RAIS wa Marekani, Donald Trump amesema  simu za mikononi  zilizotengenezwa na China na vifaa vingine vya kielektroniki havitaondolewa kwenye ushuru badala yake vimehamishiwa kwenye fungu tofauti la ushuru.

Masoko ya hisa ya Ulaya yaliimarika kuanzia Jumatatu asubuhi baada ya tangazo rasmi la Ijumaa kwamba baadhi ya bidhaa hizi zingeweza kuepuka ushuru wa hadi asilimia 145%.

China imetoa wito kwa Donald Trump kufuta kabisa utawala wake wa ushuru, na kurejea kwenye njia za  kuheshimiana . Hata hivyo maafisa wa Marekani walisema Jumapili kwamba bidhaa zitakazotozwa ni vimashine vidogo vya kielektroniki, huku Trump akitarajiwa kufichua maelezo zaidi baadaye.

Advertisement

Tishio hili la hivi punde kutoka kwa Trump linajiri siku chache baada ya Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani, kutangaza simu za mikononi na vifaa vya kielektroniki zimeondolewa kwenye orodha ya ushuru wa asilimia 10 uliokuwa ukiathiri nchi nyingi duniani, pamoja na ule wa juu zaidi dhidi ya bidhaa kutoka China.

Ikulu ya White House imesema kuwa inatumia ushuru kama mbinu ya mazungumzo kupata masharti mazuri ya kibiashara kutoka kwa mataifa mengine.

Trump amesema sera yake itarekebisha ukosefu wa haki katika mfumo wa biashara wa kimataifa, pamoja na kurejesha ajira na viwanda nchini Marekani.

Hata hivyo, uingiliaji kati wake umeleta mabadiliko makubwa katika soko la hisa na kuibua hofu ya kupungua kwa biashara ya kimataifa ambayo inaweza kuwa na athari kwenye ajira na uchumi wa mtu binafsi hasa raia wa Marekani.