Serikali ya Kenya ilitangaza hivi majuzi kuwa inaahirisha kwa muda wa miezi sita uamuzi wake wa kuifunga kambi ya wakimbizi ya Daadab iliyo karibu na mpaka wake na Somalia. 

Hapo awali Kenya iliamua kuanza kuifunga kambi hiyo mwishoni mwa Novemba mwaka huu. Ilisema imetenga kiasi cha dola milioni 10 kwa ajili ya kazi hiyo kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) na serikali ya Somalia.  

Baada ya kumalizika kwa muda wa miezi sita, wakimbizi waliobaki hapo wangelazimishwa kuondoka bila ya kupatiwa fidia. Kenya ilisema kati ya Mei na Oktoba mwaka huu tayari zaidi ya wakimbizi 30,000 walichukua hiyo fidia na kurudi kwao kwa hiyari.

Sasa Kenya inasema itaanza kuifunga kambi hiyo baada ya miezi sita, kutokana na ombi la shirika la UN la kuhudumia wakimbizi (UNHCR). Hata hivyo, kumekuwako pia na shinikizo kutoka asasi na serikali za kimataifa.

Kwa mfano, shirika la kimataifa la haki za binadamu (Amnesty International – AI) limesema kufunga kambi ya Dadaab ni sawa na kuwalazimisha wakimbizi wa Kisomali kurudi kwao ambako vita vingali vinaendelea.

Kenya imejibu kuwa hakuna mkimbizi anayelazimishwa kurudi, bali wanarudi kwa hiyari yao katika hali ya usalama na utulivu. Hata hivyo watafiti wa AI walitembelea kambi hiyo mnamo Agosti na kuwahoji wakimbizi. 

Wakagundua kuwa ndugu wawili walirudi Somalia mnamo Januari mwaka huu lakini baada ya miezi minne wakalazimika kurudi Daadab. Walipoulizwa kwanini, walisema walishuhudia baba yao akiuliwa mbele yao, kisha wakalazimishwa kujiunga na wapiganaji wa al-Shabaab, ndipo wakatoroka na kurudi Daadab. 

Asasi nyingine ya kimataifa (Human Rights Watch – HRW) imesema Kenya inapaswa kuahirisha ufungaji wa Daadab. Ikaongeza kuwa UNHCR na nchi wahisani zinapaswa kuishinikiza Kenya iwaruhusu wakimbizi kutoka Somalia kuishi nchini bila ya vitisho vya kufukuzwa, hadi hapo hali ya utulivu itakaporejea nchini mwao.

Shirika la kimataifa la madaktari (MSF) nalo lilizihoji familia 838 katika kambi ya Daadab. Wakagundua kuwa ni robo tu walikuwa tayari kurudi Somalia. Waliobaki hawataki kurudi. 

Kwa ujumla asasi za kimataifa zimekuwa zikiishinikiza Kenya ifanye mipango ya kuwapa wakimbizi hao uraia wa nchi hiyo ili waweze kuishi kama raia wa kawaida kwa kujitafutia kazi badala ya kuishi daima kama wakimbizi wakitegemea posho. Kenya haiku tayari.

Kwani Daadab ni kambi ya wakimbizi iliyo kubwa kuliko zote duniani. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) ina wakimbizi takriban 350,000. Ilianzishwa mwaka 1991 wakati vita vilipoanza kupamba moto nchini Somalia. Wachunguzi wanasema hali hii isingetokea kama Somalia isingeingiliwa na majeshi ya kigeni.  

Somalia ilipata Uhuru wake wa kisiasa mwaka 1960 baada ya wakoloni wa Kiingereza na Kitaliana kujitoa. Lakini kutokana na mipaka bandia iliyowekwa na wakoloni Wasomali wakajikuta wako si tu katika Somalia bali pia katika nchi za jirani za Ethiopia, Djibouti na Kenya.

Ndipo Wasomali walioishi kwa amani kwa karne nyingi sasa wamejikuta wamegawanywa kutokana na mipaka wasioielewa. Hivi ndivyo wakoloni walivyofanya katika bara letu na kutuachia tukivutana.

Mwaka 1969 mapinduzi ya kijeshi yaliongozwa na Siad Barre ambaye alijaribu kuwaunganisha Wasomali. Mwaka 1991 naye akapinduliwa. Yakazuka makundi ya kikabila yakiongozwa na wababe wa kivita (war lords), kila mmoja akitaka kutawala.

