Wakati Tanzania ikipambana kujiondoa katika adha ya njaa kwa kuboresha kilimo nchini kupitia mradi wa Kilimo Kwanza, wafanyabiashara wenye uchu wa utajiri wa haraka wanahujumu kilimo. Matajiri hawa wanapewa fedha za ruzuku kusambaza mbolea, lakini wanafanya kufuru. Kinachotokea, badala ya kuwapelekea wakulima mbolea, wanawapelekea mbolea iliyochanganywa saruji, chumvi na mchanga.
Madudu hayo yamegunduliwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, baada ya ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (FST) katika maghala ya mbolea kwenye kampuni za uuzaji na usambazaji wa mbolea.
Baada ya kupata ripoti hiyo, Naibu Waziri wa Wizara, Adam Malima, amecharuka na kutaka kampuni zilizobainika kujihusisha na uchakachuaji wa mbolea zifutiwe leseni za kufanya biashara hiyo kwa manufaa ya Watanzania.
Ripoti hiyo iliwasilishwa na Dk. Susan Ikera katika mkutano wa hivi karibuni mjini Dodoma, uliowashirikisha viongozi wa FST, kampuni za uuzaji na usambazaji wa mbolea, ambapo alizitaja zilizobainika kuchakachua mbolea kuwa ni pamoja na Staco, Apex na Yara.
Sehemu ya mbolea feki zilizokutwa katika maghala ya kampuni hizo iliambatanishwa katika ripoti hiyo, baadhi zikiwa zimechanganywa na saruji, nyingine zimechanganywa na chumvi.
Uchakachuaji huo ulikwisha kulalamikiwa na wakulima wa mazao mbalimbali yakiwamo ya tumbaku, pamba na mahindi katika maeneo tofauti nchini, baada ya mbolea feki walizouziwa kuwasababishia hasara kubwa katika msimu wa mwaka 2010/2011.
“Ni kweli kwamba mbolea kutoka kampuni fulanifulani za baadhi ya watu ambao wako hapa mbele yako, ambao nimewataja waziwazi kwenye ripoti niliyokuletea, siyo siri kweli mbolea hizo zilikuwa zimechakachuliwa,” Dk. Ikera alimweleza Naibu Waziri Malima na kuendelea:
“Kundi la kwanza walichanganya mbolea na chumvi, kundi la pili walichanganya mbolea na simenti, ambapo kwa mfano Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Wilaya za Songea na Namtumbo kiliuziwa mbolea aina ya NPK 2010 ikawasababishia kutopata matokeo mazuri ya mavuno ya tumbaku.
“Mbolea hiyo iliagizwa na Apex kutoka Yara, ilipowekwa shambani wakulima hawakupata tumbaku yenye ubora unaotakiwa, kwa hiyo wakulima wanadai fidia ya hasara waliyoipata baada ya kutumia mbolea hiyo.
“Nilikuta mbolea nyingine kama UREA zikiwa kwenye ghala la Mohammed Enterprises ziko chini ya kiwango, ambazo pia ziliuzwa serikalini kwa ajili ya ruzuku kwa wakulima. Pia tulikuta feki ambayo huhitaji kupeleka maabara, kampuni husika ni Staco.”
Baada ya kusikiliza maelezo hayo ya Dk. Ikera, Naibu Waziri Malima aliapa kushughulikia suala hilo kwa uzito unaostahili ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kampuni hizo zinapigwa marufuku kufanya biashara ya kuuza na kusambaza mbolea nchini.
“Haki ya Mungu, hii haikubaliki, maana wanafanya maskini kuwa maskini wa kutupwa. Mnafanyaje kazi ya ku-boost (kuinua) kilimo cha Tanzania na mbolea hii feki, this is shame (hii ni aibu),” alisema Malima huku akionesha kifurushi cha mbolea feki iliyochanganywa na saruji.
“Ninawezaje kuomba kura kwa mtu anayeuziwa mbolea hii, yaani hii ni dhambi. Hapana, hapana… Katika mbolea inayosambazwa kwa mfano mkoani Ruvuma asilimia 80 ni feki. Mmefanya mtu maskini kuwa maskini wa kutupwa,” alisema Naibu Waziri huyo na kuongeza:
“Kwanini tuwaache Watanzania innocent (wasiyo na hatia), ambao wametukabidhi dhamana ya kusimamia maisha yao wafanywe maskini… inatosha, nendeni mkafanye biashara nyingine, hatuwezi kufanya kazi na ninyi tena, hii haikubaliki.”
Alisisitiza kuwa Serikali haiko tayari kuruhusu mazingira yanayowezesha watu wachache kuwa milionea kwa kuwafanya Watanzania wengi kuwa maskini.
“Ninachosema, hatutawaruhusu kufanya kazi Tanzania, hakuna lugha nyingine. Unampa mtu mbolea hii jamani akafanye uzalishaji gani?
“Hatuwezi kuendelea huku juu wakati chini (kwa wakulima) kuna tatizo, wakulima wanajitahidi lakini hawapati kitu. Watanzania wanalalamika, wakulima wanalalamika!
“Nitamshauri Waziri (wa Kilimo, Chakula na Ushirika) aweze kuwafutilia mbali, hamna maana. Ninaumia sana ninapojua ninyi (kampuni hizo) ndiyo wa kutulinda lakini kumbe ndiyo mnatuumiza.
“Unaweza kusema kuchanganya mbolea na simenti ni accident (bahati mbaya)? This is beyond repair (hii imevuka mipaka), nimeshaomba Serikali isiwaruhusu kufanya biashara hiyo hapa Tanzania, hiyo ndiyo salamu yangu,” alisisitiza Malima.
Malima aliwanyima viongozi wa kampuni hizo nafasi ya kujitetea katika mkutano huo. Juhudi zilizofanywa na JAMHURI ili kuwapata viongozi wa kampuni hizo wazungumzie suala hilo hazikuzaa matunda.