Taifa la Marekani limefika mahala sasa linaliamini taifa la Tanzania. Miaka ya 1960 na 1970 kutokana na Vita Baridi kati ya Marekani na Urusi, ilikuwa vigumu kwa Marekani kufanya kazi na Tanzania.
Marekani iliamini kuwa Tanzania ni mshirika mkubwa wa Urusi, na hivyo ilihofu kuwa pengine kushirikiana na Tanzania kungeweza kutelekeza maslahi yao kama taifa.
Msimamo wa Tanzania wa kutofungamana na upande wowote chini ya uongozi shupavu wa Mwalimu Julius Nyerere uliwatia wasiwasi Wamarekani kuwa huenda ni danganya toto. Waliangalia Urusi ilikuwa ikiendesha siasa za Ukomunisti, ambazo kimsingi hazina tofauti kubwa na Ujamaa na Kujitegemea.
Tanzania pia ilithibitika kuwa rafiki wa karibu wa China, chini ya Mwenyekiti wa Chama cha Komunisti cha China, Mao Zedong. Haya na mengine, kama Tanzania kuwa mstari wa mbele kukomboa nchi za Kusini mwa Afrika yaliifanya dunia kuiona Tanzania kama nchi yenye sifa ya pekee.
Mfumo wa uchumi nao uliwachanganya Wamarekani, wakati wao walikuwa wakifuata mfumo wa ubepari (capitalism), sisi tulikuwa tukifuata Ujamaa (socialism). Mfumo wetu wa uchumi ulikuwa hodhi. Serikali ilishiriki kufanya karibu kila biashara ikijumuisha kupanga bei, wakati Marekani ilikuwa na soko huria.
Baada ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliamua kufungua milango kupitia kaulimbiu yake ya ‘Ruksa’. Hapa Mzee Mwinyi alikubali masharti ya Benki ya Dunia chini ya mpango wa kurekebisha uchumi uliojulikana kwa Kimombo kama Structural Adjustment Program (SAPs).
SAPs ilipokuja hapa nchini mwaka 1987, Serikali ililazimishwa kupunguza wafanyakazi, utaratibu wa kuchangia huduma za jamii kama elimu, matibabu, uzoaji taka na nyingine ukaanzishwa. Yaliyokuwa mashirika ya umma yakabinafsishwa kwa watu binafsi. Zaidi ya mashirika ya umma 400 yalibinafsishwa.
Hapa uchumi kidogo ukaanza kutoka mikononi mwa Serikali na kushikiliwa na Watanzania. Zipo taarifa kuwa wageni wengi ndiyo wanaonufaika na ubinafsishaji huu, kwani wenyeji wengi hawakuwa na mitaji hivyo wageni walipokuja nchini wakati wa ubinafsishaji wakapewa mashirika hayo tena kwa bei za kutupa.
Mwalimu Nyerere na John F. Kennedy
Mwaka 1963, Mwalimu Julius Nyerere alipata fursa ya kutembelea Ikulu ya White House ya Marekani, ambapo Rais Kennedy alieleza matarajio makubwa juu ya hatua alizokuwa anachukua Mwalimu Nyerere kujenga uchumi wa Tanganyika. Kennedy alichukuliwa na Wamarekani wahafidhina kuwa alitaka kubadili mfumo wa ubepari na kuingiza Ujamaa Marekani. Kutokana na hisia hizo, inaelezwa kuwa Kennedy aliuawa kuepusha mfumo wa ubepari kuanguka.
Ikumbukwe Kennedy aliuawa ikiwa ni miezi minne tangu Mwalimu Nyerere ametoka Ikulu ya Marekani wakiwa wamewekeana mipango lukuki ya kulisaidia Taifa la Tanganyika nao kukua kiuchumi. Marais waliofuatia hawakutaka kujihusisha zaidi na Tanganyika au Tanzania kwa maelezo kuwa ilikuwa inafuata mfumo wa Ujamaa unaopingana na ubepari.