Mwezi Desemba 1992 Marekani ikaingiza majeshi yake na ndipo Wasomali wakaja juu walipoona nchi yao imevamiwa na Wazungu tena Wakristo. Wamarekani wakakabiliwa na mbabe wa vita Mohammed Farah Aideed. Walijaribu kumuondoa Aideed lakini wakashindwa. Helikopta mbili za Marekani zikadunguliwa na wanajeshi 18 wakauliwa. 

Maiti za askari wa Marekani zikaburuzwa mitaani na kisha kutundikwa mlingotini. Marekani mara moja ikaamua kujitoa. Ikawa aibu kubwa kwa Marekani na tangu hapo wakaamua kutumia majeshi ya Kiafrika kufanya kazi yao, wao wakitoa fedha, vitendea kazi na mafunzo.  

Mapigano yaliendelea mpaka mwaka 2004 ikaundwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa (TFG). Wasomali walio wengi waliikataa kwa sababu iliundwa na “vibaraka” waliokuwa nje ya nchi. Katika fikra zao TFG ilikuwa serikali ya kupachikwa kwa maslahi ya Marekani. 

Mwaka 2006 Wasomali waliokuwa nchini waliunda serikali iliyoongozwa na mahakama za Kiislamu. Serikali hii (ICU) ilidhibiti maeneo mengi pamoja na mji mkuu wa Mogadishu. Nchi ikawa na amani na utulivu, lakini Marekani ikapatwa na wasiwasi kutokana na utawala huu wa kidini. 

Ikaamua kutuma majeshi ya Kiafrika. Mnamo 2006 majeshi ya Ethiopia yakaingia Somalia kwa niaba ya TFG. Marekani ilitumia ndege zake kusaidia uvamizi huu. Mara hii Wasomali wakaona nchi yao inavamiwa na Wakristo kutoka Ethiopia. 

Mwaka 2007 Umoja wa Afrika (AU) ukaunda kikosi cha kuisaidia TFG iliyokuwa ikishambuliwa na ICU. Kilichofanyika ni kuwapa askari wa Ethiopia waliofadhiliwa na Marekani jina la AU. Nguvu za kijeshi zikatumiwa na raia takriban 400,000 wakalazimishwa kuyahama makazi yao. 

Mwaka 2008 idadi hiyo ikafikia milioni 1.1. Umoja wa Mataifa ikaonya kuwa jumla ya raia milioni 4 walihitaji msaada wa chakula. Nchi ikakabiliwa na ukame uliotengenezwa na mwanadamu. Katika hali hii wengine wakajiunga na uharamia katika bahari. Wengine wakajiunga na kikundi cha al-Shabaab. 

Kufikia Juni 2011 Wasomali wapatao 750,000 wakalazimika kukimbilia nchi za jirani, hasa Kenya. Kila siku wakimbizi zaidi ya 3,000 waliwasili kambini. 

Leo Kenya ina wanajeshi wapatao 4,000 nchini Somalia. Shabaab inadai hawa ni wavamizi nchini mwao, na ndiyo maana nao wamekuwa wakiishambulia Kenya. Mwaka 2013 walishambulia kituo cha biashara cha Westgate (Nairobi) na kuwaua watu 67. Halafu wakashambulia chuo kikuu cha Garissa na kuwaua wanafunzi 147.

Kenya inadai kambi ya Daadab inarahisisha magaidi wa Shabaab kupenya nchini. Hivyo  inaifunga kambi hiyo kwa sababu inatishia usalama wa nchi.

Kenya inadai imechukua uamuzi wa kuifunga Daadab baada ya kushauriana na serikali ya Somalia. Lakini mnamo Juni mwaka huu balozi wa Somalia huko UN aliitaka Kenya kuachana na mpango wake wa kuifunga Daadab. 

Balozi huyo, Ahmed Awad alisema kwa kufanya hivyo Kenya itakuwa inakiuka mikataba ya kimataifa. Pia Kenya itakuwa inaingiza Somalia katika janga kubwa, kwa sababu nchi hiyo haina uwezo wa kuwapokea wakimbizi wote hao. 

Balozi Awad aliionya Kenya kuwa iwapo italazimisha kuifunga Daadab basi uhusiano wa Kenya na Somalia utaharibika.

