Kila wakati uteuzi wa wachezaji wa Taifa Stars umekuwa ukiambatana na malalamiko ya mashabiki wa Simba na Yanga. Kocha yeyote yule atakayechagua timu ya taifa, lazima atajikuta akiangukia kwenye uadui na mashabiki wa Simba au wale wa Yanga.

Wachezaji wa Yanga wakiwa wengi uwanjani, mashabiki wa Simba wataishangilia Taifa Stars kwa shingo upande. Hali huwa hivyo hivyo ikiwa wachezaji wa Simba wakiwa wengi ndani ya kikosi cha kwanza cha Taifa Stars.

Fikiria tu hapo miaka miwili iliyopita. Hakuna kiongozi wa timu ya Ligi Kuu ya Cameroon anayeweza kuupinga uteuzi wa Clinton Njie anapoitwa kuichezea Indomitable Lions na ikitokea akajitokeza kiongozi wa kuupinga uteuzi huo, itabidi amuonyeshe kocha, mfungaji anayechezea timu ya nyumbani mwenye ubora kumzidi Clinton Njie.

Naja tu miaka miwili nyuma. Timu ya Taifa ya Nigeria tulipata kutoka nayo sare ikiwa imeundwa na baadhi ya wachezaji ambao hawapati namba katika kikosi cha kwanza. Kipindi hicho, Carl Ikeme, hukaa benchi wakati Vincent Enyeama anapokuwa tayari kuichezea Super Eagles. Haruna Lukman hukaa benchi wakati Ogenyi Onazi anapoitwa na kocha.

Nwankwo Obiora ilikuwa hawezi kupata namba iwapo Obi Mikel yupo tayari kucheza. William Ekong humpisha Godfrey Oboabona wakati adui ni wa kiwango cha juu. Wachezaji wanaopangwa kwenye mechi ngumu za Super Eagles, hata hawa ambao wanaonekana kuchukua nafasi zao, wote kwa ujumla ni wachezaji wa kulipwa.

Wameshaachana na Ligi Kuu ya Nigeria. Mechi ya kimataifa inapomalizika wanapanda ndege na kwenda kuchezea timu za Ulaya. Ni kweli kabisa wengi wao walianzia soka katika timu za Nigeria kabla ya kutazamwa na mawakala pamoja na makocha wa timu za nje ya Afrika.

Mashabiki wanaoambatana na timu ya Taifa ya Nigeria na nyingine kubwa za Afrika, wanazo timu za nyumbani wanazozishabikia, ambazo katika ukuaji wao walizishabikia na pengine mpaka leo bado ni wanazi wa timu hizo. Lakini huzifuata timu za mataifa wakiongozwa na taifa kwanza wala si klabu.

Tumeshawahi kucheza na Brazil ambayo iliundwa na asilimia kubwa ya wachezaji wanaocheza nje ya Brazil. Tukacheza na Ivory Coast iliyoundwa na kina Didier Drogba waliokuwa wakichezea Chelsea na kwingineko Ulaya. Tumecheza na Cameroon mara mbili katika Uwanja wa Taifa, iliundwa na wachezaji wanaocheza timu za Ulaya, kama walikuwepo wanaochezea timu za Ligi Kuu ya Cameroon basi walikuwa wamekaa benchi.

Tulicheza na New Zealand iliyoundwa na baadhi ya wachezaji waliokuwa wanachezea ligi za Ulaya. Tulitakiwa mpaka hivi leo tuwe tumeshaondokana na ushamba wa kutaka kuifanya Taifa Stars eti iwe ni mali ya Simba na Yanga pekee.

Kila siku tunaziona picha za Mbwana Samatta akipanda ndege na kuondoka kurudi Ubelgiji  baada ya kuichezea Taifa Stars mechi ya kimataifa. Bado hatumuonei wivu.

Akili zetu zimezama kwenye utani wa Simba na Yanga, timu ambazo hazijawahi kubeba kombe lolote lile la ngazi ya Bara la Afrika! Tutakapocheza na Nigeria mwaka 2020 kwenye mechi ya kutafuta nafasi ya kushiriki AFCON ya mwaka 2021, watatuletea wadogo zao  kina Vincent Enyeama na Obi Mikel watakaokuwa wanacheza Ulaya na kwingineko duniani.

Hofu yangu ni kwamba kuna uwezekano timu yetu ya taifa ikawa inaundwa na wachezaji hawa hawa wa Yanga, Simba na Azam FC. Wachezaji saba muhimu wa Taifa Stars ambao watakuwa wanakuja kwa ajili ya mechi za kimataifa na kuondoka, watatupunguzia kelele za mashabiki wa Simba na Yanga, ambao mawazo yao ya soka yanashindwa kwenda mbali zaidi ya ushindani wa ndani ya nchi hii.

Wiki moja kabla ya mechi ya watani, wanaanzisha zile siasa zao za kumlalamikia mwamuzi wakidai kuwa ana mapenzi na mojawapo ya timu kongwe, hivyo hataweza kuchezesha kwa haki.

Timu zetu kongwe za Kariakoo zinatusumbua sana kwa sababu hatuna ‘mapro’ wengi wa viwango vya Samatta. Tungekuwa nao tungezisahau hizi timu kila mara wakati mechi kubwa za Taifa Stars zinapokaribia.

Tungekuwa tunawasubiri kwa hamu mafundi wetu wanaocheza soka la kulipwa waje watupe burudani, halafu mechi ikimalizika wapande ndege na kurudi huko nje kusikokuwa na soka la ushabiki uliojaa majungu.

Upuuzi ule ule wa miaka michache iliyopita umejirudia tena mwaka huu. Kitu cha muhimu ni mchezaji kupangwa kulingana na mfumo ambao kocha mkuu anaona unafaa kutumika. Wenye dhamana ndani ya klabu zetu hawaumii mioyoni kuona Taifa Stars inaundwa na wachezaji wa humu humu ndani.

Shabiki au kiongozi wa Yanga au Simba ambaye bado kichwani kwake anapanga kikosi cha Taifa Stars huku akiwatazama wachezaji wa klabu anayoipenda bila hata kujiuliza kocha mkuu wa Taifa Stars anatumia mifumo gani, ni wa kumsikitikia na kumuonea huruma.

Anasumbuliwa na ugonjwa unaoitwa ‘unazi’. Bahati mbaya tunachelewa kupata wachezaji wengi wanaochezea timu kubwa za Ulaya na kwingineko.

Vinginevyo, shabiki au kiongozi huyo wa timu moja kongwe ya Kariakoo angeshajua jinsi gani timu anayoishabikia ilivyo ya kawaida sana duniani.

Tunaposhindwa kuwaza kimataifa kama wanavyowaza wale wanaozisahau timu zao za ligi kuu kwa faida ya timu za mataifa yao, tutaendelea kuridhika na mafanikio madogo ya timu zetu kila mwaka.