Dunia inashuhudia kuhatarishwa kwa amani baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuliidhinisha Jeshi la Marekani, hivi karibuni, kumuua kwa shambulio la kombora Meja Jenerali Qasem Soleimani wa Iran.
Ni kawaida kwa Merakani kuua watu inayowatuhumu kwa jambo moja au lingine. Tunaambiwa Soleimani alikuwa akipanga njama za kuua raia wa Marekani. Ambalo si la kawaida, ni kumuua mchana kweupe na bila kujificha nyuma ya pazia, kiongozi wa hadhi ya Soleimani.
Hakuna njia iliyo ya wazi kabisa ya kuchochea uhasama kama kuuawa kwa Soleimani; tukio ambalo mchambuzi mmoja wa Marekani alisema ni sawa na Iran kumuua waziri wa ulinzi wa Marekani.
Iran ilitishia na kujibu mapigo kwa kushambulia vituo viwili vya Jeshi la Marekani nchini Iraq na kutamka kuwa hayo majibu yanatosha. Nadhani hilo ni tamko la kisiasa na kwamba bado hatujaona jibu halisi la Iran lenye uzito sawa na kuuawa kwa Soleimani.
Waliyozoea mtindo wa Marekani wa kuua yeyote, wakati wowote, na popote wameshangaa juu ya uamuzi wa Trump, lakini tunao wajibu kutafakari.
Jibu mojawapo linajitokeza kwa mwanajeshi aliyeishi Ulaya kwenye karne ya 18: Jenerali Carl von Clausewitz. Alisema vita ni njia mbadala ya kuendeleza siasa. Hali mbaya ya siasa inayomuandama Rais Trump na jitihada zilizopo za kikatiba za kumuondoa madarakani kwa tuhuma za kukiuka katiba, ni suala lililomsukuma Trump kuelekeza macho ya Wamarekani mbali kabisa na matatizo ya kisiasa yanayomkabili.
Kama Marekani ikikabiliwa na vita dhidi ya Iran, basi Wamarekani watasahau tofauti zao za kisiasa na wataungana kukabiliana na Iran.
Kwa sasa inaelekea vita imeepukwa. Lakini ambacho labda hakikutarajiwa ni kuwa kuuawa kwa Soleimani kumewaunganisha raia wa Iran dhidi ya Marekani. Isitoshe, nchini Iraq, serikali imepiga kura kutaka jeshi la Marekani kuondoka nchini humo kutokana na na kuuawa kwa Soleimani.
Swali la kuuliza ni kwanini ugomvi wa Marekani na Iran utuhusu? Kwanza, wakati wowote amani inapotoweka sehemu yoyote duniani, basi ni wajibu wa kila mtu kukemea vitendo vyote vinavyohatarisha amani hiyo.
Soleimani alikuwa kiongozi mwandamizi wa Iran kwa hiyo tukae na uhakika kwamba ipo siku tutashuhudia tukio la kulipiza kisasi la Iran dhidi ya Marekani. Lakini tukumbushane pia kuwa Iran haina uwendewazimu wa kupambana kijeshi, ana kwa ana, na Marekani. Marekani imejiingiza kwenye vita katika kila pembe ya dunia na kwa sasa ina kambi za kijeshi nchini Syria, Iraq, Afghanistan, na Libya- maeneo ambayo yamejaa makundi mbalimbali ya kijeshi ambayo yanaunga mkono au kushirikiana na Iran.
Kama utajitokeza ulipizaji kisasi mkubwa, basi utajitokeza kwenye maeneo haya. Na kama kuna raia wa Marekani ataathiriwa na malipizi hayo, basi itakuwa ni mamia au maelfu ya raia wa nchi hizi ambao nao pia wataathirika na majibu hayo ya mapigo.
Ilipotokea miaka ya hivi karibuni viongozi wa Tanzania na Rwanda kuanza kurushiana maneno ya uhasama baada ya Rais Jakaya Kikwete kushauri kwenye kikao cha Umoja wa Afrika (AU) kuwa serikali ya Rwanda ianze mazungumzo na waasi waliokuwa wanapambana dhidi ya Rwanda, baadhi ya Watanzania walishabikia uwezekano wa vita dhidi ya Rwanda.
Mmoja wa watu wachache ambaye aliona hatari ya vita alikuwa rafiki yangu wa Kagera. Kagera wanaifahamu vita kati ya Tanzania na Uganda, na hawahitaji kuhadithiwa athari za vita. Hali itakuwa hivyo kwa raia wa Iraq, Iran, Lebanon, na Syria ambako Marekani na Iran zinapambana kupitia makundi mbalimbali.
Hakuna takwimu za uhakika za idadi ya vifo vilivyosababishwa tangu kuvamiwa kwa Iraq na jeshi la Marekani mwaka 2003, lakini hakuna ubishi kuwa uvamizi huo umesababisha vifo na majeruhi kwa kiwango kikubwa ambacho hakijashuhudiwa na Iraq. Kama tumesahau, chanzo cha uvamizi huo ilikuwa ni uongo kuwa Rais Saddam Hussein alikuwa ametengeneza na kumiliki silaha za maangamizi.
Kama hatujali kabisa juu ya kuwapo au kutokuwapo mapambano ya wazi au ya chini kwa chini kati ya Iran na Marekani, basi tukumbuke maafa ambayo wananchi wa nchi hizo nne wamepata au wataendelea kuyapata kwa sababu ya mapambano hayo.
Sisi ambao tunaweza kujidanganya tuko mbali tukumbuke tu athari za kupanda kwa bei ya mafuta. Tayari imeripotiwa kuwa bima ya kusafirisha mafuta kutoka nchi za Uarabuni ambako Tanzania hununua mafuta, imepanda. Tutarajie bei ya mafuta ipande kwa sababu ya uhasama huu.
Kama kuna mtu hajaelewa sababu ya nchi kulazimika kuwa na silaha za maangamizi sababu iko wazi sasa. Siamini kuwa yupo kiongozi yeyote Marekani ambaye anao wendawazimu wa kutosha wa kumuua waziri wa ulinzi wa Korea Kaskazini halafu asianzishe vita ambayo hatutaki hata kuiota.
Historia ya uhasama kati ya Marekani na Iran ni ndefu na haituhusu sana; mbali na kutusaidia tu kufahamu yanaoyoendelea sasa. Kinachotuhusu ni athari zitakazojitokeza kwa sababu ya shambulizi la Marekani lililomuua Soleimani na athari zake kwa mamilioni ya raia wasio Wamarekani.
barua pepe: [email protected]