Takribani Wapalestina 19, wakiwemo watoto wanane, wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel kusini mwa Gaza usiku kucha, wanasema maafisa wa afya wa eneo hilo.

Mama mmoja na watoto wake wanne waliripotiwa kuuawa katika kambi ya mahema ya watu waliokimbia makazi yao huko al-Mawasi iliposhambuliwa, huku wanandoa wengine na watoto wao wakiuwawa katika mji wa karibu wa Khan Younis.

Jeshi la Israel limesema lilifanya mashambulizi kadhaa kuwalenga wapiganaji wa Hamas walioshiriki katika shambulio la tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israel.

Mashambulizi pia yameripotiwa katikati na kaskazini mwa Gaza, huku wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas ikisema jumla ya watu 51 wameuawa katika eneo hilo katika muda wa saa 24 zilizopita.

Kaskazini mwa Gaza, miili ya watu wasiopungua sita, ikiwa ni pamoja na mtoto mchanga, ilitolewa kutoka katika nyumba mbili zilizoshambuliwa, kulingana na afisa wa Idara ya Ulinzi wa Raia unaoendeshwa na Hamas.

Wakati huo huo, watu watatu waliuawa katika shambulio katikati mwa mji wa Deir al-Balah, wakati mtoto mwingine mchanga aliuawa katika kambi ya wakimbizi ya Bureij ya mijini.

Hakuna taarifa ya mara moja kutoka kwa jeshi la Israeli juu ya mashambulizi hayo.

Israel ilianzisha mashambulizi ya kuiangamiza Hamas kujibu shambulio la kundi hilo la tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

Zaidi ya watu 45,930 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo.