Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambaye pia ni mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mikoa ya Lindi na Mtwara, Zuberi Ally Maulid, amefichua kinachoendelea kuhusu wakulima kurudishiwa korosho zinazodaiwa ni mbovu.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo ambaye amewahi kuwa mbunge ndani ya Bunge la Tanzania, hali si shwari katika mchakato wa ununuzi na malipo ya korosho.

Katika mazungumzo yake na JAMHURI, spika huyo amebainisha mambo mawili ya kipekee katika mwenendo wa mchakato huo wa ununuzi.

Jambo la kwanza, namna wakulima wanavyorudishiwa korosho zao kwa madai kuwa ni mbovu, na katika hili, anasema wakati wa kupeleka korosho hizo kwenye vyama vya ushirika wakulima hao walikabidhiwa risiti zinazoonyesha kuwa korosho zao ni daraja la kwanza.

Jambo la pili, kwa mujibu wa mwanasiasa huyo kutoka Zanzibar, ni wakulima kulipwa sehemu ya madai yao bila kuwekwa bayana ni lini malipo yaliyobaki yatakamilishwa, akisisitiza kuwa takwimu za waliolipwa kutoka serikalini haziakisi hali halisi, na kwamba wasiolipwa ni wengi tofauti na taarifa ya serikali inayodai kuwa waliolipwa ni asilimia 80.

Zuberi ambaye amefanya ziara Lindi na Mtwara wiki mbili zilizopita, akikutana na wananchi ambao miongoni mwao ni wanachama wa CCM ngazi ya mashina, anasema hali ya kiuchumi kwa wananchi imeathirika, miongoni mwao wakishindwa kugharimia huduma za kifamilia, ikiwa ni pamoja na kulipa ada za watoto shuleni na baadhi wakipata wakati mgumu kuandaa mashamba yao kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo hicho cha korosho.

“Nimekwenda maeneo mbalimbali, uamuzi uliokuwapo ni kwamba watu wenye tani moja na nusu walipwe kwanza ambao ni wengi. Serikali inasema imewalipa kwa asilimia 80, taarifa hizi haziakisi ukweli. Nitafikisha taarifa hizi kwa Mheshimiwa Rais John Magufuli ambaye amekuwa na nia njema mno katika uamuzi wake wa kununua korosho ili kuwanusuru walalahoi,” alisema Zuberi.

Lakini wakati Zuberi akisema hayo, viongozi wakuu wa chama tawala mikoa ya Lindi na Mtwara wamekuwa na mitazamo inayogongana.

Wakati Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi, Fadhili Juma, akisema katika mkoa wake wengi wamekwisha kulipwa, akiunga mkono takwimu za serikali, hali ni tofauti kwa mwenzake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Yusuph Nanila, ambaye amewahi kuwa kiongozi wa chama cha ushirika, anayesema takwimu hizo haziakisi hali halisi.

Lakini Hassan Yakub kutoka Kampuni binafsi ya Hyate Organic Farms, anazungumzia suala la korosho mbovu akisema katika utaratibu wa miaka iliyopita, korosho mbovu zilikuwa hazirudishwi kwa wakulima, kwa kuwa baadhi ya viongozi, miongoni mwao wa Bodi ya Korosho walikuwa wakiziuza korosho hizo kwa wabanguaji wa ndani kwa bei kati ya shilingi 1,500 hadi 2,000 kwa kilo moja, kwa ajili ya soko la ndani.

“Kwa sasa serikali ndiyo mnunuzi wa korosho, haiwezi kununua korosho mbovu kwa kuwa haina sehemu ya kuziuza, ni lazima zirejeshwe kwa mkulima. Hizi korosho mbovu awali zilikuwa zinauzwa na baadhi ya watendaji kwa kushirikiana na sehemu ya wajumbe wa Bodi ya Korosho na vyama vya ushirika, fedha hizi walikuwa wanagawana,” anadai Yakub.

Lakini kuhusu suala hilo la korosho mbovu, Mohamed Said Duka, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika (TANECO) kwa kuzingatia uzoefu wao wa miaka iliyopita, anasema: “Siku zote korosho mbovu zilikuwa zinarudishwa kwa wakulima katika ngazi ya vyama vya msingi kabla ya kupelekwa ghala kuu. Kule kwenye maghala makuu zinakwenda korosho za daraja la juu kabisa.

