Wakati huu wa harakati za kutoa maoni ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni wakati mwafaka kutafakari kama mashindano ya ‘Miss Tanzania’ yanaikosea Tanzania.  Mwaka 1964 Serikali ilipiga marufuku mashindano hayo lakini yakaibuka kinyemela mwaka 1994 kwa mfano wa Azimio la Zanzibar, lililoibuka mwaka 1992 bila mwafaka wa kitaifa, na kuathiri Azimio la Arusha lililozaliwa mwaka 1967.

Shabaha ya mashindano hayo iliwahi kufafanuliwa na Rais Jakaya Kikwete, Septemba 2006 aliyesema, “… ni lazima iendane na misingi ya utamaduni wa Kitanzania ikiwa ni pamoja na kuzuia uvaaji wa vichupi katika mashindano hayo.”  Na ni kweli kwamba kifungu Na. 176 (6) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, kinaharamisha mtu yeyote kutenda, bila sababu halali kisheria, kitendo chochote cha aibu hadharani, kikiwamo kuonesha uchi.


Adhabu yake ni faini au kifungo au adhabu zote mbili kwa pamoja. Mashindano hayo huanzia kwenye kitongoji, baadaye wilaya, mkoa, kanda hadi taifa, shabaha ikiwa ni kupata mwanamke wa mvuto kabisa, majibu ya washindani papo kwa hapo, mwisho tathmini ya majaji.

 

Miongoni mwa maswali ambayo washindani wamekuwa wakiulizwa ni pamoja na,

“Unaona rangi gani nzuri kupita zote, unatokea mkoa gani, tupe sifa za mkoa wako, ni gauni gani utalichagua kwa kutokea jioni, utamwambiaje mgeni anayeingia kwa mara ya kwanza, utakuwa wapi baada ya miaka kumi…” Si maswali ya ujuzi kama kumtajia mgeni eneo la Tanzania, nchi ambazo Tanzania imepakana nazo, idadi ya milima, maziwa na mito, viwanja vya ndege, magarimoshi, upekee wa Tanzania, na kadhalika.


Kuhusu majaji, umma haujui vizuri kama ni vigezo gani vinawawezesha kuwa majaji wanaostahili kutoa uamuzi. Kumekuwapo malalamiko ya watu kwamba majaji wakati mwingine hufanya upendeleo usiostahili.


Kuhusu mashindano yenyewe, yakivuliwa hisia za urembo, yatabaki na ganda tupu. Kwamba mashindano hayo yanawapatia wanafiki kuridhisha tamaa zao za ukware kwa kupagawishwa na vichupi, nguo zinazobana na kuonesha maumbo ya kike.


Mifano miwili iliyochapishwa kwenye magazeti inatosha kuelezea. Wa kwanza: “MSHIRIKI MISS TANZANIA AONESHA MAKALIO JUKWAANI! Baadhi ya mashabiki waliofanikiwa kuona makalio hayo na kichupi hicho, waliibua shangwe zilizomfanya binti huyo azidi kukatika akiamini kuwa mauno yake yalikuwa yakiwakosha mashabiki hao.


Hata hivyo, baadhi ya mashabiki walimponda binti huyo…”  Wa pili: “PATI MSS TZ…Pati hiyo ilifanyika … na kuhudhuriwa na mastaa kadhaa wa kike na kiume ambapo baadhi yao walifanya mambo ya laana kiasi cha kuwafanya wastaarabu wachache… kuinamisha nyuso zao kwa aibu… mastaa hao wakipata kilevi, kukumbatiana, kubusiana na kulishana vyakula kwa kutumia midomo… walifunika kwa kuvaa vivazi vya ajabu vilivyoacha sehemu ya miili yao wazi na kupita navyo huku na huko ukumbini hapo bila kuona aibu …”  Misimamo ya kiserikali na kijamii inatatanisha.


Mwaka 2002, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii aliahidi kuwa Wizara yake itagharimia Miss Tanzania katika ziara ya Mbuga za Wanyama kutangaza vivutio vya utalii.

Utata mwingine: “Mashindano ya urembo yafutwe – Mbunge; Miss Tanzania aalikwa bungeni; Waziri … ashabikia ‘nusu uchi’?; Kikwete vichupi ‘No’; TBL yamwaga milioni 73 Miss Tanzania 2007”; nakadhalika.


