Marekani imemfukuza balozi wa Afrika Kusini Ebrahim Rasool. Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio amesema balozi huyo ni mwanasiasa mbabe, haipendi Marekani na anamchukia Rais Donald Trump.

Uhusano kati ya Marekani na Afrika Kusini umekuwa ukizorota tangu Trump alipokata misaada ya kifedha ya Marekani kwa nchi hiyo, akitoa mfano wa kutoidhinishwa na sera ya Afrika Kusini ya ardhi na hatua ya nchi hiyo ya kupeleka kesi kuhusu mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya Israel ambayo ni mshirika wa Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio pia alikataa kuhudhuria mkutano wa G20 wa mawaziri wa mambo ya nje uliofanyika mjini Johannesburg mnamo mwezi Februari, akidai kuwa Afrika Kusini inaendelea kufanya mambo mabaya.

Ofisi ya Rais Cyril Ramaphosa imesema uamuzi wa Marekani wa kumfukuza balozi wake ni wa kufadhaisha na imetoa wito wa kufuata taratibu za kidiplomasia katika kulishughulikia suala hilo. Taarifa hiyo imeeleza kuwa Afrika kusini itaendelea na nia yake ya kujenga uhusiano wenye manufaa na Marekani.

ufukuzwa kwa Rasool aliyewahi kuwa mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi, kumezidisha mvutano unaozidi kushika kasi kati ya nchi hizo mbili.

Juma lililopita Rais wa Marekani Donald Trump alizidi kuupa sura mpya mvutano huo kwa kusema kuwa wakulima wa Afrika Kusini wanakaribishwa Marekani baada ya kurudia madai kuwa serikali ya Afrika Kusini inawanyang’anya ardhi wakulima weupe. Trump ameyasema hayo bila kutoa ushahidi.

Bilionea mzaliwa wa Afrika Kusini Elon Musk, ambaye ni mshirika wa karibu wa Trump, amesema wazungu wa Afrika Kusini wamekuwa wahanga wa “sheria za umiliki wa kibaguzi.”

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alitia saini na kuwa sheria muswada mnamo mwezi Januari. Mswaada huo ni unalenga kuirahisisha serikali kuichukua ardhi kwa maslahi ya umma, na katika baadhi ya hatua bila ya mmiliki wa ardhi husika kupewa fidia.

Ramaphosa ametetea sera hiyo na amesema serikali yake haipangi kumnyang’anya ardhi yoyote bali sera hiyo inalenga kuondoa tofauti za umiliki wa ardhi kati ya Waafrika Kusini Weupe na Weusi walio wengi.

Amesema hakuna ardhi iliyochukuliwa na hivyo ukosoaji wa Marekani unaendeshwa na taarifa potofu. Ramaphosa amesema suala la ardhi nchini Afrika Kusini ni la kuhuzunisha sana ikizingatiwa kuwa zaidi ya miaka 30 baada ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi wa utawala wa wazungu wachache, bado asilimia 7 pekee ya wazungu ndio wanamiliki sehemu kubwa ya ardhi nzuri ya kilimo cha biashara nchini Afrika Kusini.

Matamshi makali ya utawala wa Trump kwa serikali ya Afrika Kusini yanahusu kuwatetea Waafrika Kusini weupe ambao ni wana nasaba ya Uholanzi na wengine ni wazawa wa walowezi kutoka kwenye nchi zingine za Ulaya na pia yanatokana na madai ya awali yaliyotolewa na mshauri wa Trump mzaliwa wa Afrika Kusini Elon Musk na baadhi ya wafafanuzi wa kihafidhina wa Marekani kwamba serikali ya Afrika Kusini inaruhusu mashambulizi dhidi ya wakulima wa kizungu ambayo ni sawa na mauaji ya kimbari.