Balozi huyo akaongeza: “Kuwalazimisha wakimbizi wote hao kurudi makwao wakati hali ya huko hairuhusu, ni kuharibu uhusiano mzuri uliojengeka baada ya kuwatunza kwa muda wa miaka 25. Hivyo Kenya inapaswa kusikiliza maoni ya kimataifa na nchi ya kirafiki ya Somalia”.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Kenya, Mwenda Njoka, alimjibu balozi Awad kwa kusema kuwa hatua iliyokusudiwa haina maana ya kuwatupa au kuwasukumiza wakimbizi nchini mwao, bali mipango imefanywa na wakuu wa jimbo la Jubaland karibu na Kismayu. Hapa eka 10,000 zimetengwa kuwaweka wakimbizi watakaorudi.

Awad akajibu kuwa mpango huu wa Jubaland unakiuka makubaliano kati ya Kenya, Somalia na UNHCR kuhusu wakimbizi kurejea kwa hiyari yao. Akaongeza kuwa inasikitisha kuwa Kenya sasa inafikia makubaliano na watawala wa jimbo wakati kuna mpango maalum uliokubaliwa rasmi na serikali ya Somalia.

Ni vizuri tukajua kuwa Kenya imekuwa ikishinikizwa pia na Marekani. Na kwa vile Kenya inategemea sana misaada kutoka nchi hiyo, yumkini ndio imeifanya Kenya ibadili nia yake kuhusu Daadab. 

Mwaka jana waandishi walidiriki kuona nyaraka kutoka wizara ya mambo ya nje ya Marekani. Hizi ni barua zilizoandikwa na maofisa wake waliotembelea Kenya mnamo 2011 kuona hali ya Daadab. 

Wakati huo Kenya ilikuwa inatawaliwa na serikali ya muungano wa kitaifa, waziri mkuu akiwa Raila Odinga. Naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Reuben Brigety, alimtembelea Odinga pamoja na waziri wake wa mambo ya ndani, Profesa George Saitoti na kuzungumza nao kuhusu hali ya Daadab.

Brigety akaandika ripoti kwa mabosi wake huko Washington akisema:

“Nimetumia saa nane nikiwa na Odinga. Nilisafiri katika ndege yake hadi Daadab. Tulitumia gari lake tukitembelea Daadab. Tukawatembelea wakimbizi tukiwa na waziri Saitoti. Tuliawaona watoto na wanawake walivyokondeana baada ya kutembea kutoka Somalia hadi Daadab. Nilimuona Odinga akibubujikwa na machozi. Baadaye tukarudi Nairobi katika ndege yake huku tukijadiliana. Mwishowe akakubali kuwa kuna haja ya kupanua Daadab”. 

Brigety anaeleza kuwa Saitoti alikuwa na maoni tofauti. Yeye alisisitiza kuwa Daadab inatumiwa na magaidi wa Shabaab kupenya nchini Kenya kwa kujifanya wakimbizi. Saitoti akaambiwa kuwa ni wajibu wa Kenya kuwalinda wakimbizi. Ni wajibu kwa mujibu wa sharia ya kimataifa na sharia ya Kenya yenyewe.

Bila shaka Brigety alifanikiwa. Kwani Marekani imeipa Kenya misaada ya kijeshi ya dola milioni 141 kati ya 2010 na 2014. Ikaahidi kutoa dola milioni 100 mwaka 2015. Hii ni kwa ajili ya kazi inayofanya Kenya nchini Somalia. Halafu utategemeaje Odinga akatae maoni/maagizo ya Marekani?

Licha ya Kenya nchi zingine zenye majeshi yake huko Somalia ni  Burundi, Djibouti, Ethiopia, Ghana, Nigeria, Sierra Leone na Uganda. Hawa wanajiita majeshi ya Umoja wa Afrika ambao jumla yao ni 22,000. 

Wote hawa wanafadhiliwa na Marekani ambayo pia inatumia ndege zake za kivita aina ya Drone. Utategemeaje nchi hizi kumkatalia Brigety? 

Na Brigety naye baada ya kazi “nzuri” akapandishwa cheo na kuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Afrika huko Addis Ababa.  

Sasa tuone kama baada ya miezi sita Kenya itafanikiwa kuifunga Daadab.