Masheikh 11 wa madhahebu ya Shia Ithna Sheria katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Kagera,Tabora, Kigoma, Dodoma na Katavi wamepewa vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 80. 
 
Vitendea kazi hivyo pikipiki aina ya Freedom vilikabidhiwa jana kwa mashaeikh hao na mlezi wa taasisi ya The Bhakhiyatullah Foundation ya jijini Mwanza Alhaji Sibtain Meghjee hafla iliyofanyika kwenye ofisi za Bilal Muslim Mission of Tanzania Mwanza.
Akikabidhi pikipiki hizo Sibtain ambaye ni Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation aliwataka wakazitumie kutembelea jamii na kuibua kero na changamoto zinazoikabili bila kujali imani zao za dini kwenye maeneo yao na kisha kutoa taarifa na maoni ya utatuzi wa changamoto hizo.
“Pikipiki hizi mmekabidhiwa na nyaraka zote mkazitumie vizuri kwa kuhudumia jamii na isiwe kwa waislamu tu bali na waumini wa dini zote na sisi tunatoa huduma bila kubagua.Mzitumie vizuri ili na wengine waweze kupata lakini mkishindwa mtasababisha wakose,”alisema Meghjee na akawataka watoe mrejesho wa matokeo chanya yatakayopatikana kwenye jamii baada ya miezi sita tangu wakabidhiwe pikipiki hizo.
Wakizungumza baada ya kupokea msaada huo baadhi ya masheikh walisema mbali na kuzitumia kuibua changamoto kwa waumini wao na jamii ya waumini wa dini zingine zitawasaidia kuwaingizia kipato.
“ Tofauti na zamani sasa kazi itakuwa rahisi kutokana na vipandwa (vifaa) hivi vya usafiri ambavyo vitaturahishia kuwafikishia ujumbe wa Allah (Mungu) waumini wetu lakini pia tutawafikia kwa urahisi watu mbalimbali kwenye maeneo yetu na kuibua kero na changamoto zao. Tunawashukuru wafadhili waliotovitoa,”alisema Sheikh Hussein Thuqumali wa TBF.
Naye Sheikh Daud Daud wa Mantare Kwimba alisema wanashukuru The Desk & Chair na BFT kutambua changamoto na mazingira magumu wanayofanyia kazi na vitendea kazi hivyo vitayarahisisha mazito na kuyafikia kwa urahisi ingawa pia wamepewa uhuru wa kuvitumia kujitafutia vipato pamoja na kuhudumia jamii kiroho na hivyo akamwomba Mwenyezi Mungu awajalie waliovitoa kwa maslahi ya jamii ya dini zote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa BTF Sheikh Hashim Ramadhan alisema vitendea kazi hivyo vimetolewa kwa lengo la kupigania amani na kusimamia maadili kwenye jamii kutokana na changamoto wanazopata watu wema waliobakia duniani na waja wa kiroho wa Mwenyezi Mungu ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha Hadija, mke wa Mtume Muhamad S.A.W.
“Kwa sababu ya moyo wa imani ya Mwenyezi Mungu na mafundisho , chochote unachokitoa kwa heri, amani ili kuokoa maisha ya binadamu unakuwa umewekeza kwa Mwenyezi Mungu.Ni muhimu na hakuna jambo jema kama kusaidiana kwenye shida na taabu, kikubwa ni kusafisha nyoyo za watu wote wapate kusaidiana,”alisema Sheikh Hashim
Sheikh huyo wa Bilal Muslim Kanda ya Ziwa aliwaasa waumini wa dini mbalimbali, Waislamu na Wakristo kuacha ubahiri na badala yake watoe sehemu ya mali wanazomiliki kwa mujibu wa vitabu vyote vya dini ili wawasaidie maskini, yatima na wajane wanaoishi kwenye mazingira magumu ili wapate amani ya roho.
Akizungumzia masheikh hao kuingia mkataba na TBF kuhusu pikipiki hizo alisema wamefanya hivyo ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza baadaye na zitakuwa mali ya taasisi na hawataruhusiwa kumpa (kummilikisha) mtu mwingine.
“Mikataba ya umiliki pamoja na matumizi ya pikipiki hizo inalenga kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza hapo baadaye. Leseni, mafuta na matengenezo itakuwa juu ya mtumiaji na pikipiki itatakiwa kuhifadhiwa kwenye kituo cha sheikh anakofanyia kazi,”alisema Sheikh Hashim.
Mwenyekiti wa taasisi ya The Bakhiyatullah Foundation (TBF) ya jijini Mwanza Sheikh Hashim Ramadhan akizungumza na baadhi ya masheikh kabla ya kuwakabidhi pikipiki kwa ajili ya usafiri. Kulia ni mfadhili aliyetoa pikipiki hizo Sibtain Meghjee wa The Desk & Chair Foundation tawi la Tanzania na mwenye kilemba ni Maulana (waliokaa) wa pili kushoto Sayyed Amir Abass Bakri.
Sheikh Hussein Thuqumali wa TBF akitia saini (mkataba) wa kumilikishwa pikipiki wanaoshuhudia ni Maulana Sayyed Amir Abbas Bakri katikati na Mwenyekiti wa The Bakhiyatullah Foundation (TBF) Sheikh Hasim Ramadhani.
Sheikh Daud Daud wa Lamadi Simiyu akipokea hati za pikipiki aliyokabidhiwa kutoka kwa Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Alhaji Sibtain Meghjee kulia.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Sibtain Meghjee akimkabidhi pikipiki Shekh Alhamud Said Athuman wa Mantare Kwimba .Katikati mwenye kilemba cheupe ni Sheikh Hashim Ramadhani ambaye ni Mwenyekiti wa The Bakhiyatullah Foundation.
Masheikh wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa pikipiki za usafiri kutoka taasisi ya The Bakhiyatullah (TBF) pikipiki hizo zimetolewa na The Desk & Chair kwa masheikh hao ili kuwasaidia usafiri waweze kuibua kero na changamoto kwenye jamii. picha Baltazar Mashaka