Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji, maarufu kama Mo, limeitikisa Tanzania, lakini si jipya kwa mwaka huu barani Afrika.
Mo ni tajiri mkubwa wa saba barani Afrika kutekwa tangu mwaka 2018 ulipoanza.
Matukio mengine ya namna hiyo yametokea nchini Afrika Kusini, Msumbiji na Nigeria.
1. Shiraz Gathoo – Afrika Kusini
Mfanyabiashara maarufu kutoka Afrika Kusini alitekwa Machi 10, mwaka huu. Watekaji wake walijifanya kuwa ni askari wa usalama barabarani na kuweka kizuizi bandia barabarani na kumteka.
Aliachiwa huru mwishoni mwa mwezi Agosti baada ya kukaa mateka kwa miezi sita. Haijafahamika aliachiwa namna gani lakini wadadisi wanahisi alitoa komboleo la pesa kwa watekaji.
2.Liyaqat Ali Parker – Afrika Kusini
Julai mwaka huu, Liyaqat Ali Parker, mfanyabiashara kutoka Afrika Kusini alitekwa jijini Cape town akiwa katika majengo ya ofisi yake na watu waliokuwa na bunduki.
Parker, 65, ni mwanzilishi wa Kampuni ya Foodprop Group ambayo humiliki maduka ya jumla ya Foodworld nchini humo. Anamiliki pia mali nyingine nyingi nchini humo.
Mfanyabiashara huyo alitekwa Julai baada ya kufuatiliwa kwa muda na watu watano waliotumia gari aina ya ‘double-cabin’.
Alizuiliwa kwa miezi miwili hadi aliporejea nyumbani kwake Septemba 17.
Siku ya kutekwa kwake, wanaume watano wasiojulikana wanadaiwa kulifuata gari lake hadi kwenye maegesho ya biashara yake Fairway Close, N1 City chini ya jengo.
Washambuliaji waliokuwa na silaha, mwanzoni walimshambulia mlinzi na kumfungia chooni, pia kumpokonya simu yake.
Baadaye walimtwaa mfanyabiashara huyo na kumuingiza ndani ya gari lao kisha wakatoroka naye.
3. Baba yake John Obi Mikel – Nigeria
Baba wa mchezaji nyota wa Nigeria, John Mikel Obi, pia alitekwa mwezi Juni na watu waliokuwa na silaha katika eneo la Enugu.
Alitekwa Juni 26, lakini akaokolewa na polisi Julai 2, baada ya makabiliano makali kati yao na waliokuwa wanamzuilia.
Inadaiwa waliomteka walikuwa wanataka kiasi cha paundi 21,000. Ilikuwa ni baada ya watekaji kupiga simu wakitaka fedha ndipo polisi walipofanikiwa kuwafuatilia na kufahamu walikokuwa. Waliwavamia na baada ya kufyatuliana risasi watekaji wakakimbia na kumwacha mateka msituni.
Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa Chief Mikel Obi kutekwa. Awali alitekwa mwaka 2011 na watekaji kudai fedha. Obi alifanikiwa kuokolewa na polisi lakini mtoto wake anadai aliteswa wakati alipokuwa kizuizini.
4. Andre Hanekom – Msumbiji
Raia wa Afrika Kusini anayefanya biashara nchini Msumbiji, Andre Hanekom, alitekwa katika Jimbo la Cabo Delgado Agosti katika mji wa Palma akiwa kwenye maegesho ya Hoteli ya Amarula.
Mfanyabiashara huyo aliyekuwa ameishi Msumbiji kwa miaka 26, anadaiwa kuandamwa na wanaume wanne wasiojulikana na kufyatuliwa risasi mara kadhaa. Alikimbilia hotelini lakini akakamatwa na kuingizwa kwenye gari na kutoroshwa.
Sababu za kutekwa kwake bado zina utata. Kuna taarifa zilizodai kwamba waliomteka walikuwa wanajeshi wa kupambana na ugaidi na kwamba alikuwa anahusishwa na ugaidi. Lakini mke wake, Francis, alikanusha kwamba mumewe amewahi kujihusisha na ugaidi.
Alipatikana katika hospitali moja Palma akiwa anapatiwa matibabu chini ya ulinzi wa jeshi.
5. Sikhumbozo Mjwara – Afrika Kusini
Sikhumbozo Mjwara, 41, mfanyabiashara kutoka jijini Durban, Afrika Kusini pia alitekwa mwezi Agosti na mpaka sasa bado hajulikani alipo.
Watu watatu wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo huku uchunguzi ukiendelea.
Mfanyabiashara huyo alitekwa akiwa nje ya mahakama mjini Verulam, baada ya kuhudhuria kikao cha kusikilizwa kwa kesi inayohusisha mzozo wa kifedha. Mjwara ana kampuni zinazohusika katika biashara ya madini na mighahawa.
6. Robert Mugabe wa Uganda
Mmoja wa wafanyabiashara maarufu kutoka Wilaya ya Nakasongola, Robert Mugabe, alitekwa nyara Agosti na watu waliokuwa wamevalia sare za jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mugabe, 38, alitekwa alipokuwa akisafirisha samaki kutoka Kasese kwenda Ishasha, Wilaya ya Kanungu, walipokuwa wanapitia Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth.