Marijani Rajabu kweli hatunaye tena hapa duniani, lakini kamwe wadau na wapenzi wa muziki wa dansi hapa nchini hawatamsahau.

Alikuwa miongoni mwa wanamuziki waliotoa mchango mkubwa wa maendeleo ya nchi kupitia tungo za nyimbo zake maridhawa, zilizokuwa zikiendana na wakati.

Machi 23, 2014 Marijani alitimiza miaka 18 tangu atangulie mbele ya haki. Nguli huyo alifariki Machi 23, 1995 na kuzikwa siku iliyofuata katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Marijani alizaliwa Machi 3, 1955,  Kariakoo, Dar es Salaam. Kwa mapenzi yake Mungu, akamchukua akiwa na umri wa miaka 40.

Alikuwa akitunga na kuimba nyimbo zilizokuwa zimejaa maudhui mema kwa jamii, ikizingatiwa kwamba takriban nyimbo zake zote zilikuwa ni visa vya kweli.

Nguli huyo alikuwa ni mithili ya ‘mtambo’ wa kurekebisha tabia ya mtu yeyote aliyefanya mambo kinyume cha maadili pasipo kujali cheo, urafiki, udugu hata ukaribu.

Ubora wa mashairi katika nyimbo hizo ni kati ya sababu za kuendelea kupendwa na wapenzi wa muziki hapa nchini hadi kufikia kuitwa ‘Jabali la Muziki’. Kila kumbi za starehe utakazoingia hapa nchini, nyimbo zake hazikosi kusikika zikirindima. Hali kadhalika bendi zetu za muziki wa dansi zilizosalia nazo haziwezi kumaliza onesho pasipo kupiga angalau wimbo mmoja wa nguli huyo.

Wasifu wa Marijan Rajabu unaeleza kwamba mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji.

Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa akipenda sana uimbaji wa Paschal Rochereau Tabu Ley, mwimbaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na mwimbaji kutoka nchini Guinea, Sorry Kandia. Pia alikuwa akicheza mpira wa miguu.

Alilelewa katika misingi ya dini ya Kiislamu, kwa hivyo alihudhuria mafunzo ya dini tangu alipokuwa mtoto.

Alipokaribia umri wa miaka 18, nuru yake katika muziki ilianza kung’ara. Baadaye alijiunga na Bendi ya STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo, Raphael Sabuni. Kabla ya hapo,  bendi hiyo ilikuwa unajulikana kama The Jets.

Akiwa katika bendi hiyo, Marijani alitoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza alipokwenda Nairobi, Kenya. Katika safari hiyo aliambatana na bendi hiyo ya STC kwa madhumuni ya kwenda kurekodi nyimbo zilizotoka katika nembo ya Phillips.

Akiwa na bendi hiyo, uongozi wa Shule ya Sekondari ya Tambaza alikokuwa akisoma, ulipeleka malalamiko kwa uongozi wa STC iliyokuwa ikimiliki bendi hiyo, kwa kumshirikisha Marijani katika muziki akiwa bado mwanafunzi, jambo lililofanya STC kumwengua.

Mwaka 1972 Marijani alihamia Bendi ya Safari Trippers iliyokuwa inaundwa na vijana wenzake na haikuwa ikimilikiwa na chombo cha umma.

Marijani alionekana kwamba alikuwa ‘amebanwa’ huko STC katika fursa ya kung’ara katika uimbaji, hivyo ubora wake ulifunguka hasa na kuweza kuinyanyua Safari Trippers kuwa moja ya bendi maarufu hapa nchini.

Aliwakuta vijana wenzake akina David Mussa, aliyekuwa akipiga gitaa la solo na kuimba. David hivi sasa ni mlokole ameachana na mambo ya muziki, anaishi karibu na Klabu ya TTC Chang’ombe.

Wengine walikuwa Ali Rajabu (mwimbaji), Christian Kazinduki aliyekuwa akiliungurumisha gitaa zito la besi, Joseph Bernard kwa upande wa midomo ya bata (saxophone) na Jeff, ambao hadi sasa wanapiga katika Bendi ya Mlimani Park waliojiunga nayo mwaka 1978.

Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo pia walizunguka nchi nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Matilda, Baba Nyerere mlezi, Mkuki moyoni, Kumekucha, ambao ulipendwa na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kufanywa kuwa kiamsho (signature tune) cha kipindi cha ‘Kumekucha’ kilichokuwa kikirushwa kila alfajiri.

