Na Boniphace Mwabukusi, Jamhuri Media, Dar es Salaam

Si halali kwa kampuni ya kukopesha au benki kumkejeli au kumtangaza vibaya mteja aliyeshindwa kulipa rejesho kwa ukamilifu.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mteja ana haki ya faragha na heshima yake inapaswa kulindwa hata anaposhindwa kulipa mkopo.

Sheria mbalimbali zinazoweza kutumika kulinda haki zao:

1. Sheria ya Miamala ya Kibenki na Taasisi za Fedha, 2006. Inahakikisha kwamba taasisi za fedha zinazingatia maadili ya kibenki, ikiwa ni pamoja na usiri wa taarifa za wateja.

2. Sheria ya Huduma za Malipo ya Kielektroniki, 2015. Inadhibiti jinsi taasisi zinavyoshughulikia taarifa za wateja, ikiweka masharti ya usiri na matumizi sahihi ya taarifa hizo.

3. Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, 2015

Iwapo kampuni ya mkopo au benki itamkashifu mteja kwa kutumia mitandao ya kijamii au njia za kidigitali, inaweza kuwajibika kisheria kwa kosa la kashfa au uchochezi mtandaoni.

4. Muongozo wa BOT wa Septemba, 2024.

Muongozo huu unawataka watoaji wa huduma za mikopo kidigitali kuzingatia sheria, kanuni na masharti yaliyowekwa ya utoaji wa huduma za kifedha Tanzania.

Muongozo huu una lengo la kulinda haki, faragha na hadhi za wateja wanaofikia na kutumia huduma hizi.

Hivyo kwa mukhtadha wa muongozo huu ni katazo dhidi ya lugha za dhihaka na matusi, kutoa taarifa za siri za wateja mitandaoni, kutumia ujumbe watu wasio husika mitandaoni kwa watu ambao si sehemu au wahusika wa mkopo husika.

Nini cha kufanya ukikashifiwa au kudhalilishwa?

1. Toa malalamiko rasmi

Muone wakili aliye karibu na wewe ili akusaidie kuwaandikia taasisi husika kutaka watii matakwa ya kisheria wa kusafishe kwa kutoa maelezo ya kufuta tangazo lao na kusisitiza haki yako ya faragha.

2. Ripoti BoT

Ikiwa jambo hili limefanywa na benki au taasisi ya fedha iliyoidhinishwa kisheria, unaweza kulalamika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ina mamlaka na inaweza kuchukua hatua za kinidhamu.

3. Tumia Sheria ya Makosa ya Mtandao

Ikiwa umegundua taarifa zako zinatumika vibaya mitandaoni, toa ripoti kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) au vyombo vya usalama vinavyoweza kuchukua hatua za kijinai na kimadai kuhakikisha kuwa wahalifu au wakiukaji hawa wa sheria wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

4.  Fungua Kesi ya Madai ya Kashfa (TORT OF DEFAMATION)

Unapokwaza na jambo la namna hii, muone wakili aliye karibu nawe ili apitie lalamiko lako na kuona namna tangazo au jambo unalo lililamikia lilivyo andikwa.

Baada ya kujiridhisha kuwa kuna ukiukwaji wa sheria na kwamba unastahili kudai na kulipwa fidia, wakili atakuongoza katika hatua za kisheria kudai fidia mahakamani ikiwa umeharibiwa sifa au kushushwa hadhi kutokana na kitendo hicho.

Mfano mzuri ni katika Kesi ya Grace Ndeana  dhidi ya Benki ya NBC ambapo mdaiwa alikopa fedha lakini alishindwa kufanya marejesho.

Mdai kwa kuzingatia masharti ya ukopaji akateua dalali kwa ajili ya kutimiza haki yake ya kimkataba ya kuuza nyumba ya mdaiwa na kinyume na sheria na masharti ya ukopaji alianza kuzunguka mitaa ya Mji wa Singida akitumia maneno ya kejeli yafuatayo dhidi ya mkopaji wakati wa akitangaza mnada wao: “Kukopa harusi, kulipa matanga.”

Mahakama iliamuru Grace ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi alipwe kiasi cha Sh milioni 50 kama fidia ya kuchafuliwa jina lake.

Muhimu; sheria haikatazi kabisa mdai kutangaza mnada kama haki yake ya kutimiliza masharti ya mkataba wa mkopo. Hivyo anaweza kutangaza kwamba atauza nyumba fulani kwa mnada wa benki.

Kinachokatazwa ni yale maneno ambayo kwa mazingira yake yanakuwa nje ya suala husika na kulenga kumshambulia au kumdhalilisha mkopaji aliyeshindwa kufanya marekebisho.

Hivyo itakuwa jukumu la mkopaji aliyeshindwa kulipa kuthibitisha kwa vigezo kwamba maneno yaliyo tamkwa ni ya kudhalilisha na hayahusiani na suala la mkopo au marejesho.

Mwandishi wa makala hii ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)