Nchi tano za kusini mwa Afrika zenye idadi kubwa ya tembo zimeanza kudai haki ya kuuza pembe za wanyama hao kwa msisitizo kuwa rasilimali hiyo iwekewe utaratibu utakaonufaisha wakazi wa maeneo ya mapori wanamohifadhiwa.

Marais kutoka nchi za Botswana, Zimbabwe, Zambia na Namibia, pamoja na Waziri wa Mazingira kutoka Angola walikutana wiki iliyopita mjini Kasane, Botswana, kuweka sera ya pamoja ya mambo ya nje kuhusu udhibiti wa tembo na kubainisha kuwa mgogoro uliopo kati ya tembo na wakazi wa maeneo ya vijijini umekuwa ukiongezeka. Uuzaji wa pembe za ndovu hufanyika baada ya kupata kibali kutoka jumuiya ya kimataifa kupitia taasisi ya kimataifa inayodhibiti biashara ya wanyama na viumbe vilivyo hatarini kutoweka (CITES).

Inaelezwa kuwa ujangili wa tembo katika eneo la kusini mwa Afrika umekuwa si wa kutisha tangu biashara ya pembe za tembo kudhibitiwa, lakini hata hivyo idadi ya pembe hizo imekuwa ikiongezeka kutokana na vifo vya tembo kwa njia ya asili.

Wanaharakati wa mazingira wamekuwa wakieleza kuwa marufuku ya biashara ya pembe za ndovu imesaidia kupunguza ujangili dhidi ya wanyama hao.

Katika hatua nyingine, uongozi wa CITES umepanga kukutana baadaye mwezi huu nchini Sri Lanka, lakini hata hivyo mkutano huo uliahirishwa baada ya nchi hiyo kushambuliwa kwa mabomu katika kile kinachotajwa kuwa ni kitendo cha ugaidi.

“Tumeamua kuweka wazi msimamo wetu kuhusu udhibiti wa tembo, sauti yetu iwe moja kwa ajili ya jamii yetu,” amesema Rais Emerson Mnangagwa wa Zimbabwe, nchi ambayo ni ya pili duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo ikitanguliwa na Botswana.

Ameongeza: “Hatuwezi kukubaliana na kila kitu kwenye marufuku hii chini ya CITES, kuna wakati mwingine ni lazima kuzingatia masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na juhudi za serikali zetu.

Idadi ya tembo nchini Botswana imeongezeka hadi 160,000 kutoka tembo  55,000 mwaka 1991, lakini kwa mujibu wa serikali ya nchi hiyo kumekuwa na ongezeko la migogoro kati ya wanadamu na wanyama hao, hasa eneo la uharibifu.

Kundi kubwa la tembo limekuwa likisafiri kuingia na kutoka katika nchi hizo tano kupitia mpaka mmoja unaoziunganisha, unaojulikana kwa jina la Kavango Zambezi, mpaka wa aina yake wenye malisho ya wanyama hao kama nyasi, mabwawa na mimea mingine mbalimbali.

“Hatuwezi kuendelea kuwa watazamaji tu wakati wengine wanaendesha mijadala na kufanya uamuzi kuhusu tembo wetu,” amesema Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi, katika mkutano huo wa wakuu hao wa nchi tano.

Masisi ametaka kuondolewa kwa marufuku ya uwindaji nchini Botswana, na serikali imependekeza njia mbadala ya ‘kuvuna’ tembo ili kunufaisha wananchi wa taifa hilo.

Hata hivyo, wakosoaji akiwamo mtangulizi wake katika Ikulu ya nchi hiyo, Ian Khama, wanasema msimamo huo wa rais utaathiri sekta ya utalii ingawa kisiasa unamwezesha rais huyo kupata kura za watu wa vijijini na hatimaye kukinufaisha Chama tawala cha Democratic katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba mwaka huu. Sekta ya utalii nchini Botaswana hushika nafasi ya tano katika kuchangia uchumi wa nchi hiyo.

Afrika inatajwa kupoteza tembo takriban 111,000 katika kipindi cha miaka 10 hadi mwaka 2016, katika wakati ambao ujangili ulishika kasi ikilinganishwa na kipindi cha miaka 25 nyuma ya hapo, kwa mujibu wa Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi Asili. Pembe nyingi za ndovu huuzwa nchi za mashariki mwa Bara la Asia.

Nchi hizo tano vilevile zimekubaliana kuweka mfumo mzuri zaidi wa kiteknolojia katika kujua idadi halisi ya tembo, sambamba na kuzinufaisha jamii zinazoishi kuzunguka hifadhi za tembo hao.

“Asubuhi ya leo nimewasikiliza wataalamu wakitoa mada zao kwetu, nilitaka kuwauliza wanatokea nchi gani?” amesema Hage Geingob, Rais wa taifa la Namibia na kuongeza: “Kama wanatokea nchi za Ulaya ama Marekani, nilitaka kuwauliza kwa namna gani waliangamiza tembo wote waliokuwamo nchini mwao halafu leo wanakuja kutoa mhadhara mbele yetu.”