Na Wakili Stephen Malosha
Asiyefanya kazi na asile. Hayo ni maneno maarufu sana katika utawala
huu wa awamu ya tano. Maneno haya yamekuwa yakitamkwa mara
kwa mara na Rais John Magufuli katika kuhimiza Watanzania wafanye
kazi. Hii inaonesha kwa namna moja au nyingine umuhumu wa dhana
ya kazi katika nchi yetu, na kwamba anayefanya kazi anastahili kupata
ujira (ili apate kula).
Ni busara pia nikatanabahisha kuwa Katiba ya Tanzania ya mwaka
1977 inatamka na kuelekeza kwamba yeyote yule anayefanya kazi
anastahili kupewa ujira unaostahili kulingana na kile alichokifanya.
Kimsingi, sheria za kazi zipo kwa ajili ya kusimamia mahusiano baina
ya waajiri na wafanyakazi mahala pa kazi. Umuhimu wa sheria hizi ni
kwamba zinasaidia kuleta amani, utulivu na hatimaye kuleta tija mahala
pa kazi.
Makala hii inalenga kuangalia matumizi ya sheria ya kazi nchini. Sheria
zitakazojadiliwa ni Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Na. 6/2004 na
Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7/2004.
Nadharia ya sheria za kazi (theoretical basis).
Mahusiano ya mwajiri na mfanyakazi yanajengwa kwenye mkataba wa
kazi. Lakini mkataba huu kwa sehemu kubwa hauingiwi kwa hiari (not
entered on equal footing), kukosekana kwa uhuru na hiari ya kuingia
kwenye mkataba huu kumefanya mkataba huu kwa sehemu kubwa
usitoe haki kwa wafanyakazi (weak party), aidha kukosekana kwa haki
kumefanya mahusiano ya wafanyakazi na waajiri kuwa yenye migogoro
(conflictual relationship).
Katika kuondoa migogoro hii, Marxists wanaamini kwamba ili kuondoa
migogoro, wafanyakazi wanatakiwa wachukue nguvu za uchumi
(dictatorship of proletariat), Unitary theorists wao wanasema dawa ya
kuondoa mfumo usiokuwa wa haki mahala pa kazi ni kuweka udhibiti
kwa kuweka maadili ya haki katika sheria za nchi na kuweka vyombo
vya udhibiti wa uvunjaji wa maadili hayo.
Sababu za mabadiliko ya sheria za kazi mwaka 2004
Mwaka 2004, Bunge la Tazania lilijadili na kisha kupitisha sheria mbili
muhimu sana zenye lengo la kutatua mambo ya kazi na ajira nchini.
Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004 na Sheria
ya Taasisi za Kazi namba 7 ya mwaka 2004.
Sheria hizi zinalinda na kudhibiti mambo tofauti tofauti yatokanayo na
uhusiano kati ya mwajiri na mwajiriwa, kutaja machache sheria hii
haimruhusu mwajiri kukatisha ajira au kumkata mshahara mwajiriwa
bila kufuata taratibu zilizoainishwa katika sheria husika. Pia ni muhimu
kuainisha kwamba sheria hizi hazina lengo la kumlinda mwajiriwa
mzembe, anayeshindwa kuwajibika kwa mujibu wa mkataba wa ajira au
matarajio ya mwajiri, ama yule aliye jeuri.
Sheria hizi zilitungwa kutatua changamoto kadhaa zilizokuwa zinaikabili
sekta ya ajira kwa wingi wa sheria zenye kuhusika na masuala ya kazi
zilizotangulia.
Mabadiliko ya sheria za kazi za mwaka 2004 yaliletwa na sababu
zifuatazo: –
1) Haki za msingi za mfanyakazi hazikuwemo katika sheria
2) Ulinzi kwa wafanyakazi ulikuwa hafifu
3) Sheria haikuwa imetambua na kuweka utaratibu unaofaa wa
majadiliano mahala pa kazi.
4) Vyombo vya utatuzi wa migogoro vilikuwa hafifu.
5) Vyombo vya kuzuia migogoro vilikuwa hafifu
6) Haki za kikatiba hazikuwa ndani ya sheria.
