Rais wa Marekani, Donald Trump amesema Marekani “itaachana” na kujiondoa kwenye mazungumzo upatanishi kati ya Urusi na Ukraine ikiwa Moscow au Kyiv “itayafanya kuwa ngumu zaidi” kufikia makubaliano ya amani.

Rais huyo wa Marekani aliwaambia waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval siku ya Ijumaa kwamba hakutarajia usitishaji mapigano utokee katika “idadi maalum ya siku” lakini alitaka ifanyike “haraka”.

Kauli yake ilikuja saa chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kuonya kwamba Marekani ingeachana na mazungumzo hayo isipokuwa kama kuna na dalili wazi za maendeleo ndani ya siku chache.

“Hatutaendelea na juhudi hii kwa wiki na miezi mingi,” Rubio alisema, akiongeza kuwa Marekani ina “vipaumbele vingine vya kuzingatia”.

Hii inakuja wakati mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine yanaendelea, na watu wawili wakiripotiwa kuuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika miji ya kaskazini-mashariki ya Kharkiv na Sumy siku ya Ijumaa.

Moscow ilianzisha uvamizi kamili wa Ukraine mnamo 2022, na wanajeshi wa Urusi wamekuwa wakisonga mbele – ingawa polepole – katika maeneo ya Ukraine ya mashariki.

Rais Vladimir Putin ameweka masharti kadhaa juu ya usitishaji mapigano wowote unaowezekana. Alipoulizwa kuhusu makubaliano kati ya Urusi na Ukraine, Trump alisema: “Tunazungumza hapa kuhusu watu wanaokufa. Tutaifanya (vita) isimame, ikiwezekana.

“Sasa ikiwa, kwa sababu fulani, moja ya pande hizo mbili itafanya iwe vigumu, tutasema tu, ‘Nyinyi ni wapumbavu, nyinyi ni wajinga, nyinyi ni watu wabaya,’ na tutajiondoa tu.”