TAKRIBAN watu 25 wamefariki nchini Ukraine katika wimbi la hivi punde la mashambulizi ya Urusi, maafisa wa Ukraine wanasema, huku mzozo huo ukiwa hauonyeshi dalili zozote za kurudi nyuma.
Shambulio moja katika Mkoa wa Donetsk liliua takriban watu 11 na kujeruhi 40, wakiwemo watoto sita, maafisa wa eneo hilo walisema Jumamosi. Nyumba na miundombinu zilishambuliwa katika mikoa mingine, pamoja na Kharkiv na Odesa.
Mashambulizi ya Urusi yameongezeka katika siku za hivi karibuni, wakati Marekani ilipositisha msaada wa kijeshi na ushirikiano wa kijasusi na Kyiv. Ilifuatia majibizano katika ofisi ya Ikulu wiki iliyopita kati ya Rais Donald Trump na Volodymyr Zelensky wa Ukraine.
Baada ya mashambulio ya hivi punde ya Urusi, Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk alisema: “Hivi ndivyo hutokea mtu anapowafurahisha wapuuzi.”
“Mabomu zaidi, uchokozi zaidi, waathirika zaidi,” aliongeza katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii.
Mashambulizi mabaya zaidi yalitokea Ijumaa jioni katika mji wa Dobropillya Mkoa wa Donetsk. Takriban watu 11 waliuawa wakati makombora mawili ya balistiki yaliposhambulia majengo manane ya makazi na kituo cha maduka, maafisa walisema.
Baada ya huduma za dharura kuwasili, Urusi ilianzisha shambulizi jingine “ikiwalenga waokoaji kimakusudi”, Zelensky alisema katika ujumbe kwenye Telegram. “Mashambulizi kama haya yanaonyesha kuwa malengo ya Urusi hayajabadilika,” aliongeza.
Wakati huo huo Ukraine imeendelea kuilenga Urusi, ambayo wizara yake ya ulinzi ilisema kuwa vikosi vyake vilinasa ndege 31 zisizo na rubani za Ukraine usiku kucha.
Siku ya Ijumaa, Trump alisema anapata “ugumu zaidi, kusema ukweli, kujadiliana na Ukraine” kuliko Urusi katika majaribio ya kuleta amani kati ya mataifa hayo mawili.
Marekani “inaendelea vizuri sana na Urusi”, na “inaweza kuwa rahisi kuendeleza majadiliano na” Moscow kuliko Kyiv, aliwaambia waandishi wa Habari.
