*Likilipuka litaufilisi mgodi, litawaachia wananchi umaskini

* Wengi wao ni kutoka Dar es Salaam, Mwanza

*Serikali yaombwa kuingilia, kuzuia hali ya hatari

TARIME

Na Mwandishi Wetu

Wakati serikali ikifanya jitihada kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa manufaa ya wananchi, baadhi ya wakazi wanaozunguka Mgodi wa North Mara wanahujumu maendeleo yao wenyewe kwa mfumo wanaouita ‘tegesha’.

Tegesha ni mtindo unaotumiwa na matajiri wenye fedha kukodi au kununua maeneo ya wanavijiji ambayo wana taarifa kuwa mgodi utayahitaji na mara nyingi huwa na zuio la kuendelezwa ili yafanyiwe tathmini kwa ajili ya kulipwa fidia kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi.

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI uliofanyika hivi karibuni umebaini kuwa katika Kijiji cha Komarera, moja ya vijiji vinavyozunguka mgodi huo ulioko Tarime mkoani Mara, eneo la ekari 262 linalofanyiwa tathmini sasa linaendea kuvamiwa kwa ‘kutegesha’ miti hata baada ya tarehe ya zuio ya kuliendeleza.

Tangazo la kusitisha uendelezwaji wa eneo hili lilitolewa Juni 3, 2022 lakini linaendelea kuvamiwa na matajiri wanaopanda miti mingi inayomwagiliwa asubuhi na jioni ili kuiwezesha kukua kwa kasi, wakilenga (au kutegesha) kupata fedha kwa njia ya fidia.

JAMHURI limeshuhudia vibarua wengi wakimwagilia miti eneo hilo, huku wengine wakiendelea kupanda miche ya miti ya aina mbalimbali, mingi ikiwa ni mikaratusi yenye umri wa kuanzia siku moja hadi tatu, ikipandwa kwa kubananishwa mithili ya kitalu cha mchicha ili kuwa na idadi kubwa ya miti ya kulipwa fidia.

Uchunguzi wetu wa takriban wiki mbili umebaini kuwa gharama ya fidia inayolipwa kwa mti wa mkaratusi uliokomaa ni Sh 45,000 huku mti mdogo kabisa hulipwa asilimia 15 ya gharama ya mti mkubwa (Sh 6,750).

Miche hiyo inapandwa kwa kubananishwa kiasi kwamba eneo la hatua 20 kwa 20 linaweza kuwa na miche hadi 5,000.

Uzoefu katika eneo hilo unaonyesha kuwa mche mmoja unanunuliwa kwa Sh 500 na pamoja na gharama za kuutunza na kumwagilia hauzidi Sh 3,000 na hii inampa mtu ‘aliyetegesha’ miche 5,000 kwenye eneo dogo faida ya zaidi ya Sh milioni 18.

“Hapo unakuta mtu kategesha ekari zaidi ya kumi anavuna mabilioni ya fedha kwa gharama za umaskini wa wananchi, hii ni biashara ya watu wakubwa, hakuna mwanakijiji hapa anaweza kuwekeza mamilioni hayo, wako watu wakubwa nyuma ya hili,” amesema ofisa kutoka Idara ya Ardhi Halmashauri ya Tarime (jina tunalihifadhi kwa kuwa si msemaji wa idara hii) aliyezungumza na JAMHURI hivi karibuni.

Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni, Mtathmini wa Serikali anayefanya tathmini ya eneo hilo, Rashidi Mageta, amesema wanaendelea na tathmini katika eneo hilo kwa kuzingatia tarehe ya tangazo la zuio la kuendeleza.

“Ipo miche tunayokataa kuifanyia tathmini kwa sababu inaonekana wazi kuwa imepandwa baada ya tarehe ya zuio, ziko sehemu unakuta mche umepandwa jana na haujashika ardhini,” amesema Mageta.

Aidha, amesema watathmini wakikataa kuitambua miti inayobainika kupandwa nje ya wakati, wananchi wanazua migogoro na kukataa kuendelea na tathmini katika eneo husika.

Mmoja wa vibarua aliyepatikana hivi karibuni eneo la tukio alipotakiwa kueleza ameajiriwa na nani alionyesha msimamizi aliyekuwa pembeni ya mitambo inayovuta maji yaliyotumika kumwagilia.

Msimamizi huyo alipoulizwa kama ndiye mmiliki wa eneo hilo, hakusema chochote na kwenda kujifungia ndani ya gari dogo lililokuwa maeneo hayo.

