Nakaribia wiki mbili sasa nikiwa hapa Bukoba. Naendelea na ukarabati wa nyumba ya mama yangu iliyosambaratishwa na tetemeko. Hata hivyo, pamoja na kuwa katika ujenzi huu, haimaanishi kuwa kazi yangu nimeiweka kando. Naendelea kuzungumza na wananchi, nafuatilia kinachoendelea na jinsi misaada inavyotolewa kwa wahanga wa tetemeko.
Angalau sasa watu baadhi wamepewa magodoro, wengine wamepewa mablanketi, sukari kilo 2 kwa familia, mchele kilo 5 hadi 8 na misaada midogo midogo. Kuhusu ujenzi wa nyumba zao, bado wengi wanasubiria ahadi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Aliwatangazia Watanzania kupitia bungeni, kuwa walioathirika zaidi watapewa mabati 20, mifuko 5 ya saruji na fedha za kuanzia ujenzi.
Wapangaji nao waliahidiwa kodi ya pango ya miezi sita. Nimemsikia Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu), Salum Kijuu. Ametoa taarifa inayosikitisha kuwa baadhi ya watu wameendelea na mchezo wa kutumia maafa kama sehemu ya kivuno. Kwamba baadhi ya watu wameandikisha watoto wao wakidai ni wapangaji. Hii inasikitisha.
Sitanii, ukiacha hayo, shida bado ni kubwa. Ukiacha mjane aliyechangiwa na Rais John Magufuli moja kwa moja, wananchi wengine ni shida. Wachache wenye uwezo angalau wameanza kurejesha nyumba zao katika hali ya kawaida, ila wengi tetemeko limewarejesha katika ufukara. Ni katika hatua hii ingefurahisha Serikali kuonesha dhana ya hifadhi ya jamii (social security).
Nchi kama Tanzania kwa uchaguzi tunaoufanya katika jamii yetu tunategemea falsafa ya mkataba wa jamii (social contract theory). Hii inamaanisha kuwa matatizo yanapotukumba, kwa pamoja kupitia Serikali yetu tunapaswa kukusanya nguvu; kwa michango na kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina kuhakikisha tunawarejesha wananchi katika hali ya kawaida ili kuwaondolea majonzi. Ni kama bima baada ya ajali. Natamani kuona hili likifanyika.
Sitanii, ukiacha hilo, zipo takwimu zinazotolewa na kuacha maswali mengi. Mimi nazifahamu vyema shule za sekondari za Nyakato na Ihungo zilizokumbwa na dhoruba ya tetemeko. Takwimu zinazotolewa kuwa kila shule moja inahitaji wastani wa Sh bilioni 30 kukarabatiwa zinaacha maswali mengi kuliko majibu. Hapa Bukoba kuna jengo la ghorofa nne au tano linaitwa Bugabo House. Limejengwa kwa gharama ya Sh milioni 700 kwa taarifa nilizopata.
Napata wakati mgumu kufikiri kwamba mabweni 10 au 20 yaliyovunjika yanahitaji Sh bilioni 30? Kweli? Niwahamishie Dar es Salaam kidogo. Jengo la PPF Tower lililopo Mtaa wa Garden na Ohio, lina ghorofa 18. Lilijengwa kwa gharama ya Sh bilioni 18. Jengo hili unaweza kulaza wanafunzi wote wa Ihungo na Nyakato na bado nafasi ikabaki. Katika hili nasema Rais John Magufuli chonde chonde usikubali kila taarifa unayopewa. Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako!
Jingine, zipo taarifa za mlipuko wa ‘volcano’ huko Bwanjai, Mugana. Moto umeibuka ghalfa, ukawaka juu ya ardhi, udongo ukawa mwekundu. Maprofesa wetu bila kujipa hata sekunde ya kufanya uchunguzi, wakaibuka na majibu mepesi wakidai kuwa mizizi iliyokuwa ardhini ndiyo iliyowaka moto. Wakiulizwa nani aliikoka? Kiberiti ilikipata wapi? Mbona eneo halikuwa na msitu? Imekuwaje ardhi kavu iwake moto hadi iwe nyekundu? Kwa nini itokee sasa na si siku zilizopita? Hakuna majibu.
Ni kweli maeneo kama Liganga huko Ludewa huwa moto unawaka wenyewe ardhini. Hii si ajabu kwani kuna makaa ya mawe. Niliamini na naendelea kuamini kuwa majibu yaliyotolewa juu ya moto wa Bwanjai uliolipuka ni mepesi mno. Serikali inapaswa kufanya uchunguzi pengine kuepusha maafa yanayoweza kutokea siku za usoni.
Wakati Bwanjai ardhi ikiwaka moto, huko Misenye zipo taarifa kuwa kuna sehemu ujiuji umetoka ardhini na kutengeneza kimlima kidogo. Hili nitaendelea kulifuatilia, na ukiangalia ukanda wa Misenye na Bwanjai hauna tofauti na safu ya Mlima Ruwenzori, Uganda uliotokana na volcano. Ni kutokana na hili nasema Serikali isitoe majibu mepesi Bukoba.
Uchunguzi ufanyike juu ya chanzo halisi cha moto huu na ikibidi kama kuna hatari dhahiri, wananchi wahamishwe haraka katika maeneo haya badala ya kusubiri siku ya siku moto ukalipuka wananchi na mifugo yao wakafunikwa. Maswali haya na mengine Bukoba yanahitaji majibu. Taratibu zinazoandaliwa na Serikali kusaidia wahanga wa tetemeko kasi iongezeke. Mungu ibariki Tanzania.