Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar Salaam

Chama cha Mchezo wa Kuogelea Africa (Africa aquatics) kwa kushirikiana na mchezo wa kuogelea nchini vitaendesha mashindano ya wazi kwa mchezo wa kuogelea yanayotarajiwa kufanyioa visiwani Zanzibar.

Mashindano hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza nchini katika historia yakiwa na lengo la kueneza na kukuza mchezo huo wa kuogelea katika nchi zote za Afrika.

Aidha mashindano hayo pia yanaenda sambamba pia na utoaji mafunzo kwa makocha pamoja na waogeleaji wa mchezo huo.

Akizungumza mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo ya wazi Thauriya Diria amesema kuwa mashindano hayo yamekuja mara baada ya mazungumzo kati ya Rais ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt Hussein Mwinyi pamoja naye Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea dlDuniani Hussain Al Musallam ambapo miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni kuendesha mashindano ya wazi visiwani humo kwani kwa kiasi kikubwa ardhi ya Zanzibar imezungukwa na bahari asilia na idadi chache ya mabwawa ya mchezo wa kuogelea.

“Alipokuja Rais Hussain wa Chama cha Kuogelea Duniani alipoonana na Rais wa Zanzibar Dk Mwinyi alimuahidi kuwa atataka kufanya mashindano ya wazi hapa Zanzibar kwani kuna maji na hakuna mabwawa hivyo huu ni mpango wa kuhakikisha watu wanaogelea sana na kuona Zanzibar inatoa waogeleaji mahiri watakaoweza kushindana kuogelea baharini” amesema.

Mashindano hayo yanafanyika mara baada ya maagizo kutoka Chama cha Kuogelea cha Dunia kwenda kwa chama cha Kuogelea Afrika.

Hatua hiyo inatajwa kama muendelezo wa jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ufunguaji milango ya fursa kupitia michezo.

Mashindano hayo yanatarajia kuhusisha waogeleaji kutoka mataifa yote ya Afrika ambapo waogeleaji watashindana kuogelea katika eneo la bahari huko visiwani Zanzibar.

Mashindano hayo ya wazi ya kuogelea yanatarajiwa kufanyika Septemba 21 mwaka huu katika eneo la bahari ya Madinat Al bahr iliyoko mbweni huko visiwani Zanzibar.

Please follow and like us:
Pin Share