Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Biharamulo

WAKATI Serikali ikiendelea na uchunguzi wa chanzo cha ugonjwa wa Marburg ulioibuka hivi karibuni wilayani Biharamulo mkoani Kagera na kusababisha vifo, baadhi ya wananchi wa Kata za Ruziba, Nyarubungo, Bisibo na Nyakahura,wamesema wapo hatarini kukumbwa na njaa kutokana na ongezeko la nyani.

Hatua hiyo inatokana na wananchi kuogopa kuwafukuza nyani wanaoshambulia mazao yao kwa hofu ya kuambikizwa ugonjwa wa Marburg.

Aidha wameiomba Serikali kufanya jitihada za makusudi kuwaondoa haraka wanyama hao kwa madai wamekuwa tishio la uhai wa jamii kutokana na kuhisiwa kuwa chanzo cha ugonjwa huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo,Leo Rushahu,akitoa maelezo kwa madiwani.

Diwani wa Kata ya Ruziba,Athanas Sumbuso, amesema mazao mengi ya wananchi wake yameshambuliwa vibaya na nyani hali inayotishia familia nyingi kukosa chakula cha kujikimu.

“Nyani wameongezeka sana na wanashambulia mahindi,mihogo na maharage ya wananchi na tunashindwa kuwafukuza kama zamani kwa kuhofia kuambikizwa ugonjwa wa marburg, tunaiomba sana serikali itutazame kwa jicho la huruma siye wakazi wa Ruziba kwa kuwa ndiyo waathirika wakubwa wa maambukizi ya ugonjwa huo”

“Hata jana kuna mwananchi wangu amefariki dunia akiwa na dalili za ugonjwa huo,japo siwezi kuthibitisha kama ni Marburg moja kwa moja kwa sababu mie siyo daktari, isipokuwa baada ya wataalam kumpokea hospitali na muda mfupi kufariki ndugu waliambiwa itakayozika ni Serikali na kwamba hawaruhusiwi kuweka matanga wala kukusanyika”amesema Sumbuso.

Kadhalika diwani wa Kata ya Nyarubungo, Petro Kizuluja,amesema wananchi wake wapo na hofu kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa marburg kutokana na baadhi yao kushirikiana chakula na wanyama hao.

“Sasa hivi tunaambiwa na wataalam kuwa ugonjwa huo unaambukizwa kwa njia ya maji maji na huku kwetu ni msimu wa kilimo nyani wanakula mihogo, mahindi,na maembe ambayo wananchi nao wanatumia chakula hicho kila siku kwanini Sasa serikali isiwaondoe nyani hao ili kuwanusuru wananchi” amehoji Kizuluja.

Diwani wa Biharamulo mjini, David Mwenenkundwa, ameiomba Serikali kuwaondoa wanyama hao,pamoja na popo waliopo majumbani kutokana na kuhisiwa kuwa chanzo kikuu cha ugonjwa wa marburg hatua itakayo punguza hofu kwa jamii.

Walikuwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi kwaajili ya kupitia mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 na kusoma mpango wa bajeti wa 2024/25 kabla ya kupitisha mpango mpya wa 2025/26.

Bakari Salimu,Mratibu wa Afya Wilaya ya Biharamulo,amesema changamoto ya wananchi kukabiliwa na tishio la njaa hasa kwenye kata zilizoathirika na ugonjwa wa marburg, zitawasilishwa kwenye wizara ya afya pamoja na mashirika ya ndani na nje yaliyojitokeza kushirikiana na serikali katika mapambano ya ugonjwa huo.

“Yapo mashirika mbalimbali ikiwemo shirika la afya duniani (WHO) ambao wanatusaidia pesa, tutafikisha kilio hiki cha wananchi ili tuone wakakavyo tushika mkono kuwanusuru wananchi wetu kukumbwa na baa la njaa,hata hivyo ipo miradi ambayo itaanza kuwanufausha wananchi wa wilaya ya Biharamulo baada ya serikali kutoa fedha pamoja na wahisani mbalimbali katika mpango huu”amesema Salimu

Merisa Kyamani,Mratibu wa Afya ngazi ya jamii mkoa wa kagera,akitoa ufafanuzi wa maswali ya madiwani hao amesema ni vyema wananchi kuendelea kuchukua tahadhali za kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kujiepusha kugusa au kula wanyama kama vile popo,tumbili,nyani na sokwe.

Vilevile kugusa majimaji ya mwili wa mgonjwa kama vile damu,mate, matapishi, kinyesi,machozi, kamasi,jasho au mkojo.