Migongano ya vigogo

Katika hali inayoashiria mgongano kati ya wanasiasa, Mwenyekiti wa CCM Mtwara, Yusuph Nanila, amezungumzia mvutano kuhusu wakulima waliolipwa akisema: “Asilimia 80 ya malipo kwa wakulima imetoka wapi? Huku (Mtwara) hiyo hali haipo. Sisi kama chama tawala hatujaambiwa chochote ingawa ndio wasimamizi wa ilani, hatuna taarifa za serikali, nasi tunasikia tu, ofisi yangu haina taarifa. Tunasikia tu mtandaoni malipo yamefanyika kwa asilimia 80.

“Tumemwambia mlezi wa chama mkoani kwetu (Spika Zuberi Maulid) kwamba taarifa za serikali nasi tunazisikia kuwa ni asilimia 80 ya malipo yamefanyika. Lakini tulimpeleka vijijini, akakutana na wananchi, wengine ni viongozi wa CCM kwenye mashina, wote wanadai hawajalipwa, tumempeleka vijijini halmashauri za Newala, Masasi na Mtwara.

“Baada ya ziara hiyo naye alionyesha wasiwasi kuhusu uhalisia wa malipo ya asilimia 80. Mimi hata kwenye kikao kimojawapo cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ni limwomba Mwenyekiti wetu, Rais John Magufuli, aje kufanya ziara bado wananchi wanamuamini na kumpenda, wanajua yeye ndiye mwenye suluhisho la sakata hili.

“Kwa hali inavyokwenda nahisi kuna viongozi wetu serikalini hawampatii taarifa halisi rais wetu. Tunajua alifanya uamuzi mzuri kwa ajili ya kusaidia walalahoi lakini tatizo ni wanaotekeleza uamuzi huo mzuri wa rais. Bado wananchi wanatamani aje Mtwara kuzungumza na wakulima.”

Lakini Mwenyekiti wa CCM Lindi, Fadhili, anagongana na mwenzake huyo wa Mtwara akisema: “Malipo yamefanyika vizuri. Mimi nasema ni zaidi ya asilimia 85, si tena ile asilimia 80 inayosemwa na serikali. Huku Lindi watu ambao wamelipwa ni wengi sana.”

Naye Hassan Yakub kutoka Kampuni binafsi ya Hyate Organic Farms, anasifu uamuzi wa serikali kununua korosho kutoka kwa mkulima kwa kuwa kwa sehemu kubwa umepunguza maumivu kwa wakulima.

Yakub anasema wanaolalamikia uamuzi wa sasa kwa namna fulani masilahi yao binafsi yamevurugika baada ya serikali kuingilia kati suala hilo la ununuzi wa korosho.

Mohamed Said Duka, katika kuzungumzia malipo ya wakulima wa korosho, anasema: “Licha ya mimi kuwa kiongozi wa chama cha ushirika lakini wanaolipwa mimi siwajui. Mwaka jana nilikuwa nawajua kwa sababu sisi wa ushirika tulishirikishwa. Kwa sasa wanaofanya malipo ni Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Ninachojua ni kwamba kwenye chama chetu tulikusanya tani 19, lakini sijui namna malipo kwa wakulima yalivyofanyika.

Ahadi ya serikali

Katika hatua nyingine, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, mwishoni mwa wiki aliwaambia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji  waliofanya ziara mkoani Lindi kwamba, hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, wakulima wote wanaodai fedha za korosho baada ya kuziuza kwa serikali watakuwa wamekwishalipwa.

“Kumekuwa na urasimu mkubwa tangu kuanza kwa zoezi hili la uhakiki lakini sasa tumeamua kama serikali kabla ya mwisho wa mwezi huu wa tatu wakulima wote wawe wamelipwa malipo yao ili kuondoa adha wanazokumbana nazo,” amesema waziri huyo.

Waziri amesema hadi sasa tani 222,684 zimekwishakusanywa na kwamba hadi kufikia Machi 14, 2019 tayari jumla ya shilingi bilioni 596.9 zimekwishalipwa kwa wakulima kati ya shilingi bilioni 723.

Lakini kwa upande wake, Mwenyekiti Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge, Dk. Christine Ishengoma alimtaka Waziri huyo wa Kilimo kuhakikisha kuwa taarifa ya malipo ya wakulima wote wa korosho inafika bungeni Aprili 2, mwaka huu.

Uamuzi wa serikali kununua korosho ulitolewa mwishoni mwa mwaka jana kupitia agizo la moja kwa moja la Rais John Magufuli, na katika utekelezaji wa suala hilo, rais alilazimika kufanya mabadiliko madogo ya mawaziri, akimwondoa aliyekuwa Waziri wa Biashara, Charles Mwijage na mwenzake wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, nafasi hizo zikachukuliwa na Japhet Hasunga – Wizara ya Kilimo, na Joseph Kakunda – Wizara ya Biashara.