Rais John Magufuli amejipambanua kama kiongozi mpenda wanyonge. Mara zote amesikika na hata ameonekana akiwatetea watu wa kada hiyo ambao kwa muda mrefu wametaabika. Hili ni jambo jema linalostahili kutendwa na kiongozi mkuu wa nchi.

Katika kutekeleza dhana hiyo ya kuwa “Rais wa Wanyonge”, amehakikisha kodi nyingi zilizokuwa kero kwao zinaondoshwa.

Akaona hiyo haitoshi. Akaandaa vitambulisho vya wachuuzi kwa kuwatoza Sh 20,000 pekee kwa mwaka. Sambamba na kutoa vitambulisho hivyo, akawazuia viongozi na watumishi wa mamlaka mbalimbali kuwabughudhi popote walipo ili waendeshe uchuuzi wao kwa raha mustarehe. Jambo hili likapokewa kwa shangwe na nderemo kila mahali nchini. Lakini baadaye kukaonekana kuwapo ugumu wa kugawa vitambulisho hivyo, na ndipo tulipoanza kuona na kusikia mikwara ya baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa. Ikatolewa ilani kuwa yeyote atakayekaidi kulipa fedha ili apewe kitambulisho atakuwa amejiweka katika mazingira magumu na hata kuadhibiwa.

Ukitazama nia ya Rais Magufuli kwenye mpango huu ni njema kabisa. Analenga kuona kila mtu mwenye uwezo wa kujibidisha, anafanya hivyo na kujipatia kipato halali.

Sina shaka hata kidogo kwamba rais wa nchi ndiye kiongozi pekee anayepokea taarifa nyingi zinazoihusu jamii na nchi kwa ujumla wake. Hakuna taarifa anayoweza kuitaka akanyimwa. Tofauti ni moja tu kwamba kwenye taarifa anazopewa kunaweza kuwamo chache au nyingi zisizo sahihi, kwa hiyo hoja hapa ni ukweli au uhalali wa hizo taarifa anazozipata.

Kwa hili la wamachinga nadhani kulihitajika utafiti wa kina kabla ya kulianzisha. Pamoja na nderemo za kufaidi walizonazo wachuuzi hawa, zipo athari zilizoletwa na mpango huu. Jambo lolote linakuwa lenye tija endapo tu upande wa faida unauzidi upande wa hasara.

Kwenye hili la wamachinga, naamini watendaji waliokula viapo vya uadilifu na kusema ukweli daima watamweleza rais kuwa tunapaswa kurekebisha dosari zilizokwisha kujitokeza. Haya yanapaswa yafanywe mapema kabla hayajakomaa, ingawa kwa hali ya mwaka huu na mwaka kesho sidhani kama hilo litawezekana.

Bahati mbaya wapo baadhi ya watendaji ambao ni waoga na wengine kwa kukwepa lawama wameamini katika kuremba au kusifu. Tabia hiyo haiwezi kumsaidia rais au nchi yetu. Wamejipa hofu kwamba kumpa rais mawazo mbadala ni kujihalalishia njia ya kutumbuliwa.

Wanaona baadhi ya mambo yanahitaji kurekebishwa, lakini kwa hofu tu waliyojipa mioyoni na katika akili zao wameamua kuimba mapambio ya sifa wakitaka kuuaminisha uongozi wa juu kuwa kila kitu kinakwenda sawa. Lakini ni hawa hawa ambao siku mambo yakiharibika watakuwa wa kwanza kusema “tulijua”.

Nimebahatika kumfahamu kwa kiasi kidogo Rais Magufuli, na nikiri kuwa kwa muda wote huo sikupata kumweka kwenye kundi la viongozi wasiopenda kusikia wasiyoyapenda. Ni kiongozi anayetoa mwanya wa kupokea maoni na ushauri, lakini msimamo wake umekuwa si wa kubadilika kwa lile analojua lina masilahi kwa jamii na taifa.

Ndiyo maana nasema kwa hili la wamachinga inawezekana akiupata kweli na hali halisi ya matokeo ya vitambulisho huku mitaani, huko tuendako kuna mabadiliko atayafanya. Wajibu wa wasaidizi wake ni kumpa “black and white” ya kinachoendelea mitaani. Wasihariri taarifa wanazomfikishia.

Vitambulisho vya wamachinga vimekuwa na faida na hatari zake. Jambo la kwanza kubwa linaloonekana ni ongezeko kubwa mno la vijana katika miji, manispaa na majiji yote nchini. Pia kuna ongezeko kubwa la wageni waliotumia fursa hiyo kujinufaisha. Hivi karibuni pale Mwenge, Dar es Salaam nimewaona wamachinga kutoka Zimbabwe wenye vitambulisho vya wamachinga. Ndiyo, huu ni utandawazi lakini pamoja na ukweli huo tunapaswa kutazama namna milango yetu ilivyo wazi.

Vijana wengi wamekimbilia mijini kwa sababu ndiko kwenye biashara na kama wamesikia “leseni ya biashara kwa mwaka” inapatikana kwa Sh 20,000 hakuna wa kuwazuia kwenda mijini. Hili ni kama la Ngorongoro ambako baada ya kutolewa chakula cha bure ndugu zetu wengi wa jamii ya wafugaji wamekwenda kuishi eneo la hifadhi ili wafaidi huduma za bure. Nia ilikuwa nzuri, lakini matokeo yamekuwa mabaya. Hatua zisizopochukuliwa Ngorongoro [hifadhi] ina miaka michache ya kuwapo.

Hakuna sheria ya kibaguzi ya kumzuia kijana au mtu mzima kwenda anakotaka. Hoja iliyopo hapa ni je, miji, manispaa na majiji yetu wamejiandaa vipi kwa miundombinu kuhimili ujio huu wa maelfu ya vijana wanaotoka vijijini?

