Wapalestina wanaokaribia 70 wameuawa leo na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi makali ya anga ya vikosi vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.

Mashambulizi hayo yanatajwa kuwa makali tangu utawala mjini Tel Aviv ulipotangaza kurejea kwa operesheni ya kijeshi kwenye eneo hilo.

Takwimu hizo za vifo zimetolewa na maafisa wa afya wa Ukanda wa Gaza unaotawala na kundi la wanamgambo wa Hamas. Matibabu wamesema mashambulizi ya Israel yamezilenga nyumba kadhaa kaskazini na kusini wa Gaza hususani ksenye miji ya Khan Younis, Rafah na Beit Lahiya.

Hayo yanaripotiwa wakati Israel imesema hapo jana kwamba vikosi vyake vimeanzisha tena operesheni ya ardhini kwenye maeneo ya kaskazini na kusini mwa Gaza baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa tangu mwezi Januari.

Vilevile imesema inachukua tena udhibiti wa ujia muhimu wa Netzarim unaotenganisha upande wa kusini na kaskazini mwa ukanda huo, hatua ambayo kundi la Hamas limeitaja kuwa “ukiukaji wa kutisha” wa mkataba wa kusitisha vita.