IDARA ya Ujasusi ya Marekani imemuonya mgombea urais kwa tiketi ya Republican, Donald Trump, juu ya kile inachodai ni kitisho cha kweli na cha wazi kutoka Iran inayotaka kumuua.

Timu ya kampeni ya mgombea huyo ilisema kwenye taarifa yake ya jana kwamba Ofisi ya Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa ilimpa taarifa kwamba kumekuwa na juhudi za wazi za kumuua kutoka Iran, kwa lengo la kuihujumu Marekani na kupandikiza machafuko.

Kwa mujibu wa timu hiyo, idara ya ujasusi inaamini kumekuwa matukio ya mashambulizi dhidi ya Trump katika miezi ya karibuni na kwamba imeimarisha ulinzi kwa bilionea huyo anayetaka kurejea madarakani kupitia uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka huu. Iran inakanusha vikali tuhuma hizo.

Marekani inafanya uchaguzi wake mkuu Novemba 5, ambapo hadi sasa utafiti wa maoni ya wapigakura yanaonesha kuwa Trump na hasimu wake wa Democrat, Kamala Harris, wanachuana vikali.

Please follow and like us:
Pin Share