Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Gaita
Zaidi ya ekari sita za mashamba ya mpunga, mahindi, mihogo na viazi yameharibiwa na maporomoko ya udongo ambayo yametokana na mvua kubwa ambayo inaendelea kunyesha mkoani Geita.
Tukio hilo limetokea kwenye mtaa wa Nshinde Kata ya Nyankumbu Mjini Geita ambapo zaidi ya wananchi 20 wameathirika na maporomoko hayo.
Baadhi ya wananchi ambao wanafanya shughuli za kilimo wamesema tukio hilo la maporomoko lilienda sambamba na kimbunga ambacho kilitokea wakati mvua zikinyesha.
“Ilikuwa ni Jumapili jioni tulisikia mtikisiko mkubwa baada ya kuja kuangalia siku ya jana ambayo ilikuwa Jumatatu tulikuta ardhi imefunika mazao yetu mimi nilikuwa nimelima viazi ekari moja vyote vimeteketea na maporomoko na ndio chakula ambacho nilikuwa nategemea kwa ajili ya familia yangu sina tena namna zaidi ya kuiomba Serikali kuona namna ya kutusaidia” amesema Neema Mapambano, mkazi mtaa wa Nshinde.
“Ekari mbili za Mpunga zote zimeharibika kwa kufunikwa na matope ambayo yametokana na maporomoko na hii ni mara ya pili mwaka 2016 yalitokea tena haya maporomoko na kuharibu maeneo yetu ukweli tumeathirika sehemu kubwa ya mashamba yetu”Masumbuko Masanja Mkazi wa mtaa wa Nshinde.
Mwenyekiti wa mtaa wa Nshinde Edward Lukonya ,ambaye amefika na kuona uharibifu mkubwa wa mashamba kwenye maeneo hayo ametumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuona namna ya kuwasaidia wananchi hao ambao vyakula vyao vimeathirika na maporomoko.
“Ni jambo la kusikitisha sababu wananchi wangu wamepatwa na ofu kubwa ninachokiomba kwa serikali waje wataalumu waone nini kimesababisha pamoja na kuja kufanya tathimini ya wananchi ambao wamepata hasara kubwa kutokana na maporomoko ambayo yametokea”Edward Lukonya M/kiti Mtaa wa Nshinde.