Marekani imeishutumu Urusi kwa kufadhili pande mbili zinazopigana nchini Sudan, hatua inayoonekana kusisitiza madai ya awali ya Washington kwamba Moscow imekuwa ikichochea kuendelea kwa mgogoro huo.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield, ameishutumu Urusi kwa kusema ilichagua kuweka kizuizi, kusimama peke yake na kuweka raia hatarini:

“Baraza hili lilikutana miezi miwili tu iliyopita kujadili azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano nchini kote, kuongeza ulinzi wa raia na mtiririko wa misaada usiozuiliwa.”

“Wanachama 14 wa baraza waliidhinisha maandishi yaliyotayarishwa na Sierra Leone na Uingereza na bado, Urusi, ilichagua kuweka kizuizi, ikisimama peke yake ilipopiga kura kuwahatarisha raia huku ikifadhili pande zote mbili za mzozo.”

Alipoulizwa kuhusu maelezo zaidi katika madai yake, Balozi Greenfield, alisema Washington inafahamu kuhusu maslahi ya Urusi katika biashara ya dhahabu ya Sudan na inalaani msaada wa aina yeyote kwa pande zinazopigana ima kupitia biashara haramu ya dhahabu au kupeana zana za kijeshi.

Aidha Greenfield ameeleza kwamba wanaamini ushirikiano wa mamlaka ya Sudan katika uchimbaji dhahabu na makampuni yaliyowekewa vikwazo ya Urusi pamoja na watu binafsi wanaweza kuzidisha kwa muda mrefu matarajio ya Wasudan ya kukomesha vita.