima hakuchoka wala hakusita kutoa msaada wowote uliohitajika, hata kama kwa kufanya hivyo kuliathiri familia yake. Hili linapaswa kuigwa na matajiri wengine.

Tunatoa mwito kwa Watanzania kutafuta njia sahihi ya kumuenzi mzee Mengi. Imekuwa kawaida wakati wa msiba watu hulia na kuonyesha hisia kali, lakini punde husahau. Tunaomba isiwe hivyo kwa Mengi. Tutafute njia sahihi ya kumuenzi ili kizazi kijacho kiendelee kuona alama halisi za kazi zake zilizotukuka.

Tunaungana na ndugu, jamaa na marafiki katika kumwombea Dk. Mengi apate pumziko la milele. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amina.