Tukumbuke kuwa wamachinga hawa wanahitaji matibabu. Je, kuna zahanati, vituo vya afya, hospitali, dawa na vitendea kazi vya kutosha? Watazaa watoto watakaohitaji kwenda shule, tena elimu bure! Je, kuna mpango wa kupanua huduma za elimu, vifaa, walimu na miundombinu ya elimu?

Uzalishaji taka zinazotokana na biashara zao unaongezeka mno. Je, wazoa taka wamejipanga kuongeza vitendea kazi na watoa huduma za usafi? Palipo na wengi kuna mengi – wingi wao unaweza kuongeza matukio ya uhalifu. Je, vyombo vya usalama vimejipanga vipi kuikabili hali hiyo? Miundombinu ya majisafi na majitaka imezingatiwa? Usafiri wa umma umeandaliwa au ndiyo huu wa mwendokasi uliokwishalemewa? Maswali ni mengi.

Pili, vitambulisho vimefifisha mapato ya halmashauri za miji, manispaa na majiji. Tunaona maduka mengi, ama yamefungwa, au yamebadilishwa maghala ya kuhifadhia bidhaa. Waliofunga maduka wamefungua mikeka na matoroli ya kuuzia bidhaa. Wenye maduka wameajiri wamachinga. Wanagawana kulingana na bidhaa zilizouzwa. Wamefanya hivyo ili kukwepa kodi na ushuru.

Migahawa mingi imefungwa, si kwa sababu watu hawali vyakula, la hasha! Waendesha migahawa wameshindwa kukabiliana na ushindani wa kina mama na baba ntilie. Nani anunue chakula mgahawani cha Sh 5,000 ilhali chakula hicho hicho au chenye utamu kuzidi hicho kikiuzwa kwa Sh 1,500?

Sasa vyakula vingi vinapikwa nyumbani kisha vinapakiwa kwenye magari madogo na bajaji tayari kwa kuuzwa mijini. Huko vinakopikwa ni Mungu tu anajua mazingira yake. Tunaongeza bajeti ya afya na wakati huo huo tunaruhusu magonjwa yaenee. Hawa hawalipi ushuru wowote kwa miji, manispaa au majiji.

Hatua hii imezifanya mamlaka hizo ziwe hoi bin taabani kifedha. Juzi, Jiji la Tanga limetangaza hali mbaya kimapato. Wanasema tangu kuanza kwa vitambulisho hivi wamepoteza Sh milioni 700 na hadi ninavyoandika huenda kiasi kikazidi Sh bilioni 1. Wanashindwa kutekeleza baadhi ya kazi na miradi.

Hali hii ya Tanga iko katika miji, manispaa na majiji nchini kote. Si jambo la kificho. Wanaumia kimya kimya kwa woga tu uliowajaa japo wataumbuka kwenye namba za mapato yao.

Tatu, hali ya ustaarabu mitaani imekuwa mbaya. Barabara na njia za waenda kwa miguu zimevamiwa na kupangwa bidhaa. Hakuna wa kulisemea hili maana wote wamepigwa ganzi kwa hofu ya kupoteza kazi. Sidhani kama agizo la rais lilikuwa njia hizi za waenda kwa miguu zivamiwe na wachuuzi. Rais hakuagiza hicho kitu.

Natoa mapendekezo machache. Mamlaka zinazohusika ziende Cairo, Misri zijifunze namna wamachinga walivyoandaliwa mazingira ya biashara zao. Nilikwenda nikaona. Tuna mengi mazuri ya kujifunza Cairo kwa upande huu wa wamachinga.

Serikali itenge fedha za kununua maeneo ya kibiashara na ishirikiane na sekta binafsi wajenge maghorofa mengi katika kila panapoonekana kuwafaa wamachinga. Majengo yawe ya viwango vizuri kwa nchi nzima tofauti kabisa na yale yaliyojengwa Ilala, Dar es Salaam.

Mpango huu unaweza kuanza kutekelezwa mwaka 2021 au hata 2022. Kadi walizonazo wamachinga zihakikiwe ili ijulikane kwa dhati kuwa wanaozimiliki ni wamachinga kweli. Mamlaka zihakikishe kila mmachinga anaponunua bidhaa za jumla anatunza stakabadhi; na hiyo itasaidia kuwatambua waliolipa kodi ya matumizi. Kwa njia hiyo serikali itakusanya VAT ya kutosha na kwa kiwango cha kustaajabisha. Hakutakuwa na haja ya kukimbizana na wamachinga.

Kama nilivyosema awali, nia ya Rais Magufuli kwenye uamuzi huu ni nzuri. Inalenga kuwaona Watanzania hawa wakipata fursa ya kujiingizia kipato. Kwa kuwa kumeonekana kuwapo kasoro za hapa na pale, matarajio ya wengi ni kuona kasoro hizo zikipatiwa ufumbuzi ili kuifanya dhana hii ya vitambulisho kuwa yenye tija. Tukiacha hali hii iendelee hivi ilivyo sasa madhara yake kijamii na kiuchumi kwa nchi yatakuwa makubwa.

Viongozi wa miji, manispaa na majiji waketi pamoja waje na mapendekezo mujarabu ya namna ya kuboresha huduma hii ya vitambulisho vya wamachinga ili iwe na tija kwa nchi. Najua wanaumia, lakini wameamua kufa kimoyo moyo kwa sababu ya woga tu wa kufikirika kwamba wakisema watatumbuliwa. Rais asihukumiwe kwa hisia. Aelezwe hali halisi ya mapato ilivyo.