Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kondoa

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma kujiandikisha kwa wingi katika daftari la mpigakura ili kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi ya Kondoa Mji uliofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani wakati wa ziara yake wilayani humo aliwataka wananchi kupuuza watu wanaopiga porojo kuhusiana na utendaji kazi wa serikali.

“Mjitokeze siku ya kupiga kura ili muwachague viongozi wachapakazi na watakaoendeleza maendeleo anayoyaleta Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Akijibu changamoto zilizowasilishwa na Mbunge wa Kondoa Mjini, Ally Makoa kuhusiana na suala la upatikanaji wa maji, Masauni alisema serikali imeshasikia kilio cha wananchi wa Kondoa na yote waliyowasilisha yameanza kufanyiwa kazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kondoa Mjini, Makoa aliishukuru serikali kwa kuleta miradi ya kutosha katika sekta ya afya, elimu na umeme na kuiomba isaidie ujenzi wa daraja la Mto Bubu ili wananchi waendelee kiuchumi wakati wote.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Nyangasa alisema wananchi wa wilaya hiyo wataanza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpigakura kuanzia Oktoba 11 hadi Oktoba 20, mwaka huu na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vilivyoainishwa.