Mashindano ya Miss Tanzania yamezalisha mashindano mengine: “Msichana mwenye tamanisho kuliko wote” na “Kapera mwenye tamanisho kuliko wote”.


Matangazo mengine katika magazeti:” Skendo 10 za warembo; PICHA ZA FARAGHA MTANDAONI.”  Wanaopinga mashindano hayo wanatoa hoja kwamba yanaisababishia Tanzania uozo wa maadili na ubaguzi kinyume cha ibara ya 13 (4) na (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inaharamisha ubaguzi kwa maana kwamba watoto wa maskini hata wakiwa warembo kiasi gani hawawezi kupata pesa za kushiriki mashindano hayo, kwa kununua nywele na kope za bandia, vipodozi; kuzungumza, kutabasamu na kucheka Kiingereza, kuchanganya Kiswahili na Kiingereza, nakadhalika.


Kuna hoja nyingine ya kupinga kikatiba. Kwamba neno ‘Tanzania’ halijafafanuliwa katika ibara ya 151 ya Katiba ya Muungano. Ibara hiyo inafafanua maneno ‘Tanzania Bara’ na ‘Tanzania Zanzibar’.


Ingawa ibara ya 1 ya Katiba hiyo inatamka kwamba Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 2 ya Katiba ya Zanzibar, ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010, inatamka kwamba Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar inafafanua kwamba Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba, visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilikuwa ikiitwa ‘Jamhuri ya Watu wa Zanzibar’.

 

Kwa hiyo, ni sahihi kabisa kuuliza kama mashindano ya Miss Tanzania yanahusu ‘Tanzania Bara’ na ‘Tanzania  Zanzibar’; kuuliza kama neno ‘Tanzania’ katika “Miss Tanzania Contest” ni matumizi mabaya ya neno hilo na ni kinyume cha Katiba ya Muungano. Izingatiwe kwamba ‘Utamaduni’ siyo suala la Muungano.


Mashabiki wa Mashindano ya Miss Tanzania wanatoa hoja kwamba mashindano hayo yanapandisha hadhi ya Tanzania kimataifa kwa kuvutia watalii wengi nchini, yanatutengenezea ajira kama vile maonesho ya mitindo, nakadhalika.


Lakini kuna hili kwamba, kama mashindano hayo ni kitu cha hekima na busara sana, basi tufanye mashindano hayo kutafuta ni yupi mwanamke mzuri sana katika makundi mbalimbali ya wanawake waliolewa, watalaka, wajane, wabunge, wafanyakazi wa Serikali, mahakimu, majaji, mawakili, polisi, askari jela, wafungwa, walimu, wauguzi, wanafunzi wa chekechea na shule za msingi.


Tunaweza kuendelea na makundi ya wanyama wa kike kwa uzuri tukashindanisha ngedere, nyani, sokwe, fisi, kenge, ngiri, kiboko, panya, nakadhalika. Pengine kama mnyama mzuri sana wa kike angeishachaguliwa kabla ya mwaka 2002, mshindi wa Miss Tanzania angepeana mkono na miss Fisi au Miss Kenge.

Taarifa imetolewa kwamba, tangu mwaka 1994, washindi wa Miss Tanzania ni 17. Pengine kila mmoja wao achunguzwe nini cha kutukuzwa alichokifanyia Tanzania bila unafiki kabla na baada ya kuwa Miss Tanzania.


Kwa vyovyote, kuna mshindi mmojawapo ambaye miaka karibu sita tangu awe Miss Tanzania, ameapa kuwa hataachana na maonesho ya vichupi.

Wanaoshabikia “Urembo Kwanza” watahadharishwe kwamba kuwa mrembo hakuhakikishii mtu mafanikio maishani, na kwamba kuwa na sura mbaya hakumaanishi kamwe kutokufanikiwa.


Kuna mfano wa kutokusahaulika wa mwanamuziki maarufu nchini, Dk. Remmy Ongala. Miaka michache iliyopita (kabla ya kufariki), alishiriki mashindano ya wenye sura mbaya. Alisikitika sana kwamba alichukua nafasi ya pili badala ya kwanza.

Kutofaulu huko hakujazungumzwa kwamba kuliteteresha kuimba na kuimbisha kwake na hilo halijawa hoja ya kushabikia kutaka kujua kama udaktari wake alitunukiwa na chuo cha taaluma au la!

0784 312623