Rais wa Marekani Barack Obama yupo hapa nchini kwa ziara ya kiserikali. Ujio wa Obama umekuwa na shamrashamra nyingi si tu Dar es Salaam bali macho na masikio ya Watanzania wote yameelekezwa katika safari hii. Ni ziara ambayo pamoja na mambo mengine mengi, pia imekusudia kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Maekani.

Kwa miongo mingi iliyopita, Marekani imekuwa na historia ya kuzisaidia na kushirikiana na nchi mbalimbali za Kiafrika. Maeneo ambayo Marekani imeng’aa kuisaidia Afrika ni katika mapambano dhidi magonjwa ya malaria na Ukimwi.

 

Pia Marekani imekuwa mstari wa mbele katika kuzisaidia nchi za Afrika kibajeti, kiulinzi, haki za binadamu na utawala bora. Eneo jingine muhimu ambalo Marekani imeelekeza macho yake Afrika ni katika ushirikiano wa kibiashara. Ni katika ushirikiano huu wa kibiashara ndipo Marekani iliamua kuanzisha mpango na sheria maalum iitwayo Africa Growth Opportunities Act (AGOA).

 

Kupitia mpango na sheria hii, Marekani imekusudia kuimarisha ushirikiano wa kibiashara wenye usawa baina ya Africa na wao. Kabla ya AGOA ilionekana kuwa nchi nyingi za Afrika hazikuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye kukidhi vigezo vya viwango vilivyoko katika masoko ya Marekani.

 

Mojawapo ya zana muhimu katika kupambana na umaskini ni biashara. Afrika inahitaji kuongeza uwezo wake wa kusafirisha bidhaa inazozizalisha kwenda nje ya nchi iweze kugharimia maendeleo yake. Mbali na changamoto za ruzuku katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, fursa ya Afrika kusafirisha bidhaa zake katika nchi zilizoendelea ni finyu mno.

 

Ukomo wa ujazo (quotas) unazuia kiwango cha bidhaa zinazoweza kuingia katika soko fulani; na wakati huohuo ushuru unaotozwa kwa bidhaa hizo unazifanya bidhaa hizo kuwa gharama na zinashindwa kushindana katika masoko hayo ya kimataifa. Wakati mwingine viwango vya ushuru vinakuwa vikubwa mno kiasi kwamba Afrika inakwama kuendelea kuzalisha bidhaa hizo kwa kukosa masoko na ushindani.

 

AGOA ni njia mojawapo ambayo Marekani imeamua kuitumia ili kufungua masoko yake kwa Afrika. AGOA ilianzishwa mwaka 2000 kama sheria ya kibiashara inayokusudia kuongeza na kuhamasisha biashara baina ya nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara na Marekani. Katika sheria hii Marekani inaruhusu bidhaa kutoka nchi hizi kuingia nchini humo pasipo kulipiwa kodi.

 

Tangu kuanza kwa mpango huu nchi nyingi zimeendelea kunufaika mno kibiashara. Zaidi ya bidhaa 6,000 zimeorodheshwa kunufaika na mpango huu wa AGOA.

 

Kimsingi ili nchi ipate fursa ya kuingizwa katika mpango wa AGOA, inatakiwa iwe imetimiza masharti kadhaa ikiwamo kuboresha utawala wa sheria, haki za binadamu na kuheshimu haki na viwango vya wafanyakazi. Tanzania imekuwa ni moja ya nchi takriban 40 zilizokidhi vigezo, hivyo na hadi sasa imo ndani ya AGOA.

 

Baadhi ya bidhaa zilizomo kwenye orodha ya mpango wa AGOA ni pamoja na madini, mafuta, bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, bidhaa zilizoongezwa thamani zikiwamo nguo, viatu na vinywaji. Hii ina maana wakulima wa maua, wafugaji wa nyuki, ng’ombe na bidhaa nyingine wote wana nafasi ya kunufaika na AGOA.

 

Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha bidhaa zinazoingia Marekani kutoka katika nchi za AGOA, kimekuwa kikiongezeka kila mwaka tangu kuanzishwa kwa AGOA.  Inatajwa kuwa kiwango hicho kimekuwa kikiongezeka kwa wastani wa asilimia 30. Vile vile biashara baina ya pande hizi mbili imeongezeka mara tatu zaidi ya ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwa sheria hii ya AGOA.

 

Wajasiriamali wa Tanzania hatujachangamkia vya kutosha fursa ya AGOA kwa sababu taarifa zinaonesha kuwa nchi zinazoongoza kuitumia fursa hii ni zile za Magharibi mwa Afrika. Katika jumla ya thamani ya bidhaa zilizopelekwa Marekani za takriban dola bilioni 100, mafuta yanaonekana kuongoza, ingawa nchi zinazozalisha bidhaa za kilimo, nguo na mashine za kimakenika zimenufaika pia.

 

Ingawa AGOA ilipangwa kukoma mwaka 2008, lakini Marekani iliamua kupitisha marekebisho ya sheria ya AGOA na kurefusha mpango wa AGOA hadi mwaka 2015. Katika mpango na marekebisho haya inaruhusu nchi maskini kutumia malighafi za bei nafuu kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa ajili ya kutengeneza nguo na kuzipeleka Marekani.

