Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amewapa siku 14 Jeshi la Polisi Mkoani Lindi kuwaondoa wafugaji katika maeneo ya ambayo hayajatengwa na Serikali Wilayani Liwale kwa ajili ya shughuli za ufugaji.

Waziri Masauni ambaye pia aliambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi katika ziara hiyo, alitoa kauli hiyo leo Novemba 2, 2022 baada ya kuwepo na migogoro kati ya Wafugaji na Wakulima iliyosababisha vifo vya watu 12 Mkoani Lindi.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Linegene, Kata ya Mirui, Waziri Masauni amesema kitendo cha wafugaji kufanya shughuli za ufugaji katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kufanya kazi hizo ndio sababu ya kutokea mauaji hayo ambayo yanasababishwa na mifugo kuingizwa katika mashamba ya wakulima na kusababisha migogoro isiyoisha.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Linegene, Kata ya Mirui, Wilayani Liwale, Mkoa wa Lindi, leo Novemba 2, 2022. Ametoa siku 14 kwa Jeshi la Polisi kuwaondoa wafugaji katika maeneo ya ambayo hayajatengwa na Serikali Wilayani humo kwa ajili ya shughuli za ufugaji.

“Natoa siku 14 kwa Jeshi la Polisi, wahakikishe wafugaji wote waliopo katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kwa ajili ya ufugaji waondolewe haraka iwezekanavyo,” amesema Masauni

Aidha,Waziri Masauni amewataka Polisi kuwakamata wafugaji ambao wanatembea na visu, mapanga, panga, nondo, mikuki na michale maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo ambapo silaha hizo zinasababisha watu kujeruhiwa pamoja na mauaji.

“Kama mtu amechukua fimbo, mkuki na kisu anakukimbiza maana yake ni nini, hivi una uhakika gani kuwa akikukamata atakuua, mtu akifikia kiwango cha kutaka kuua huyo si muuaji anawezaje kwenda polisi alafu akachukuliwa ni mwizi wa kuu, Polisi wawachukulie hao ni wauaji,” amesema Masauni.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wafugaji waliopo Wilayani humo kuondoka haraka iwezekanavyo katika maeneo yote ambayo hayaruhusiwi kwa ajili ya mifugo.

“Mimi ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi lakini sipendi kuona wafugaji wanaleta taharuki katika nchi hii, wanavunja sheria, wanapaswa kufanya ufugaji unaotambulika, kwanini tufanye kiuhalifu, haiwezekani, lazima tuishi kama watu na sio kuishi kama wanyama, yeyote anayelisha shamba la mtu, huyo akamatwe ashughulikiwe vizuri, apigwe faini, afungwe, acheni mambo ya kitoto kama hayo,” amesema Ndaki.

Naye Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini, CP Awadhi Haji amesema Jeshi la Polisi haliwezi kuchezewa hivyo Jeshi litachukua nafasi yake kwa kuwakamata wanaofanya uhalifu Wilayani humo ikiwemo kuanza na wafugaji wanaotembea na silaha Wilayani humo.

“Narudia tena, tutafanya operesheni ya nyumba kwa nyumba na pia tutawakamata wafugaji wanaotembea na silaha, wananchi endeleeni kutupa ushirikiano katika kupambana nah awa wahalifu,” amesema CP Awadhi.

Mkazi wa Kata ya Mirui, Joseph Abdalla amesema Wafugaji katika Kijiji hicho wameingiza ngombe katika shmaba lake na kumsababishia hasara kubwa, hata hivyo alivyolalamika wakati afugaji hao wanafanya uhalifu huo walimjibu kuwa hawana sehemu ya kulisha mifugo hiyo.

“Hali tuliofikia ni mbaya sana, wafugaji wanaingiza mifugo shambani kwangu na pia kunitisha na hawana woga kabisa, shmaba langu limemalizwa na mifugo, nimelalamika kwanini mnaingiza ngombe katika shamba langu, wakanijibu sasa sisi tukalishe wapi, majibu gani haya, kwani mimi ndio nawatafutia malisho mifugo hiyo?,” amelalamika Joseph.

Mawaziri hao wanaendelea na ziara katika Mkoa huo ili kudhibiti mgogoro wa wakulima na wafugaji ambao unaendelea kuleta madhara ya watu kujeruhiwa pamoja na vifo.