Mwishoni mwa miaka ya 1990 Rais mstaafu wa Marekani, Jimmy Carter, alikuja Tanzania na kutembelea mbuga mbalimbali za wanyama katika ziara binafsi. Kabla ya hapo kiongozi wa juu wa kuja Tanzania alikuwa ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Henry Kissinger, miaka ya 1976, ambaye alijaribu kumshawishi Mwalimu Nyerere kuachana na Ujamaa ikashindikana.
Kulipuliwa Ubalozi wa Marekani
Mambo yaliendelea hadi Agosti 7, 1998 ambapo Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulilipuliwa na watu 11 kupoteza maisha. Kenya nako siku hiyo hiyo Ubalozi wa Marekani ulilipuliwa na wakafa watu zaidi ya 250. Tangu tarehe hiyo ndipo milango ya Marekani ilifunguka kwa Tanzania.
Nakumbuka mashushu wa FBI walipokuja nchini na kuruhusiwa kuingia katika vitengo nyeti vya ulinzi, malalamiko yalikuwa makubwa kwa wananchi wa kawaida na watu wa kada mbalimbali. Wakasema Serikali ya Rais Benjamin Mkapa ilikuwa imefungua mno milango na kwa haraka kwa Wamarekani.
Hofu ya wananchi ilikuwa ni kwamba Marekani wangetumia fursa hiyo kuchunguza na kufahamu siri za taifa. Na kweli wasiwasi huo ulikuwa sahihi. Hapana shaka Wamarekani wakati wanachunguza mlipuko wa bomu, walichunguza na uwezo wetu kujeshi. Si hilo tu, lipo moja lililowavutia Wamarekani.
Serikali ya Tanzania tofuati na Kenya au nchi nyingine zilizopata kukumbwa na milipuko ya aina hiyo, hakushiriki mchezo wa kuwashutumu na kuwalaumu Wamarekani, badala yake ilishiriki kwa vitendo kusaka magaidi, wakatiwa mbaroni na tunakumbuka mmoja Mohamed Ghailani amefungwa maisha huko Marekani.
Ushirikiano iliouonesha Tanzania uliwapa imani Wamarekani. Katika kurejesha wema kwa mara ya kwanza, Rais wa Marekani wa wakati huo, Bill Clinton, alifanya ziara mwaka 2000 na kuja nchini Tanzania akiwa na mkewe. Tunakumbuka alivyokwenda Arusha Rais Clinton akatangaza mji ule kuwa ni ‘Geneva of Africa.’
Baada ya tangazo hilo, idadi ya watalii iliongezeka kutoka 450,000 hadi 750,000. Ushirikiano huo uliendelea hadi mwaka 2008.
Ujio wa George Bush
Rais George W. Bush alikuwa Rais wa Pili wa Marekani kuja Tanzania. Rais huyu alikuja kuidhinisha rasmi mradi wa Millennium Challenge Corperation (MCC), ambao mazungumzo yalikwishafikia hitimisho. Tanzania ilikwishaidhinishiwa na Marekani msaada wa dola milioni 698 sawa na shiling trilioni 1.14.
Fedha hizi zimetumika kujenga na kuchochea ukuaji wa uchumi, kuinua kipato na kuleta maisha bora kwa wananchi katika ujumla wao kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, usafirishaji, nishati na maji. Ni kutokana na lengo hili kuu, miradi mingi chini ya MCC ilijielekeza katika kuchochea maendeleo ya kilimo, ujasiriamali na utalii kwa Tanzania Bara na Visiwani.
Ujenzi wa Barabara
Chini ya mradi wa MCC, barabara zifuatazo zimejengwa au ujenzi unaendelea:- (i) Barabara kutokaTunduma hadi Sumbawanga (Km 224.5), (ii) Barabara ya Tanga-Horohoro (Km 68), ( iii) Barabara ya Tunduru-Songea-Mbamba Bay (Km 407.5) na (iv) Barabara mbalimbali Zanzibar (Km 142.7). Pia ukarabati mkubwa unahusisha Kiwanja cha Ndege Kigoma na Kiwanja cha Ndege Mafia.
