Wakati mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Uropa yakiingia hatua ya robo fainali, hali imekuwa mbaya kwa England kwa mwaka huu, baada ya timu zake zote kuondolewa kwenye michuano hiyo mikubwa yenye mvuto wa aina yake Ulaya.
  Everton iliyosalia hadi Alhamisi wiki iliyopita kwenye michuano ya Uropa, nayo ilikutana na balaa lililowapata Chelsea, Manchester City, Arsenal zilizokuwa zinashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya. Timu zote zimeondolewa katika hatua ya 16 bora.
  Everton ya England imetupwa nje ya mashindano hayo baada ya kuchapwa mabao 5-2 dhidi ya Dynamo Kiev ya Ukraine, na kufanya matokeo ya jumla kuwa ni 6-4 baada ya mchezo wao wa awali Everton kushinda nyumbani bao 2-1.
  Usiku huo wa Alhamisi iliyopita pia ilishuhudia AS Roma ikiangukia pua baada ya kuchabangwa mabao 3-0 nyumbani pale walipocheza na Fiorentina zote kutoka nchini Italia. Kwa matokeo hayo Roma imetupwa nje kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wao awali.
  Nayo Inter Milan ikakwaa kisiki baada kufungwa mabao 2-1 walipocheza na Wolfsburg ya Ujeruman na kuondoshwa pia katika mashindano hayo kwa mabao 5-2 baada ya awali kufungwa mabao 3-1, huku Villarreal ikikaangwa 2-1 ilipocheza na Sevilla na kubwagwa nje kwa mabao 5-2 ambapo awali walifungwa mabao 3-1.


  Kwenye Ligi ya Mabingwa mambo yanatarajiwa kuwa matamu zaidi baada ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Real Madrid kupangwa na wapinzani wao wakubwa wa soka la Hispania, Atletico Madrid, katika mechi ya robo fainali.
 Timu hizo zilikutana katika fainali ya mwaka jana (2014), Real Madrid wakisubiri dakika 120 kuwapiga vijana wa Diego Simeone. Real walifuzu hatua ya robo fainali kwa kuichapa Schalke ya Ujerumani, wakati Atletico walisubiri mpaka mikwaju ya penalti kuwafunga Bayern Leverkusen.
  Barcelona wao watakutana na kiboko ya Chelsea, yaani PSG huku FC Porto wakikutana na mzigo wa Bayern Munich na Juventus watapambana na AS Monaco ya Ufaransa iliyoitoa Arsenal.


  Mechi za robo fainali zitachezwa Aprili 14 na 15 na marudiano ni Aprili 21 na 22. Droo ya Nusu Fainali itafanyika Aprili 24 na Mechi zake kuchezwa Mei 5 na 6 na Marudiano ni Mei 12 na 13. Fainali ya michuano hii itachezwa Juni 6 katika dimba la Olympia jijini Berlin, Ujerumani.
  Kutokana na kukosa nafasi hiyo, Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema sheria ya mabao ya ugenini inapaswa kutumika baada ya muda wa nyongeza kuliko katika muda wa kawaida kama ilivyo sasa.
  Arsenal walienguliwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Monaco ya Ufaransa.


  Timu hiyo ilipoteza mchezo wao wa kwanza kwa kufungwa mabao 3-1 Februari 25 mwaka huu kabla ya kujirudi na kuifunga Monaco mabao 2-0 katika mchezo wao wa marudiano uliofanyika katika Uwanja wa Louis 11 wiki iliyopita.
  Wenger amesema sheria hiyo ilitungwa katika miaka ya 1960 na uzito wa bao la ugenini hivi sasa ni mkubwa. Bao la ugenini huwa linahesabika baada ya muda wa nyongeza katika mechi za mkondo wa pili kwenye michuano ya Kombe la Ligi hatua ya nusu fainali, lakini kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Uropa League sheria hiyo hutumika baada ya muda wa kawaida wa dakika 90 kumalizika.


  Wenger amesema timu mbili za Uingereza zimeondolewa katika michuano hiyo kwa sheria ya bao la ugenini, jambo ambalo wahusika wanapaswa kujiuliza na pengine kuangalia upya sheria hiyo.
  Kocha huyo aliendelea kudai kuwa wakati sheria hiyo ikitungwa katika miaka ya 1960 ilikuwa na madhumuni ya kuzifanya timu kushambuliana lakini soka hivi sasa limebadilika.