Safari Trippers iliyokuwa katika ushindani na bendi nyingine za vijana na hasa Afro 70, iliuza zaidi ya nakala 10,000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kununua vyombo vyake vizuri aina ya Rangers, vilivyokuwa maarufu wakati huo, ikiwa na makao yake makuu eneo la Chang’ombe Uhindini, Temeke, Dar es Salaam.

‘Jabali la Muziki’ Marijani pia alihusudu kwa kiasi kikubwa uimbaji wa aliyekuwa kiongozi wa Empire Bakuba, Kabasele Yampanya ‘Pepe Kale’. Hata baadhi ya nyimbo zake zilizokuwa akizighani zilishabihiana na ladha ya uimbaji wa Pepe Kale.

Msemo wa la kuvunda halina ubani ulijionesha pale maelewano yalipokuwa mabaya kati ya wanahisa wanne wa bendi hiyo, na kusababisha kusambaratika licha ya bendi hiyo kuwa juu kimuziki wakati huo.

Marijani akiambatana na wenzake Kazinduki, ‘Pacha’ wake katika kuimba hata kushabihiana majina, Ally Rajabu, Benard na Jeff wakajiunga na bendi mpya ya Dar International iliyokuwa ikiongozwa na mpigaji solo Abel Baltazar aliyeambatana na gwiji mwingine Muhidin Maalim Gurumo.

Wakiungana na wanamuziki wengine mahiri, walishikamana kuunda kikosi ‘moto’ ambacho baada ya kupakua ‘vibao’ vyake vya kwanza kikiwamo cha Margaret, walitikisa anga ya muziki hapa nchini.

Katika bendi hiyo ya Dar International waliwakuta wanamuziki wazuri nao wakaongeza nguvu na kuifanya bendi hiyo kupata umaarufu wa hali ya juu. Vibao vyao vya Zuwena na Mwanameka vilitamba katika vipindi kadhaa vya salamu vya Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) wakati huo.

Wakati ule bendi ilirekodi vibao vyake Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kuambulia Sh 2,500. Yaelezwa kwamba nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa Kampuni ya PolyGram bila ya ridhaa yao.

Kati ya mwaka 1979 na 1986 bendi ilipita kupiga muziki karibu kila wilaya hapa nchini, kwa minajili ya kutoa elimu sanjari na kuwaburudisha wananchi wakipiga katika mtindo wao wa Super Bomboka.

Mara nyingi ilipokuwa hapa Dar es Salaam kama ilivyokuwa Safari Trippers, makao yake makuu yalikuwa katika Hoteli ya Princess Mnazi Mmoja, Super Bomboka lilisakatwa kila wiki katika ukumbi wa Super Fanaka Buguruni.

Mbio za  sakafuni huishia ukingoni. Uchakavu wa vyombo hatimaye mwaka huo 1986 ukamaliza mbio ndefu za bendi hiyo.

Marijani alikuwa mmoja wa wanamuziki 57 waliounda kundi la wasanii lililojulikana kama Tanzania All Stars mwaka 1987.

Kundi hilo lilitia fora kwa wimbo wake wa Fagio la Chuma. Wimbo huo ulikuwa ni kuitikia kaulimbiu ya Rais wa Awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, juu ya uwajibikaji.

Kundi hilo lilirekodi vibao vingine vinne ambavyo si rahisi kwa bendi zilizopo sasa kufikia ubora wake kimuziki.

Kuna wakati Dar International ilisimama kimuziki. Marijani alishiriki kupiga muziki katika Bendi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya Mwenge Jazz alikopiga muziki kwa muda mfupi.

Marijani alipiga hodi jijini Arusha na kujiunga na Bendi ya Kurugenzi Jazz. Huko alidumu kwa mwaka mmoja na kurejea Dar es Salaam.

Mfanyabiashara wa jijini Dar es Saam aliyejulikana kwa jina Roger Malila, alimchukua Marijani kwa ajili ya kuanzisha Bendi ya Orchestra Bene Bene. Bendi hiyo wakati huo ilitamba na mtindo wake wa ‘Mahepe’ mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Kwa mara nyingine tena bahati haikuwa upande wake, kwani bendi hiyo haikudumu kwa kipindi kirefu kutokana na ukosefu wa vyombo vya muziki.  Hatimaye mambo yakaenda kombo tofauti na walivyotarajia.