 

Kila mwaka huwa kunaitishwa jukwaa la AGOA ambapo huwaleta pamoja viongozi wa kiserikali na sekta binafsi kutoka Afrika na Marekani. Jukwaa hili hufanyika jijini Washngton kila mwaka na pia huitishwa katika mojawapo  ya nchi zilizokidhi vigezo kuwamo katika AGOA. Hadi sasa majukwaa ya AGOA yamefanyika mara nne jijini Washington, na mara moja moja katika nchi za Senegal, Ghana, Kenya na Zambia.

 

Kimsingi mpango wa AGOA umelenga kuwanufaisha wajasiriamali ambao ndiyo wanaotakiwa kuchangamkia fursa ya kuzalisha bidhaa na kuzisafirisha Marekani ambako licha ya kusamehewa ushuru lakini pia kuna masoko ya uhakika. Ni katika njia hii ndipo ambapo nchi yetu inaongeza thamani yake kwa kupata fedha nyingi za kigeni na kukuza uchumi.

 

Wajasiriamali na kampuni zote zinazotaka kusafirisha bidhaa zake kupitia mpango wa AGOA, ni sharti wafikie vigezo kadhaa vya biashara za kimataifa ikiwamo kuwa na maelezo sawia na ya kina kuhusu asili (zinakotoka) ya bidhaa zenyewe.

 

Msafirishaji husika (kampuni, mjasiriamali) anatakiwa kujisajili katika wizara husika katika nchi anakotoka. Kwa hapa msafirishaji atatakiwa kujisajili katika Wizara ya Viwanda na Biashara. Vile vile kunakuwa na hatua kadhaa za kufuata ili kupatiwa vibali vya kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi.

 

Vitengo katika serikali na ndani ya wizara zinazohusika na ufanikishaji wa mpango wa AGOA, kwa pamoja wanahitaji taarifa za wajasiriamali na hizi kampuni kwa ajili ya takwimu, kudhibiti ubora na viwango vya bidhaa zinazopelekwa huko nje kila inapohitajika.

 

Nimebainisha hapo juu ya kwamba wajasiriamali na kampuni zina fursa za kusajiliwa na kunufaika na AGOA, hata hivyo pia niseme kuwa anayesajiliwa anaweza kuwa mzalishaji, mtengenezaji ama msambazaji wa bidhaa zilizopo kwenye orodha ya AGOA.

 

Kwa upande wa Tanzania yeyote anayetaka kusajiliwa kwa ajili ya AGOA anashauriwa kuwa amejiunga ama kusajiliwa na mpango wa EPZ (Export Processing Zone). EPZ ni maeneo maalum ya kiuchumi na kiuzalishaji yenye lengo la kuwasaidia wazalishaji kuongeza ubora wa bidhaa zao na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa katika maeneo hayo zinakidhi vigezo vyote vya kimataifa.

 

Vigezo rahisi vinahitajika kwa msafirishaji kujiunga na AGOA ikiwamo jina la biashara, majina ya wakurugenzi, orodha ya bidhaa zinazokusudiwa kusafirishwa kwenda nje, orodha ya malighafi zinazotumika na rejea zake za ushuru, ufafanuzi kuhusu bidhaa na mchanganuo gharama.  Si lazima mzalishaji, msambazaji ama mtengenezaji kuhangaika na kila kitu, isipokuwa inawezekana kuwatumia mawakala wa usafirishaji na uingizaji.

 

Serikali kupitia vyombo vyake vinavyohusika na biashara ikiwamo TRA vinatoa usaidizi na maelekezo ya kutosha sana kuwawezesha wajasiriamali wanaochangamkia AGOA. Katika vitengo hivi mjasiriamali anayechangamkia fursa ya AGOA atapewa nyaraka zote zinazohitajika ambazo zitamsaidia kupokewa kwa bidhaa zake huko Marekani.

 

Serikali kupitia vyombo vyake vya kibiashara vitakagua na kujiridhisha katika maeneo yafuatayo kabla ya kutoa nyaraka na ruhusa: Watakagua maghala ya kuhifadhia, watasaidia kuidhinisha malighafi za bidhaa husika, watapitia takwimu za usafirishaji kwa mujibu wa taratibu za AGOA, watakabidhi vyeti na nyaraka kwa mjasiriamali.

 

Wajasiriamali wa Tanzania tunatakiwa tujiamini kwa kuchangamkia fursa za kimataifa ikiwamo AGOA. Hakuna sababu ya kujiweka kando na kudhani kuwa AGOA ni ya watu fulani fulani ama kudhani ni kwa ajili ya kampuni kubwa. Kila mjasiriamali ana haki ya kunufaika na AGOA mradi tu akidhi vigezo vilivyoainishwa.

 

Tujenge mazoea ya kutembelea vitengo mbalimbali serikalini ikiwamo Wizara ya Viwanda na Biashara ili kujifunza na kupewa maelekezo ya namna ya kunufaika na mpango wa AGOA. Mbali na kutembelea wizarani, vile vile wajasiriamali wanaweza kutembelea Kituo cha Uwekezaji (TIC) pamoja na chemba ya TCCIA.

 

0719 127 901,

[email protected]