Siku niliposikia Mahakama Kuu (Bukoba) imetoa hukumu ya kunyongwa hadi kufa kwa Mwalimu Respicius Patrick kwa kosa la kumuua mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kibeta, Sperius Eradius, niliduwaa.

Katika kuduwaa, nilianza kutafakari juu ya ndoto yangu hii ya kuwa mwalimu niliyoipigania kwa nguvu zote, kwa uwezo wa Mungu, na hatimaye kufanikiwa.

Ni kwamba nikiwa mwanafunzi ndoto ya kuwa mwalimu au mwanasheria ilininyima usingizi kwa miaka mingi. Nikiwa mwanafunzi nilikuwa nikijisemea kuwa sitapiga mwanafunzi wala kutoa adhabu yoyote kwa mwanafunzi. Niliamini kutoa adhabu hasa ya viboko ni ukatili na unyanyasaji.

Kuhusu ndoto ya kuwa mwanasheria, nilitaka kukomesha tabia za watu wanaonyanyasa na kuonea wenzao, niliapa kuwatetea wanyonge hasa wananchi wa kawaida wasiojua sheria na haki zao. Hii ndiyo ilikuwa ndoto yangu.

Lakini nilipofanikiwa kuwa mwalimu mambo yalibadilika kabisa. Nilijitahidi kadiri niwezavyo nisichape wanafunzi lakini haikuwa hivyo. Nilikutana na wanafunzi watukutu kupitiliza, nikajitahidi kuwashauri wabadilike, hawakubadilika hata chembe.

Nikawauliza wanafunzi wenzao kujua wanavyojisikia na wangependa nitoe adhabu gani itakayowafanya kusoma kwa bidii na kufuata sheria, taratibu na miongozo ya shule. Wengi wao walisema ni bora kuchapwa kwa sababu maumivu ya fimbo huisha mapema, achilia mbali sheria ya viboko sambamba na midahalo mingi inayoendelea juu ya adhabu hii inayoweza kuleta maafa kama ilivyotokea kwa Mwalimu Respicius.

Nirudi kwenye mada kuu. Ni vigumu kwa nafasi yangu kama mwalimu kuamini kilichotokea hivi karibuni juu ya hukumu ya kifo kwa Mwalimu Respicius kutoka Bukoba. Lakini, hata hivyo, sina budi kuamini kwa kuwa tukio hilo limekwisha kutokea.

Mwanzoni nilitamani walimu wote tuandamane kwa amani kupinga hukumu hii lakini nikajua kuwa nafasi ya kukata rufaa bado ipo, hivyo hakuna sababu hiyo kwa sasa.

Lakini japokuwa nafasi ya kukata rufaa bado ipo, hukumu hii imeacha maswali mengi kuliko majibu.

Ni hivi karibuni Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba imemhukumu mwalimu huyo aliyekuwa mwalimu wa nidhamu wa Shule ya Msingi Kibeta, Respecius Patrick Mutazangira, kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Sperius Eradius, aliyekuwa akituhumiwa kuiba mkoba wa Mwalimu Herieth Gerald ukiwa na simu aina ya Nokia 1280 na fedha shilingi 75,000, huku mkoba huo ukiletwa baadaye na dereva wa bodaboda baada ya Mwalimu Herieth kuusahau.

Mwanafunzi Sperius Eradius alituhumiwa kuiba mkoba huo kwa kuwa ndiye aliyempokea mizigo Mwalimu Herieth na kuipeleka ofisini kisha kurudi darasani.

Mwanafunzi huyo baada ya muda aliitwa na kuulizwa mkoba huo na kukana kuuchukua ndipo akaadhibiwa na mwalimu wa nidhamu hadi kupoteza maisha kwa kipigo.

Baada ya hukumu hiyo kwa mwalimu huyo, mahakama ilimuachia huru Mwalimu Herieth Gerald.

Hukumu hii ya kihistoria kwenye kada hii ya ualimu imeibua hisia na mijadala mbalimbali, wengi wakihoji uhalisia wa adhabu iliyotolewa kama imezingatia haki na mazingira halisi ya elimu yetu hapa nchini.

