*TAKUKURU wajiandaa kumfikisha mahakamani muda wowote

*Anatuhumiwa kuendesha ufisadi wa kutisha Hifadhi ya Ngorongoro

*Dk. Hoseah asema wanakamilisha taratibu, yeye aeleza mshangao

Mtikisiko mkubwa utaikumba nchi muda wowote kuanzia sasa, baada ya kuwapo taarifa kuwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) inajiandaa kumfikisha mahakamani mwanasiasa mkongwe, Pius Msekwa, kwa tuhuma za ufisadi.

Habari zisizotiliwa shaka kutoka TAKUKURU zinasema taasisi hiyo imekamilisha uchunguzi wa kina, uliochukua zaidi ya mwaka mmoja na sasa inasubiri kukamilisha taratibu za kiutawala kumfikisha Msekwa kortini.

 

Msekwa anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake alipokuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kipindi cha miaka sita hadi mwaka jana.

 

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, alipoulizwa na JAMHURI juu ya taarifa za uwezekano wa kumfikisha mahakamani Mzee Msekwa kwa ufisadi, alisema: “Ninachofahamu ni kwamba uchunguzi umekamilika, ila hatujafikia uamuzi wa kumfikisha mahakamani. Bado kuna taratibu tunazokamilisha.”

 

Dk. Hoseah alipododoswa, alisisitiza kuwa taratibu zinakamilishwa na si muda mrefu Watanzania watashuhudia hilo likitokea kama kila jambo litakwenda sawa na mwelekeo wa uchunguzi ulivyo. Hakutaka kuingia katika undani wa suala hili wala kutaja tuhuma zinazomkabili Msekwa.

 

Kwa upande wake, Msekwa alipowasiliana na JAMHURI, alisema: “Hii ni habari mpya kwangu. Wananipeleka mahakamani kwa kosa gani?” JAMHURI ilipomweleza tuhuma zinazomkabili, aliomba apewe muda aweze kupata chakula cha mchana Jumamosi, lakini baada ya chakula akasema anakwenda kwenye shughuli na hakuwa katika nafasi nzuri kulizungumzia suala hilo.

 

Moja ya tuhuma kubwa zinazomkabili na zitakazompandisha kizimbani ni kutumia mamlaka yake na jina la Rais vibaya, kumgawia mwekezaji eneo la kujenga hoteli katika Hifadhi ya Ngorongoro.

 

Kutokana na hali hiyo, jina halikujumuishwa katika orodha ya majina ya watu wanaopendekezwa na kupelekwa Ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete. Muda wa Bodi hii uliisha Oktoba 5, mwaka jana, na hadi sasa Ngorongoro haina Bodi.

 

Msekwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM-Tanzania Bara), amekuwa akituhumiwa kwa uongozi mbovu ambao Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele (CCM), mwaka jana alidiriki kusema Msekwa amevuruga kabisa Mamlaka hiyo. Kwa muda wote huo Kaika amekuwa akitajwa kuongoza mashambulizi dhidi ya Msekwa.

 

Kwa muda mrefu wabunge wengi wa CCM na upinzani wamekuwa wakipiga kelele wakihoji uadilifu wake, hasa kwa kutoa vibali vya kuruhusu ujenzi wa hoteli kwenye kingo za Bonde la Ngorongoro na katika mapito ya faru.

 

Katika Bunge la Bajeti mwaka jana, Telele aliendeleza mashambulizi dhidi ya Msekwa, na kumsihi Rais Jakaya Kikwete asimwongezee muda mwingine wa uenyekiti.

 

Telele alisema Msekwa ameifanya Ngorongoro kama mali yake, huku akishindwa kuwasaidia watu wa jamii ya Wamaasai ambao wanaishi katika Mamlaka hiyo kwa mujibu wa sheria.

 

Kaika amerejea kauli hiyo alipozungumza na JAMHURI kwa kusema, “Msekwa anaburuza watu, Shirika limerudi nyuma, maeneo anatoa tu kienyeki kwa wawekezaji, malisho ya wanyama anagawa, kama atamaliza muda wake, Mheshimiwa Rais atuteulie mwenyekiti mwingine mwenye manufaa.”

 

Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso (Chadema), kwenye Bunge lililopita alihoji matumizi ya Sh milioni 200 zilizotumiwa na Bodi kwa safari za nje ya nchi wakati muda wake wa kuwapo madarakani ukikaribia ukingoni.

 

Jambo jingine linalozua mjadala mkali ni kutokuwapo kwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, baada ya aliyekuwapo, Bernard Murunya, kuondoka. Kwa sasa Murunya ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Pamoja na Pareso, Mbunge mwingine aliyehoji kutokuwapo kwa mtendaji huyo ni Beatrice Shellukindo (Viti Maalumu-CCM).

 

Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka jana, ilithibitisha kuwa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaingilia utendaji wa kazi wa menejimenti.

 

Msekwa ajibu mapigo

Suala hili limefukuta muda mrefu kwani mwaka jana Msekwa alijibu tuhuma zinazoelekezwa kwake na baadhi ya wabunge, juu ya uongozi wake wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

 

Agosti, mwaka jana, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dodoma na kumjibu Telele na wabunge wengine, akisema kwamba kauli alizotoa bungeni dhidi yake ni fitina yenye uongo ndani yake. “Ni aina ya uongo unaoitwa usongombwingo,” alisema.