Baada kuhangaika kwa muda mrefu huku na kule, Marijani aliamua kuanzisha kundi lake la muziki lililoitwa Africulture. Lakini nalo halikudumu na kufa ‘kifo cha mende.’

Maisha ya mwanadamu ni kitendawili kilichojaa majaribu mengi. Inasemekana kuwa kufikia mwaka 1992, hali ya maisha ya Marijani ilikuwa ngumu kupita kiasi. Alifikia kuendesha maisha yake kwa kuuza kanda za nyimbo zake. Alijenga kibanda nje ya nyumba yao maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Pamoja na kuimba nyimbo nyingi za kukisifu Chama Cha Mpinduzi (CCM) na Serikali, na hata tungo yake Mwanameka kutumiwa katika mtihani wa kidato cha nne, hakuwahi kuenziwa.

Ndipo Septemba 9, 2012 Rais Jakaya Kikwete alipomtunukia Tuzo ya Heshima ya Muungano katika maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Wasanii wengine waliotunukiwa siku hiyo ni pamoja na kiongozi wa zamani wa Msondo Ngoma, Muhidin Maalim Gurumo, mwimbaji mkongwe wa taarab, Fatuma Bint Baraka (Bi Kidude), msanii wa maigizo ya filamu, Fundi Said ‘Mzee Kipara’ na mwanariadha mkongwe John Steven Akwari.

Hapana shaka utakuwa unazikumbuka nyimbo za nguli huyu alizotunga na nyingine kushiriki kikamilifu kuimba kama vile Masudi, Habari yako, Sauti yako nyororo, Baba Anna, Kitinda mimba, Salama nakuita, Namsaka mbaya wangu, Zuwena na Ndoa ya mateso.

Marijani Rajabu hakuishia hapo kwani alitoka na nyimbo nyingine za Tabu ni hali ya dunia,  Mama Watoto, Tamaa mbele na Baba watoto, ambazo ziligusa hisia za  wapenzi wa muziki na wale wa kawaida waliokuwa wakizisikia redioni.

Wimbo wa Uke wenza una mambo ulifanya ndoa nyingi za mitala zilijirekebishe kitabia na wimbo wa Georgina ulikuwa wimbo uliotia fora miongoni mwa nyimbo bora hapa nchini.

Mtunzi wa wimbo huo wa Georgina alikuwa wanamuziki mkung’utaji gitaa la rhythm mahiri nchini, Jumanne Uvuruge, ukaimbwa kwa umahiri mkubwa kwa sauti yenye hisia kali na Marijani Rajabu.

Marijani alithubutu kukemea tabia mbovu ya ndugu yake wa karibu kupitia wimbo wa Chakubanga. Huo ulikuwa ni kisa cha kweli ambacho ndugu yake huyo baada ya kutoka Ulaya, akajiita John Smith badala ya jina lake halisi la Chakubanga.

Kupata ladha halisi ya wimbo huo, sehemu fupi ya ghani zake katika kibao cha Chakubanga ni kama ifuatavyo:

“Leo kijana ninasema eeh, Hayo mambo yako unayofanya eeh, Mwisho wake bwana, mambo yatakuwa mabaya, Wala usidangayike na cheo ulichopata, Kudharau wazazi kuhadaika na dunia, Mwana vibaya eeh, vibaya mwana vibayaa.

“Fikiri kwanza ulikotoka, usijifanye huna baba wala mama waliokulea, kwa taabu nyingi na mashaka, wakakusomesha ukahitimu mafunzo, mbona unawanyanyasa na matusi kuwatukana, mwana vibaya, vibaya mwana vibayaa. Mambo ya ajabu uliyofanya eeh, ulipochaguliwa kwenda ng’ambo uliporudu bwana, na jina umebadilisha, jina lako Chakubanga, unajiita John Smith, na mwendo umebadili bega moja umelishusha…

Nyimbo za nguli huyu zitaendelea kusikika vizazi na vizazi kwa kuwa zimebeba ujumbe mzito kwa jamii yoyote ile.

Je, tunamuenzije Marijani Rajabu? Ushauri wangu kwa vijana wa muziki wa kizazi kipya ni kuwa wafuate na kuyaendeleza yote mazuri ya watangulizi wao kama akina Marijani, Gurumo, Mbaraka Mwinshehe na wengine wengi.

Mungu aiweke roho yake Pahala Pema Peponi, Amina.

 

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba 0874 331200, 0767 331200 na 0713 331200.