Takribani watu 80 wameuawa nchini Nigeria katika jimbo la Benue tangu kuanza kwa mwaka huu mpya. Hiyo ni kwa mujibu wa ofisa wa wakala wa dharura.

Mapigano kati ya wafugaji wa jamii ya Fulani na wakulima yamekuwa yakiongezeka tangu mwaka ulipita yaani 2017 na huku maafisa wanasema mashambulizi bado yanaendelea.

Milipuko ya vurugu imekuwa ikitokea katika eneo la kati la Nigeria lakini mapigano hasa yamekuwa makali katika jimbo la Benue ambako watu 80 wameuawa na elfu 80 wakipoteza makazi yao.

Mapigano makali ya mara kwa mara kati ya wafugaji wa kiislam kutoka jamii ya Fulani na wakulima wakristo yamekuwa yakitokea katika eneo hilo kwa muda lakini yalipamba moto zaidi mwanzoni mwa mwaka huu mpya.

Katika mwezi wa Novemba, Benue ilipitisha sheria ya kuzuia ufugaji horera, jambo ambalo ni kawaida kwa wafugaji wa ng’ombe kutoka jamii ya Fulani, pia kiliundwa kikosi chenye silaha kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo.

Image caption Ufugaji holela katika jamii ya Fulani

Wakati mara nyingi mapigano haya huwa yanatokea kwa sababu ya kugombania ardhi, hivi sasa yanaonekana kuchukua sura mpya ya ukabila na tofauti za dini. Rais Muhammadu Buhari amemuagiza mkuu wa Polisi kuhamia Benue ili kuidhibiti hali hiyo.