 

“Maneno yaliyonukuliwa na magazeti kwamba yalisemwa bungeni na Mheshimiwa Telele yalikuwa na lengo la kuchafua jina langu mbele ya umma. Yalikuwa ni maneno ya kashfa dhidi yangu, yaliyojikita katika kuchafua historia ya muda mrefu ya uadilifu wangu katika kutekeleza kazi za umma nilizopangiwa katika nyakati mbalimbali na marais wangu, kuanzia Rais Nyerere hadi Rais Kikwete,” alijitetea.

 

Alisema hakuweza kufika bungeni Dodoma wakati Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwasilisha bajeti yake, kutokana na kazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hoteli za kitalii ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na si kugawa viwanja kwa wawekezaji.

 

Alisema pia alikuwa akikagua miradi mingine inayotekelezwa kwa fedha za NCAA ikiwamo Shule ya Sekondari ya Nainokanoka, ambayo imekuwa ikijengwa kwa muda mrefu bila kukamilika.

 

“Hii ni kazi muhimu zaidi kuliko kukaa tu kwenye Gallery ya Bunge na kulipwa posho za kusikiliza hoja mbalimbali za wabunge zinazoelekezwa kwa Waziri,” alisema.

 

Akanusha kutumia jina la Rais

Tuhuma nyingine ambayo Msekwa aliikanusha ni madai kwamba alitumia jina la Rais Kikwete kuhalalisha utoaji wa maeneo ambayo ni mapitio ya wanyama kujengwa hoteli.

 

Alisema Desemba 28, 2006 alikutana na Rais Kikwete pamoja na Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Murunya, wakati huo akikaimu nafasi hiyo, na kiongozi huyo wa nchi aliwapa maagizo ambayo yaliwasilishwa kwenye mkutano wa bodi kwa waraka maalum.

 

“Katika waraka huo, maelekezo ya Rais kuhusu haja ya kuongeza idadi ya vitanda katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro yameainishwa waziwazi,” alisema.

 

Alisema maombi ya kujenga hoteli kwenye mapitio ya wanyama yaliwahi kutolewa na Bodi iliyokuwapo wakati huo, lakini mradi ulizuiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

 

“Tunaendelea kutekeleza uamuzi wa NEMC kwa kutoruhusu hoteli yoyote nyingine kujengwa katika mapitio ya wanyama. Ndiyo sababu katika orodha ya viwanja vilivyogawiwa na Bodi katika mkutano wake wa 87 wa Oktoba 2007, hakuna kiwanja chochote kilichopo kwenye mapitio ya wanyama kama Mheshimiwa Telele anavyodai,” alisema.

 

Kuhodhi kazi za menejimentiMsekwa alisema hajawahi kufanya kazi za watendaji na kwamba tuhuma hizo si za leo, kwani zilianza muda mfupi tu baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi.

 

Alisema baada ya siku 100 tangu kuteuliwa kwake, alimwandikia waraka Waziri husika ambaye wakati huo alikuwa Anthony Diallo, akimweleza jinsi atakavyofanya kazi na kwamba amekuwa na utaratibu wa kutoa taarifa ya Bodi yake kila baada ya muda fulani kwa waziri.

 

Alisema tuhuma hizo ziliendelea hata baada ya Waziri Jumanne Maghembe kuhamishiwa katika wizara hiyo, na kwamba waziri huyo alifanya uchunguzi na kubaini kuwa hazina ukweli wowote.

 

Msekwa aliongeza kuwa hata kikao cha Bodi kilichojadili tuhuma hizo, kilizitupilia mbali na kwamba anamshangaa Telele ambaye wakati huo alikuwa mjumbe kuziibua upya, hali akifahamu kwamba zilikuwa zimeshawekwa kando.

 

Alisema Ngorongoro haiwezi kufia mikononi mwake kwani tangu alipochukua uenyekiti wa Bodi, ameongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato kutoka Sh bilioni 17.79 mwaka 2005/2006 hadi Sh bilioni 48.7 mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2011.

 

Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), naye alikuwa akitoa wito bungeni wa kuvunjwa kwa Bodi ya NCCA kwa maelezo kwamba ilikuwa imekiuka ushauri wa NEMC kwa kuruhusu ujenzi kwenye mapitio ya faru.

 

Msekwa alikuwa Katibu wa Bunge wa Kwanza mwaka 1961, kisha akawa Mtendaji wa Kwanza wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kati ya mwaka 1967 hadi 1970, akawa Katibu Mtendaji wa CCM ilipoanzishwa mwaka 1977 hadi 1980.

 

Baadaye alishika vyeo vingi ikiwamo ukuu wa mkoa, ubunge, ukatibu mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, na mwaka 1991 alichaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge na hatimaye akawa Spika wa Bunge hadi mwaka 2005, alipotolewa na Samuel Sitta akiitwa “Agano la Kale.”

 

Baadaye Msekwa alipotea kwenye siasa, hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM baada ya Sekretariati iliyokuwa ikiongozwa na Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, kuvunjwa. Mwaka 2012 Msekwa naye alistaafishwa wadhifa huo, ukachukuliwa na Philip Mangula.