“Malengo yao si kuvuna miti ya mbao, si unaona ilivyobanana kama kitalu cha mpunga, wametegesha kulipwa fidia na mgodi, ingekuwa miti ya mbao wasigefanya hivi, hii ikikua hivi hauwezi hata kupata ubao mmoja kwa mti,” amesema kibarua huyo aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Matiko, akihofia kukosa kazi ya kumwagilia ikiwa msimamizi wa shamba hilo atajua ameongea na vyombo vya habari.

Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni kuhusu utegeshaji huo, Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Asasi ya Muungano wa Jumuiya Tanzania (MUJATA), Tawi la Tarime, inayojishughulisha na kutetea haki za wananchi kulipwa fidia za haki, Samuel Kimasi, amesema tatizo la tegesha ni kubwa na lisipotatuliwa mapema litasababisha umaskini mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.

“Kuna mtandao wa watu wakubwa wenye nguvu kutoka Mwanza na Dar es Salaam wanatafuta taarifa kutoka mgodini, wakishajua mwelekeo wa mgodi kununua maeneo ni upi, wanakwenda kununua maeneo kwa wananchi ambao hawana taarifa ya kitakachokuja, wanayaendeleza ili walipwe fidia nono,” amesema Kimasi.

Amesema wakishanunua kwa gharama ndogo, wanaliboresha na kwa kuwa wana taarifa sahihi kuhusu vitu gani vinalipwa fidia kubwa, wanawekeza hapo.

“Huyu mwananchi anayelipwa fedha kidogo akiondoka kwenye eneo lake, fedha aliyonayo haiwezi hata kumjengea nyumba, anabaki anatangatanga wakati watu wengine wamelipwa fedha nyingi kwenye ardhi yake,” amesema.

Kimasi anashauri ili kuondokana na tatizo hili, mgodi uwe unapatana na wenye ardhi moja kwa moja badala ya tathmini ya sasa ya serikali ili kuwasaidia wananchi wasiwe na tamaa ya kuuza maeneo yao kwa wategeshaji.

“Mgodi nao ujiangalie, kuna watu wanavujisha siri, vinginevyo watu wanajuaje kwamba watakwenda kupanua mgodi kuelekea eneo fulani, wadhibiti uvujaji wa taarifa,” amesisitiza katibu huyo.

Hata hivyo, uchunguzi wetu umebaini kwamba baadhi ya maeneo kumekuwa na namna mpya ya utegeshaji wanaouita ‘chomoa’, ambapo wategeshaji wanakodisha eneo kwa mmiliki, wanapanda miti, wakati wa fidia mmiliki halisi wa ardhi analipwa fidia ya ardhi na wao wanalipwa fidia ya miti waliyotegesha, wenye miti wanaambulia fedha nyingi kuliko mwenye ardhi.

“Kwenye maeneo ya migodi kuna kitu kinaitwa sustainability (uendelevu), kwa sababu rasilimali hizi zinakwisha, zinapaswa ziwaache wananchi wakiwa na hali ya uchumi inayoweza kujiendeleza hata baada ya maisha ya mgodi, lakini kwa hali ilivyo hapa wananchi wanakubali kutumiwa na wenye fedha wananufaika kupitia ardhi zao wao wanabaki maskini,” amesema mtumishi mwingine wa ofisi ya Wilaya ya Tarime aliyeomba asitajwe jina gazetini.

Amewaasa wananchi wa Tarime kujifunza kwa Wilaya ya Kahama ambako migodi imenufaisha jamii nzima na mji umekuwa na shughuli nyingi za kiuchumi kiasi kwamba hata shughuli za mgodi zikifikia ukomo, tayari ziko shughuli nyingi za kiuchumi za kuuendeleza.

Tayari mtindo huo wa tegesha umewagharimu wategeshaji hao katika eneo jingine kijijini Komarero lenye ukubwa wa ekari 652, ambapo watu 5,273 walibainika kutegesha miti yenye thamani ya Sh bilioni 20.

Kwa mujibu wa Kimasi, katika eneo hilo wananchi 6,847 waliokuwa ndani ya muda wa zuio lililowekwa Mei 28, 2022, huku fidia hiyo ikiwa na thamani ya Sh bilioni 26, wameanza kulipwa na hadi tunakwenda mitamboni wananchi 3,468 walikuwa wamefidiwa jumla ya Sh bilioni 15.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Komarera, Nyamaganya Marwa, alipotafutwa hivi karibuni kuelezea suala hilo la tegesha katika eneo lake hakuwa tayari kulizungumzia.

Hata hivyo, mwanzoni mwa Juni, 2022 alinukuliwa na Gazeti la Sauti ya Mara kuwa utegeshaji huo haukubaliki kwa kuwa unakiuka zuio la serikali lililotangazwa kwa mujibu wa sheria.

“Hao wanaofanya vitendo hivyo kwa sasa wanakosea, tumeshawazuia kwamba kufanya hivyo ni nje ya utaratibu,” amesema.