Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mashindano ya kitaifa ya wazi kwa mchezo wa kuogelea yamehitimika rasmi kwa kishindo Jumapili ya Septemba 15, 2024 katika bwawa la shule ya kimataifa ya Tanganyika iliyoko mlMasaki, Dar es Salaam.

Mashindano hayo yamefanyika ikiwa ni sehemu ya kalenda ya Chama cha Kuogelea Nchini kwa mwaka huu na yanakuwa mashindano ya kwanza kwa mwaka 2024/2025.

Mashindano hayo yameshirikisha jumla ya waogeleaji 238 kutoka vilabu 16 ambavyo 14 kati yake ni kutokea hapa nchini na vilabu viwili pekee vikiwa ni vilabu kutoka nchi jirani za Kenya pamoja na Uganda.

Akizungumza na Jamhuri Digital Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa Kuongelea nchini Mhandisi David Mwasyoge ameonekana kufarajika na viwango vilivyoonyeshwa na waogeleaji kwa mwaka huu.

Mwenyekiti Mwasyoge alianza kwa kuwapongeza washiriki wote wote kushindana na pia kuvishukuru vilabu viwili vigeni ambavyo vimetoka nchini Kenya na Uganda kuja kushiriki mashindano hayo kwani vimesaidia kuongeza hali ya ushindani kwa waogeleaji.

“Kwanza tumefurahi vijana wakionyesha ushindani na niwapongeze waogeleaji wameonyesha viwango vizuri. Mashindano ni muhimu kwa waogeleaji ili kutoa tathmini halisi ya viwango vyao kujua wamefika wapi na wapi wanatakiwa waongeze nguvu na kuboresha zaidi. Kwabhiyo tunafarijika zaidi kuona kwamba tuna timu kutoka nnje ya Tanzania, Kenya na Uganda zimekuja kuongeza ushindani na hiyo inawapa changamoto nzuri waogeleaji wetu”

Aidha mwenyekiti Mwasyoge aliongeza pia kwa kuzungumzia adhma yao ya kupeleka idadi kubwa ya waogeleaji katika mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2028.

“Kupitia ushindani uliopo kwa sasa kwa waogeleaji wetu sisi kama chama tunaona mwaka 2028 kwa mipango tuliyonayo kwa vijana wetu na ikizingatiwa kuna vijana wa miaka 12 mpaka 15 wana muda mzuri sana kiasi kwamba inatupa moyo kuwa kwa mwaka 2028 tunazimia kupeleka vijana wengi zaidi kwenye mashindano ya Olimpiki na angalau tuweze kufika hatua ya nusu fainali” amesema.

Pia kwa upande mwingine miongoni mwa mambo ambayo amegusia mwenyekiti Mwasyoge ni suala la changamoto kubwa ya miundombinu iliyokuwepo na mpaka sasa suala hilo liko katika mikono ya serikali na linafanyiwa kazi ambapo wameelekezwa kuwa kupitia ukarabati mkubwa unaofanywa na serikali katika uwanja wa Benjamin Mkapa serikali imekusudia pia kujenga bwawa lenye ukubwa wa mita 50 ambalo litasaidia kuendesha shughuli mbalimbali za mchezo wa kuogelea.

Pamoja na hilo pia mwenyekiti ameeleza kuwa kupitia kituo cha michezo cha Samia academy kilichopo visiwani zanzibar kupitia ukarabati wake wamearifiwa kuwa kutakuwa na bwawa la Olimpiki lenye ukubwa wa mita 50 litajengwa pia ambapo litasaidia mchezo wa kuogelea.

Lakini mbali na suala hilo la miundombinu mwenyekiti Mwasyoge amesema pia bado wanaendelea kuwekeza kwa wakufunzi ili kuweza kutoa mafunzo sahihi kwa waogeleaji.

“Bado tunaendelea kuwekeza kwa makocha wetu ili kuweza kutoa mafunzo sahihi kwa sababu uogeleaji unaanzia chini ukianza vibaya huku juu kubadilika inakuwa ngumu. Kwahiyo tumewekeza nguvu zaidi kwa walimu ambao watakuwa wanachukua watoto wadogo kuanzia miaka mitatu mpaka mitano kuongeza nguvu kazi ya walimu ili waweze kuwapa misingi sahihi ambazo zitawafanya waogeleaji wakifika ngazi za juu kufanya vizuri zaidi.” Aliongeza kwa kusema hayo mwenyekiti Mwasyoge.

Kwa upande mwingine muwakilishi wa timu kutoka nchini Uganda ijulikanayo kama Ozpreys aliyejitambulisha kwa jina la Asima Gabriella akizungumza mara baada ya mashindano ameonekana kufurahia ushindani walioupata kama timu kutoka kwa waogeleaji wa vilabu vingine pia .

“Mashindano yalikuwa mazuri na yenye ushindani ukilinganisha na mara ya mwisho tulivyokuja na imekuwa ni furaha pia kukutana na watu niliokutana nao mara ya mwisho tulivyokuja kushiriki na pia imekuwa ni sehemu nzuri kwetu kuja kushindana.”

Mashindano hayo yalihitimishwa kwa ugawaji wa zawadi za medali kwa wachezaji wote waliofanya vizuri katika mashindano hayo pamoja na uvunjwaji wa rekodi mbalimbali zilizokuwa zimewekwa na waogeleaji wengine hapo awali.

Miongoni mwa waogeleaji wachache kati ya wengi waliofanya vizuri katika mashindano hayo ni:

Muogeleaji wa kimataifa wa Tanzania Collins Saliboko kutoka klabu ya Dar swimming club, amefanikiwa kuvunja rekodi mbalimbali za mashindano hayo zilizokuwepo hapo awali.

Delbert Ipilinga muogeleaji kutoka klabu ya talliss (Ist) ambaye nae amefanikiwa kushinda medali mbalimbali ikiwemo ya fedha na dhahabu pamoja na kuvunja rekodi zake binafsi alizoziweka katika mashindano hayo siku za nyuma.

Aryiel Angemi muogeleaji wakike mwenye umri wa miaka 12 kutoka klabu ya talliss Ist ambaye amefanikiwa pia kuwa mshindi wa jumla wa medali ya dhahabu katika waogeleaji wenye umri kati ya 11-12.

Fidel Kavishe muogeleaji kutoka klabu ya primier swimming club ya hapa nchini kutokea mbweni dsm. Muogeleaji huyo amefanikiwa kushinda ya medali ya fedha na shaba katika vipengele tofauti tofauti vya mashindano hayo.

Samba Mhina muogeleaji kutoka klabu reptide kutoka jijini Arusha. Muogeleaji huyo amefanikiwa kushinda medali fedha ambapo pia amefanikiwa kuvunja rekodi binafsi alizoziweka katika mashindano yaliyopita siku za nyuma.

Mashindano hayo ya wazi ya kitaifa kwa mchezo wa kuogelea yalifanyika kwa takribani siku mbili kuanzia septemba14 na kuhitimika rasmi jumapili ya jana septemba 15.

Please follow and like us:
Pin Share