Naomba nieleweke wazi kuwa sitetei wala kuunga mkono ukatili dhidi ya watoto (wanafunzi) na sikubaliani kabisa na adhabu kali kwa wanafunzi zinazosababisha madhara, ikiwa ni pamoja na ulemavu au hata vifo, isipokuwa najiuliza, kazi hii inayozalisha wataalamu wa kada zote duniani ikiwemo mahakimu na majaji haina ajali kazini? Au kazi hii inayozalisha wasomi wa kila aina ndiyo jela ya mwalimu? Ama ni kusema kuwa kuteleza kwetu ndiyo hukumu yetu?

Wote mmenyamaza kimya licha ya mema yote tuliyotenda kwenu, watoto wenu na jamii yenu? Wazazi, walezi, wanafunzi, viongozi, wanaharakati wa haki za binadamu ni lini mtawatetea walimu?

Hivi walimu tumekosea wapi? Kosa letu ni kuwapa maarifa shuleni ndiyo iwe shukrani ya punda?

Leo hii kazi yangu haina bahati mbaya na sina nafasi ya kurekebisha makosa?

Enyi wadau wa elimu, viongozi wa taasisi za elimu na wanaharakati mnaobeza kazi ya ualimu na walimu kumbukeni mlifundishwa na walimu, ninyi ni zao la walimu.

Kwa nini mnashindwa japo kidogo kuwatetea walimu? Kinyume chake mmekuwa mwiba kwa walimu, kumbukeni watoto mnaowatetea ni wetu sote. Sisi walimu si wakatili kama mnavyojaribu kutujengea taswira ovu.

Walimu ni wazazi, walezi bora na ndio tunaishi na watoto wenu zaidi na kuwajua vizuri kwa kutambua mienendo na tabia zao mbalimbali pindi tunapokuwa nao shuleni.

Tumekuwa washauri wao katika maisha ya shule na baada ya shule. Tunawashauri mazuri kwenye taaluma na nidhamu ili wafanikiwe kutimiza ndoto zao.

Tumekuwa daraja la mafanikio yao wote waliotii na kufuata maelekezo yetu.

Ninaomba Mwenyezi Mungu awakumbushe kuwa mko hapo mlipo kwenye ofisi nzuri zenye viyoyozi kwa kazi ya mwalimu.

Tambueni mnao wajibu kuwatetea na kuwatia moyo walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Na si kuwalaumu na kuwabeza kila mara wanapoonekana kuteleza, jengeni utamaduni wa kuwapongeza walimu. Tukatae utamaduni ovu na usiofaa, uliojengeka kwenye jamii yetu kulaumu na kuona mabaya tu ya walimu.

Kwa mfano wanafunzi wanapofeli hulaumiwa walimu, lakini wanafunzi hao hao wanapofaulu sifa zote huenda kwa wanafunzi. Hii si sawa kabisa, tubadilike.

Ni matamanio yangu walimu watakaokuwa wakifanya vizuri nao wataalikwa bungeni na kwingine kwa ajili ya kuwapongeza.

Rai yangu kwa wadau wa elimu na serikali, turejeshe heshima kwa walimu, tukumbuke wema wa walimu katika taifa hili. Tusisahau mmoja wa waasisi wa taifa letu na aliyeshiriki harakati za kuleta uhuru ni mwalimu.

Nipaze sauti kwa walimu wenzangu, viongozi wa Chama cha Walimu (CWT), serikali bila kusahau Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), kwamba ili sekta hii ya elimu iheshimike hatuna budi kumtetea mwalimu huyu ambaye yeye na familia yake wanapitia kipindi kigumu.

Vilevile, hukumu hii itoe funzo kwa walimu kujitathmini na kuacha kukurupuka kabla ya kutoa adhabu.

Pia walimu tupende kutoa adhabu zenye tija, tusione kuwa viboko ndiyo suluhisho pekee katika kubadilisha tabia za mwanafunzi.

Tunaweza kutoa adhabu za kawaida kwa wanafunzi watundu na wavivu, lakini ziwe adhabu zinazoruhusiwa kisheria.

Walimu watakaokiuka sheria, taratibu na miongozo ya taaluma yao, wapewe adhabu zinazostahili, si hukumu wala adhabu za kukomoana.