Vikosi vya Marekani vimefanya mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa yanayotajwa kuwa ngome za kundi linalojiita dola la Kiislamu ISIS nchini Syria, kulingana na Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani kupitia mtandao wa X.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa mashambulizi hayo mfululizo yalilenga kuvuruga uwezo wa kundi hilo katika mipango yake ya kuishambulia Marekani na washirika wake kwenye eneo hilo na kwingineko.

Jeshi la Marekani lina takriban wanajeshi 900 Syria ambao ni sehemu ya muungano wa kimataifa unaopambana dhidi ya kundi hilo. Muungano huo ulianzishwa mwaka 2014 ili kusaidia kupambana na kundi hilo lenye silaha, ambalo limeteka maeneo mengi ya Iraq na Syria.

Mwezi Septemba, vikosi vya Marekani vilifanya mashambulizi mawili tofauti nchini Syria, na kuwauwa “magaidi” 37 wakiwemo wanachama wa IS na wanachama wa kundi lenye ushirika na Al-Qaeda la Hurras al-Din.

Hata hivyo, Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani imesema tathmini ya uharibifu kutokana na mashambulizi hayo bado inaendelea na hakuna ishara yoyote ya kuwepo kwa raia waliojeruhiwa.