Hatimaye watuhumiwa watatu kati ya watano wa mauaji ya John Massawe, katika Kijiji cha Kindi, Kibosho mkoani Kilimanjaro, wamekamatwa.
Masawe aliuawa kikatili Juni 9, 2009 kijijini hapo, lakini baadaye watuhumiwa wa mauaji hayo wakaachwa. Waliokamatwa na kuwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi ni John Kisoka (Magazeti) na mkewe ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja. Mwingine ni mdogo wake John aitwaye Deo Kisoka.
Wanaoendelea kusakwa ni Lucas Joseph Kisoka na Musa Joseph Kisoka wanaodaiwa kukimbia baada ya kupata taarifa za kutafutwa.
Kwa miaka mitatu, Gazeti la JAMHURI limekuwa likiandika habari za uchunguzi kuhusu kesi hiyo na kuachwa kwa watuhumiwa wakuu. Pia JAMHURI imekuwa ikiandika malalamiko mengi ya ndugu wa marehemu waliofikia hatua ya kuomba msaada kutoka kwa Rais John Magufuli, ili haki itendeke.
Watuhumiwa hao wanamiliki vitegauchumi kadhaa jijini Mwanza ambako ndiko walikokamatwa.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman, hakuwa tayari kuzungumzia kukamatwa kwa watuhumiwa hao, akisema asingependa kuvuruga upelelezi kwani kuna wengine wanatafutwa.
DCI Athumani aliiambia JAMHURI: “Nakushuruku kwa concern (kuguswa) yako, na tayari linafuatiliwa na timu kutoka hapa makao makuu ya upelelezi. Kinachohitajika ni ushirikiano/ukaribu wa timu ya upelelezi ya hapa makao makuu na mashahidi wa upande wetu.”
Kukamatwa kwa watu hao wanaotajwa kuwa ‘watuhumiwa muhimu’ katika tukio hilo la mauaji, ni faraja kwa familia ya marehemu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamika kuwa vyombo vya dola, hasa Polisi wameamua kuwalinda watu hao.
Vyanzo vya habari vinasema kukamatwa kwa watuhumiwa halikuwa jambo jepesi, kutokana na mtandao mpana uliowezesha wakati fulani hadi kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa nyaraka na vielelezo muhimu katika majalada ya kesi.
Maelezo ya mashahidi ambao majalada yao yaliibwa katika mazingira ya kutatanisha kwa msaada wa Ofisi ya RCO Kilimanjaro ni ya Alfonsina John, Ludovick Munisi, Lelo Selengia, Peter Gerald, Boniface Munishi na Fulgence Gerald.
John aliuawa baada ya kuingia kwenye mtego wa wauaji waliompigia simu na kumweleza kuwa kaka yake aitwaye Raymond John Massawe (Kichwa), alikuwa amegongwa na gari na alikuwa katika hali mbaya.
Simu hiyo ilimfanya John aache kazi na kwenda eneo la ‘ajali’. Katika Barabara ya Sukari alikutana na ‘wauaji’ ambao walimwingiza kwenye gari lao na kumpeleka nje ya mji, umbali wa kilometa 15 katika eneo la Kindi. Huko inaaminiwa aliteswa hadi akafariki dunia.
Inadaiwa kuwa mateso hayo yalilenga kumshinikiza awataje watu waliohusika kwenye mauaji ya mama mzazi wa watuhumiwa hao, Martha Kisoka (68), aliyeuawa Mei, 2009.
Awali, mwaka 2007 John (marehemu) na wenzake wanne walihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela kwa kosa la kuvunja na kuiba nyumbani kwa Kisoka, lakini walikata rufaa na kuachiwa mwaka 2008.
Kutokana na mazingira hayo, inadaiwa kuwa watuhumiwa hao waliamini kuwa John ndiye aliyeshiriki tukio la kuvamiwa na hatimaye kuuawa kwa Kisoka. Mauaji ya James yanatajwa kuwa ni ya kulipiza kisasi.
MATESO KABLA YA KIFO CHA JOHN
Ndani ya nyumba ya watuhumiwa hao, inadaiwa alikuwamo John na vijana wengine watatu ambao nao walikamatwa kwa nyakati tofauti na watuhumiwa hao na kuteswa pamoja naye.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, John alining’inizwa kichwa chini huku akichomwa sehemu mbalimbali za mwili kwa upanga uliokuwa ukiwekwa kwenye moto.
Inadaiwa kuwa kabla ya kumuua, John aliomba aagane na mtoto wake mchanga aliyekuwa na umri wa mwezi mmoja.
Tukio hilo lilishuhudiwa na wanakijiji ambao waliizunguka nyumba ya watuhumiwa hao wakijaribu kutaka kuwaokoa vijana hao, lakini watuhumiwa wanadaiwa kufyatua risasi za moto hewani kuwatisha.
Baada ya tukio hilo, watuhumiwa walikimbilia nje ya nchi, lakini aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko, aliutangazia umma kuwa John aliuawa na ‘wananchi wenye hasira kali!’
Baada ya vyombo vya habari kulivalia njuga tukio hilo na kumbana Kamanda Ng’hoboko, hatimaye akayataja majina manne ya watuhumiwa wa mauaji hayo na kuahidi kuwa wangekamatwa.
