Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab amesema Serikali imeboresha mazingira ya Waandishi wa Habari ili kuongeza ufanisi katika kazi.

Ameyasema hayo wakati wa kipindi cha Asubihi Njema, kinachoendesha na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuhusiana na miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Karume House, Mnazimmoja.

Amesema, Serikali imeboresha Maslahi ya Wafanyakazi ikiwemo Waandishi wa Habari ambapo Waandishi hao wamepatiwa Posho la mazingira hatarishi.

Aidha amesema Sheria ya Habari imeshafikishwa katika ngazi ya Makatibu Wakuu ili kuondosha kilio cha Waandishi wa Habari juu ya Sheria hiyo.

Akielezea kuhusu Vijana Katibu Fatma amesema Serikali imetoa mafunzo mbalimbali ikiwemo ya Uongozi, Biashara na Uzalendo ili kuwajenga kuwa Raia wema wa kujenga Nchi yao.

Kwa upande wa Michezo Katibu Fatma amesema Serikali inaendelea na Ujenzi wa Viwanja vya Michezo 17 vya Wilaya na Mikoa sambamba na kufanya ukarabati wa Uwanja wa Amani na Gombani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ndg. Fatma Hamad Rajab akielezea miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kipindi cha Asubuhi Njema, kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) huko Karume house Mnazimmoja.

Aidha amesema lengo la Ujenzi wa Viwanja hivyo ni kuwapatia fursa Vijana kucheza na kuibuwa vipaji vilivyopo Nchini kwani Zanzibar ina Vipaji mbalimbali.

Mbali na hayo amesema kwa upande wa Sanaa milango imefunguka kwani Vijana wamepata fursa ya kwenda nchi za nje kuonyesha Sanaa ya Zanzibar na kuwataka kuzingatia Mila, Silka na Tamaduni za Nchi.

Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano.