Viogozi wa Marekani na Urusi waliokutana Jumanne mjini Riyadh, Saudia Arabia wamekubaliana kuanzisha mchakato wa amani katika mzozo wa Ukraine licha ya Kiev na washirika wake wa Ulaya kutoalikwa kwenye mazungumzo hayo.
Maafisa wa ngazi za juu wa Marekani na Urusi walikutana kwa takriban masaa manne katika kasri la Diriyah mjini Riyadh, Saudi Arabia, na wameafikiana kuanzisha juhudi za kuvimaliza vita vya Ukraine kwa kuunda timu ya wapatanishi, lakini wakakubaliana pia kurekebisha mahusiano yao ya kidiplomasia na kiuchumi, katika kile kinachotazamiwa kama mabadiliko makubwa ya kisera kati ya Washington na Moscow tangu Urusi ilipoivamia Ukraine karibu miaka mitatu iliyopita.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu kutoka pande zote mbili, akiwemo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov ambao kwa pamoja wamesema majadiliano hayo ya Riyadh yalikuwa na manufaa makubwa na kuwa ni hatua nzuri ya kwanza.
Wengine waliohudhuria mazungumzo hayo ya ngazi ya juu ni mshauri wa usalama wa taifa wa Trump, Michael Waltz, na mjumbe maalum wa Mashariki ya Kati, Steven Witkoff, huku Urusi ikiwakilishwa pia na mshauri wa mambo ya nje wa Rais Vladimir Putin, Yuri Ushakov.
Hata hivyo, hakuna afisa yeyote wa Ukraine wala wa nchi washirika wa Ulaya aliyeshiriki mazungumzo hayo, jambo lililoibua wasiwasi mkubwa kwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ambaye alitangaza kuwa nchi yake haitakubali matokeo yoyote ya mazungumzo hayo. Zelensky aliahirisha pia ziara yake iliyopangwa kufanyika nchini Saudi Arabia hadi mwezi ujao, akisema hakutaka ihusishwe na mazungumzo ambayo nchi yake haikualikwa.