Kamanda Ng’obhoko na Polisi kwa jumla hawakuwakamata watuhumiwa, isipokuwa vijana wawili – Idrisa Munishi na John Mallya (Small Boy) – na kuwafikisha mahakamani ambako walishitakiwa kwa mauaji ya John.
Vijana hao walifikishwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Stella Mugasha, katika shauri la jinai namba PI 9/2009 lakini Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliliondoa shauri hilo mahakamani.
FAMILIA YAMWANDIKIA BARUA RAIS JOHN MAGUFULI
Novemba 13, mwaka jana, ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli kuapishwa, familia hiyo ilimwandikia barua kuomba ofisi yake isaidie kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
“Tunakuandikia barua hii tukiwa wanyonge na tuliokata tamaa kutokana na namna watuhumiwa wanne tuliowashuhudia wakimuua ndugu yetu James John mnamo Juni 09, 2009 wakiwa mitaani huku jalada la polisi la uchunguzi likipotea au kuibwa,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Familia hiyo ilihoji nguvu waliyonayo watuhumiwa hao hadi kuweza kula njama na kuweza kuiba majalada yote yanayohusiana na mauaji hayo.
Ndugu wa marehemu walimwomba Rais Magufuli afanye mambo matatu – kuliagiza Jeshi la Polisi nchini kuwakamata wafanyabiashara hao ili kuepusha kuvuruga upelelezi; kuunda tume kuchunguza mazingira ya kuibwa kwa jalada la polisi la uchunguzi pamoja na majalada madogo ya shauri hilo; na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliofanya hujuma hiyo.
Waliomba uchunguzi huo usihusishe askari wa Kilimanjaro ambao ndiyo watuhumiwa kama ilivyofanyika wakati wa uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na mfanyabiashara Abubakar Jaffar (JJ) mwaka 2002.
Barua hiyo ilisainiwa na Beda Massawe, msemaji wa familia hiyo, akilalamikia DPP, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kwa kushindwa kuwasaidia.
Awali, Oktoba 13, mwaka jana, IGP alimwandikia barua DCI akiagiza kufuatiliwa kwa malalamiko ya msemaji wa familia hiyo, Beda Massawe, ili kubaini kama kulikuwa na ukweli wa ukiukwaji wa maadili.
Barua hiyo ilisainiwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, S.M. Ambika, kwa niaba ya IGP. Ilimpa siku 17 DCI kushughulikia malalamiko hayo na kumjulisha (IGP) matokeo ya ufuatiliaji huo.
Nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa msemaji huyo wa familia ikimtaka afike ofisi ya DCI kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa suala lake. Alifika Dar es Salaam, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa wakati huo.
DCI ATUMA MAKACHERO KUANZA UPYA UCHUNGUZI
Baada ya barua ya malalamiko ya familia hiyo kumfikia Rais Magufuli, IGP Ernest Mangu alimwagiza DCI kufanyia kazi malalamiko hayo.
DCI Athuman aliunda kikosi kazi cha uchunguzi kikiongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Charles Kenyela, ambacho kilijichimbia kwa muda mrefu mkoani Kilimanjaro kikikusanya ushahidi wa kutosha kuhusu mauaji hayo.
JAMHURI imebaini kuwa chini ya uchunguzi huo, mashahidi 16 walijitokeza kwa makachero kutoa ushahidi wao wakiwamo vijana watatu waliokuwa miongoni mwa walioteswa pamoja.
Habari kutoka ndani ya timu hiyo ya makachero zinaeleza kuwa vijana hao ‘walimwaga’ kila kitu. Miongoni mwa waliohojiwa ni polisi walioshiriki kuupeleka mwili wa John katika Hospitali ya Mawenzi. Makachero hao pia wamefanikiwa kupata nakala halisi ya ripoti ya uchunguzi wa kifo (Postmortem Report).
Uchunguzi wa awali wa JAMHURI umebaini kuwa ripoti ya awali ya Ofisi ya RCO Kilimanjaro, ilighushiwa na ofisi hiyo na kuwekwa kwenye jalada la kesi.
KUNA MBINU ZA KUVURUGA UPELELEZI?
Wakati watuhumiwa hao wakiendelea kuhojiwa, baadhi ya matajiri wamemwaga mamilioni ya shilingi kuhakikisha upelelezi wa mauaji hayo unavurugika, lengo likiwa kuwaokoa matajiri hao.
Taarifa za uhakika kutoka Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi zinaonesha kuwa mmoja wa wafanyabiashara ambaye ni mwanachama na kiongozi katika Chama cha Wasafirishaji wa Mabasi ya Abria katika miji ya Arusha na Moshi (AKIBOA), anatajwa kuhusika katika mipango hiyo. Jina la mfanyabiashara huyo linahifadhiwa kwa sasa kutokana na kuendelea kupata vielelezo vya madai hayo.
Juhudi kubwa zinafanywa na ndugu wa watuhumiwa hao wakishirikiana na askari kadhaa (majina tunayo), kutaka kumpa dhamana mmoja wa watuhumiwa ili ‘apigane vita hiyo akiwa nje’.
Wakati wa kampeni na hata baada ya kuapishwa, Rais Magufuli aliwaahidi Watanzania kuwa atasimamia suala la haki kwa watu wote bila ubaguzi.