Sekta ya Maji
Katika sekta ya maji Mradi wa MCC unafadhili ujenzi wa Bwawa la Kidunda kwa ajili ya kuimarisha huduma ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam, Mradi wa Maji Bukoba Mjini, Mradi wa Mambogo Morogoro, Mradi wa Maji Misungwi, Mradi wa Maji Bunda, Mradi wa Maji Bariadi, Mradi wa Maji Tarime, Mradi wa Maji Geita, Miradi mbalimbali ya Maji Zanzibar (Unguja na Pemba) na Usimamizi wa shughuli za Maji kwenye mamlaka za maji.
Sekta ya Nishati
Mradi wa MCC umeshughulikia uimarishaji wa mtandao wa usambazaji umeme katika mikoa ya Tanga, Mbeya, Mwanza, Iringa, Morogoro, Mtwara na Dodoma. Itakumbukwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Mambo ya Nje, Hilary Clinton, alipoitembelea Tanzania mwaka 2010, alisema Marekani itahakikisha Tanzania inazalisha umeme kwa wastani wa megawati 3,000. MCC mbali na megawati 400 walizotia saini bado unafadhili mpango wa umeme wa Malagarasi Mini-Hydro (Kigoma) na ujenzi wa mkongo wa Taifa kwa Dar es Salaam na Zanzibar.
Ujio wa Rais Barak Obama
Rais Obama aliyewasili nchini jana, amekuja na ndoto moja tu. Anasema Afrika imekuwa gizani kwa muda mrefu. Afrika inafahamika kama Bara Jeusi (Black Continent) si kwa sababu ya rangi ya ngozi za watu wake, bali kutokana na ukweli kwa umeme unaotumiwa na Afrika yote, haufikii hata moja ya nane ya umeme unaotumiwa na Marekani.
Kwa mfano, wakati Tanzania tunatumia umeme wastani wa magawati 675, Marekani wanatumia umeme wastani wa megawati 350,000. Hapa ndipo Obama anaposema Afrika haiwezi kuendelea bila kuwa na umeme wa uhakika.
Sitanii, katika kuhakikisha hilo linawezekana Rais Obama ameamua kutoa msaada wa dola bilioni 7. Mpango huu utawezesha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Ghana, Nigeria na Sudan Kusini. Mpango huu unalenga kupima wazo la Rais Obama iwapo umeme unaweza kuzikomboa nchi za Afrika kiuchumi.
Mawazo yake ni kwamba ukiwapo umeme wa uhakika, basi nchi itaweza kujenga viwanda na hivyo kuzalisha ajira na kukucha uchumi.
Hofu ya madini kuibwa
Sitanii, kimsingi nchi yetu imeingiwa vilivyo na dozi ya Ujamaa na Kujitegemea. Dozi hii imewafanya Watanzania kuwa na mawazo yaliyojifungia. Wakati leo tunaisifia China kwa uchumi unaokua kwa kasi, soko kubwa la bidhaa za China ni Marekani na Ulaya.
Ukiacha suala la soko, wawekezaji wakubwa nchini China ni Wamarekani. Hawa wanazo fedha za kutosha na njia nzuri ya kulisaidia taifa letu ni kuwekeza katika sekta ya umeme, hali itakayozaa viwanda na hivyo kuwa na bidhaa za kuuza sokoni.
Uwekezaji wa aina hii unaiondoa Tanzania katika kundi la kuwa taifa la kupokea misaada bali kufanya biashara. Kwa njia yoyote tunahitaji mitaji kutoka nje ya nchi mitaji hii kwa nchi nyingi duniani inatoka Marekani. Tukizitegemea nchi za Ulaya tutasubiri mno.
