Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Arusha
Baadhi ya mataifa nje ya Afrika yameomba kujiunga kama wanachama waangalizi katika Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Almasi Afrika (ADPA) zikiwemo taasisi zilizobobea kwenye masuala ya madini hayo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko wakati akifunga Mkutano wa Tatu wa Dharurra wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo uliofanyika jijini Arusha na kutanguliwa na mkutano wa wataalam kutoka mataifa wanachama.
Dkt.Biteko ameongeza kwamba, suala hilo lilikuwa miongoni mwa ajenda tatu zilizojadiliwa katika mkutano huo na kwamba jumuiya hiyo imepanga kuangalia sifa na vigezo kwa nchi hizo na wakati utakapowadia italazimika kubadilisha Katiba ya jumuiya hiyo.
Lengo likiwa ni kutoa fursa kwa nchi hizo kujiunga waweze kuendelea kujengeana uwezo na kubadilisha uzoefu na nchi zilizo nje ya Afrika katika masuala ya almasi.
Pia, amesema kuwa ajenda nyingine iliyojadiliwa katika kikao hicho ni kuhusu uteuzi wa watendaji wa kudumu katika sekretatieti ya umoja huo ambapo baraza liliamua hadi kufikia katikati ya mwezi Septemba, mwaka huu watendaji hao wawe wamepatikana.
Akizungumzia utaratibu wa ajira katika umoja huo, amesema mwananchi yoyote kutoka nchi wanachama anaruhusiwa kuomba na kwa watu ambao wako nje ya mfumo wa Serikali watatakiwa kupata idhini ya Serikali.
Ameongeza kwamba, ajenda nyingine iliyojadiliwa ni kupitiwa upya na kuidhinishwa kwa Katiba ya jumuiya ambayo itawezesha kutekelezwa kikamilifu kwa matakwa ya jumuiya hiyo.
Katika hatua nyingine, washiriki wa mkutano huo walipata fursa ya kutembelea katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kujionea vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo.
Katika Mkutano wa Tatu wa Dharura wa Baraza la Mawaziri, Tanzania ilikuwa nchi mwenyeji na Mwenyekiti wa sasa wa umoja huo.