Malengo makuu ya sheria za kazi
Katika nchi yoyote duniani, kabla ya kufanya maamuzi (uamuzi) yoyote,
hususani yale yanayohusu mabadiliko ya sheria, lazima kuwepo kwa
malengo yatakayotoa dira ya mabadiliko ya sheria husika. Malengo
makuu ya sheria za kazi za mwaka 2004 ni yafuatayo:
1) Kuleta usawa na haki mahala pa kazi (social justice)
2) Kuinua uchumi (economic productivity)
3) Kuweka utaratibu unaofaa katika mahusiano, kuweka viwango vya
chini vya kazi na masharti ya kazi (ikiwamo flexibility of law).
4) Kuweka viwango vya kazi na masharti ya kazi.
5) Kuweka mfumo wa majadiliano (collective bargaining)
6) Kuweka mfumo bora wa utatuzi wa migogoro
7) Kutekeleza haki za kikatiba
8) Kutambua na kutekeleza mikataba ya kimataifa.
Muundo wa sheria za kazi
Malengo yaliyotajwa hapo juu yanaleta muundo ufuatao wa sheria za
kazi nchini: –
1) Sheria zinatoa ulinzi kwa wafanyakazi (Protective laws)
2) Sheria za uthibiti (regulative laws)
Mahusiano baina ya sheria za kazi (ELRA & LIA) na sheria za
utumishi wa umma (PSA na Public Service Regulation)
Sheria za kazi (ELRA na LIA) ni sheria za jumla (General Law) ambazo
zinapokea na kushughulikia watumishi wote yaani wa sekta binafsi na
sekta ya Umma ili hali sheria za utumishi wa Umma zina hadhi ya
(specific law) zinapokea na kushughulikia watumishi wa umma pekee.
Aidha sheria za kazi (ELRA na LIA) ni pana kwa aina ya malalamiko
yanayopokelewa na nafuu zilizotolewa. Mfano, tafsiri ya neno mgogoro
kwa mujibu wa marekebisho ya sheria Na. 6/2004 yaliyofanywa kupitia
Misc Act No. 8/2006, lalamiko linaweza likahusu uvunjaji wa sheria hii,
uvunjaji wa mkataba (Breach of Contract) ama lalamiko la
kusababishiwa madhara (tortious claim).
Sheria ya ajira na mahusiano kazini na sheria ya taasisi za kazi na
utekelezaji wake
Haki za msingi za mfanyakazi
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6/2004 inabeba haki za msingi
za wafanyakazi na mwajiri, kuanzia kifungu cha 5 hadi 11 sheria
imeweka haki za msingi mfano kuzuia ajira kwa watoto, ajira ya
kulazimishwa, ubaguzi, haki ya kushiriki, kuanzisha au kujiunga na
vyama vya wafanyakazi au waajiri.
Aidha, vyama vya wafanyakazi vina haki ya kuunda katiba zao bila
kuingiliwa na mwajiri, haki nyingine ni kujiunga na miungano ya vyama
vya wafanyakazi ndani na nje ya nchi.
Viwango vya ajira
Kuanzia kifungu cha 13 hadi 44, sheria imeweka viwango vya chini vya
haki mfano saa za kazi, kuwa na mikataba, kupewa likizo aina zote,
muda wa kupumzika katikati ya muda wa kazi, haki ya kupewa
mshahara uliopungua kima cha chini, haki ya kupinga kuachishwa, haki
ya kulipwa stahili mbali mbali pale mkataba wa kazi ukikoma.
Uanzishwaji na usimamizi vya vyama vya wafanyakazi
Kuanzia kifungu cha 45 hadi 74 ni eneo linalohusu uanzishaji wa vyama
vya wafanyakazi, usimamizi wa vyama vya wafanyakazi, haki za vyama
na jinsi ya kupata haki zao. Suala kubwa kabisa hapa ni jinsi vyama vya
wafanyakazi vinavyoweza kuinua maslahi ya wafanyakazi kupitia
chombo mahsusi kiitwacho collective bargaining ambayo kimsingi
inagawanyika katika sehemu mbili za productivity bargaining na
distributive bargaining. Mamlaka na uwezeshaji vyama vya wafanyakazi
vinao.
Makala hii itaendelea wiki ijayo…
Ends