Ikumbukwe pamoja na misukosuko yote iliyopo, bado Marekani ndilo taifa lenye uchumi mkubwa kuliko nchi zote duniani. Kwa mantiki hiyo, busara inaonesha kuwa hatua ya Marekani kuifungulia milango Tanzania tunapaswa kuipokea kwa mikono miwili badala ya kuibeza kutokana na tambo za kisiasa.
Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa baada ya Rais Clinton kutoka Tanzania, alimjulisha Rais Bush kuwa Tanzania ni taifa rafiki kwa Marekani, vivyo hivyo Rais Bush wakati anaondoka madarakani, alimwambia Rais Obama kuwa Tanzania ni taifa rafiki kwa Marekani na linayo nafasi ya kuisaidia Marekani kuendeleza amani duniani.
Sababu za Tanzania kukubalika
Sitanii, nimezungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kutoka kufahamu nini kimewavutia marais wa Marekani kuchagua kuja Tanzania mfululizo.
Katika mazungumzo hayo, Membe ameniambia kila mara marais hawa wanaiona Tanzania kama nchi imara katika ukanda huu wa Afrika. Wanakumbuka harakati za ukombozi ilizoziongoza Tanzania ikiwa Mstari wa Mbele kusini mwa Jangwa la Sahara, wanakumbuka msimamo wa Tanzania juu ya suala la Palestina, wanakumbuka msimamo wa wazi wa Tanzania juu ya Polisario nchini Morocco na mingine mengi.
Kikubwa ni utaratibu wa uchaguzi huru na wa haki, ambapo marais wanachaguliwa na kuingia madarakani kwa njia ya sanduku la kura nchini Tanzania. Hii kwa Wamarekani inamaanisha utawala bora. Historia nyingine ni ya Tanzania kusuluhisha nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Ushelisheli, Kenya, Anjuan, Darfur na Lebanon, haya yote yanaiweka Tanzania kwenye chati.
Pamoja na kwamba yapo mtatizo ya hapa na pale, Tanzania ikilinganishwa na nchi zilizoizunguka, vyama vya upinzani vinaweza kutajwa kufanya kazi kwa uhuru tofauti na nchi kama Uganda, ambako wapinzani wa Yoweri Museveni akina Dk. Kiiza Besigye wanaambulia kipigo angalau mara moja kwa wiki.
Hata hivyo, Tanzania nayo inapaswa kuwa makini kwani mwelekeo wa siasa zinazoendelea katika Jiji la Arusha ikiwamo milipuko ya mabomu ikiwa hazitatafutiwa ufumbuzi, basi Tanzania haitakuwa tofauti na nchi nyingine ambazo vurugu ni sehemu ya maisha yao.
Mwisho, ninao wito kwa viongozi wetu. Wito wangu si mwingine, bali ni kuwasihi fursa hizi tunazozipata ziwe zenye manufaa kwa Watanzania. Tukikurupuka, tukajisahau na kuona kuwa kitendo cha Rais wa Marekani, Barack Obama kuja kutangaza Sera ya Marekani kwa Afrika nchini Tanzania, sawa na alivyofanya Rais xi Jinping tukalewa sifa, tutaishia kuwa na hotuba nzuri huku maisha yakizidi kuwa magumu.
Ombi langu ni kuwa viongozi wetu wawe wabunifu, fursa hizi wazitumie kuwawezesha Watanzania kuanzisha viwanda na kufanya biashara kati ya Tanzania na nchi za Ulaya. Tukifanikiwa katika hilo, nchi yetu itapiga hatua kubwa kimaendeleo kwa kasi ya ajabu.
Karibu Rais Obama, hongera Rais Jakaya Kikwete kwa kufanikisha ugeni huu mkubwa ajabu. Majirani zetu Kenya, kwa miaka 50 iliyopita hawajawahi kupata hata Rais mmoja kutoka Marekani kutembelea taifa hilo.
Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.
Dar es Salaam, Tanzania
0713404827/0784404827